loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wataalamu: Tuache kuwapa watoto chini ya miezi 6 vyakula

IMEELEZWA kuwa iwapo mama ataanza kumpatia vyakula mtoto ambaye hajafikisha miezi sita anaweza kumsababishia magonjwa ikiwemo utapiamlo na kuharibu mfumo mzima wa makuzi yake.

Pia, watoto wanapoumwa au kuonesha dalili za kuumwa wazazi wanapaswa kuwakimbiza hospitalini badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao huweza kuharibu mfumo wa makuzi yao.

Hayo yamebainishwa na wataalamu wakati wa kongamano la afya ya mama na mtoto lililoandaliwa na Mradi wa USAID ‘Tulonge Afya’ kwa ajili ya kuwapatia elimu ya makuzi ya watoto wanawake wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza jana.

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Bertha Yohana alisema kumekuwapo na changamoto ya afya ya makuzi ya watoto kutokana na mila, tabia na desturi za jamii kushindwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.

“Tumekuwa na tabia kwenye jamii wanafundishana wao kwa wao, wapo wanaoamini kwamba mtoto akinyonya maziwa ya mama pekee hashibi, jambo hili sio kweli, mtoto anaweza kunyonya maziwa ya mama akashiba bila kula chakula kingine mpaka afikishe miezi sita,”alisema.

Alisema wakati mwanamke anapokuwa ananyonyesha mtoto mchanga anatakiwa asiwe na msongo wa mawazo, ale ashibe ili aweze kuzalisha maziwa ya kutosha.

Naye mhudumu ngazi ya jamii kata ya Mhandu, Rachael Mahulu alisema hakuna budi jamii ikaondokana na mila potofu za kutaka kuwalisha watoto wadogo vyakula na dawa kwa misingi ya kuwakuza kumbe kufanya hivyo wanawaharibu.

Naye Ofisa Uwanda kutoka mradi wa USAID Tulonge afya wilaya ya Nyamgana, Esuphvat Lewis alisema katika kongamano hilo wamefundisha tabia nne za kiafya katika makuzi ya mtoto ambayo ni pamoja na unyonyeshaji wa maziwa kwa kipindi cha miezi sita.

Zingine ni kuhakikisha mama analala na mtoto kwenye chandarua kimoja angalau mpaka afikishe miezi tisa, mama akiona dalili zozote hatarishi ampeleke mtoto hospitalini na njia za uzazi wa mpango baada ya mtoto kufikisha miezi 24.

Alisema katika mafunzo hayo jumla ya wanawke 50 wameshiriki kutoka kata za wilaya ya Nyamagana.

Nao baadhi ya wanawake walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Ester Suleiman kwa nyakati tofauti walisema  mafunzo hayo yameweza kuwafungua na kutambua mambo muhimu katika makuzi ya mtoto ambayo walikuwa hawayajui awali.

“Nimejifunza unyonyeshaji wa mtoto na jinsi ya kumlinda na malaria, kuna changamoto kubwa wanawake wengi wanashauriana kuwapa watoto uji hasa wa udaga kumbe unaweza kumsababishia matatizo makubwa,” alisema Mkazi wa Igoma, Tatu Ramadhani.

Mradi huu ambao unafahamika kama Mothers Meets Up events unafanyika katika wilaya 27 za  Tanzania kupitia majukwaa ya watu wazima ya ‘Naweza’ chini ya mradi wa Tulonge afya Tanzania.

Lengo ni kuhamasisha huduma bora za afya kwa ngazi ya familia na jamii kwa kuondoa mila potofu na kuwapatia mbinu za kiafya kujikinga na maradhi kama ukimwi , malaria, uzazi wa mpango na afya ya uzazi pamoja na ugonjwa wa kifua kikuu.

Waziri Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi wetu, Mwanza

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi