loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wajue waoruhusiwa kupiga kura nje ya vituo walivyojiandikisha

OKTOBA 28, mwaka huu Watanzania watapiga kura ya kuchagua viongozi wanaowataka ambao watawaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo. Upigaji kura ni zoezi muhimu katika msingi wa kuimarisha demokrasia.

Zoezi hili litahusisha wananchi wote wenye sifa za kupiga kura. Sifa kubwa ni lazima uwe umejiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura katika kituo husika na pia uwe na kadi ya kupigia kura katika kituo hicho.

Kwa muktadha huo, kila mtu atapiga kura katika kituo alichojiandikisha.

Ili kuhakikisha kuwa kila mtu anapiga kura kwenye kituo alichojiandikisha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura mwaka 2019/2020.

Lengo la uboreshaji wa daftari hilo lilikuwa ni kuandikisha wapigakura wapya kwa maana ya wale ambao hawakujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura mwaka 2015, waliotimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo ifikapo Oktoba 2020.

Uboreshaji huo pia ulilenga kuondoa wapigakura waliokosa sifa kama vile waliofariki, kuboresha taarifa za wapigakura waliohama makazi yao kwa maana ya jimbo au kata na waliopoteza au kadi zao kuharibika.

Katika kufanikisha hilo, Tume ilitoa elimu ya mpigakura pamoja na matangazo ili kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi wajitokeze kujiandikisha au kuboresha taarifa zao, katika vituo ambavyo watapigia kura wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu ili waweze kupata haki yao ya kikatiba.

Vilevile, kabla ya tarehe ya uchaguzi Tume itabandika orodha ya wapiga kura katika vituo vyote vya kupigia kura ili kutoa fursa kwa wapigakura kukagua orodha hiyo na kufahamu vituo watakavyopigia kura.

Hivyo, ni wale tu watakaorodheshwa katika kituo husika na wenye kadi za kupigia kura ndio watakaoruhusiwa kupiga kura katika kituo hicho.

Ikiwa mtu ataona jina lake lakini hana kadi ya kupigia kura basi hataruhusiwa kupiga kura isipokuwa, kama Tume itaamua vinginevyo kama vile kuruhusu matumizi ya vitambulisho mbadala kwa wale waliopoteza kadi zao kama ilivyoruhusu katika chaguzi ndogo zilizopita.

Kwa minajili hiyo, mpigakura atapaswa kupiga kura katika kituo alichojiandikisha tu.

Ni vema kujiuliza je, vipi kwa watendaji wa vituo vya kupigia kura ambao wanafanya kazi nje ya vituo walivyojiandikisha, pamoja na wagombea ambao wanafuatilia mchakato wa uchaguzi katika vituo mbalimbali katika kata au majimbo wanayogombea?

Tume kwa kutambua mazingira hayo, imeruhusu watendaji wa uchaguzi, mawakala wa upigaji kura pamoja na wagombea kupiga kura nje ya vituo walivyojiandikisha kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

Watendaji wa uchaguzi ni msimamizi wa kituo, wasimamizi wasaidizi wa vituo pamoja na makarani waongozaji. Hawa kisheria wanaruhusiwa kupiga kura nje ya vituo walivyojiandikisha.

Watendaji pamoja na mawakala wa upigaji kura watapaswa kufuata utaratibu uliowekwa ambapo watawasiliana na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi ili wapewe kibali maalumu (fomu Na. 18) kitakachowaruhusu kupiga kura nje ya vituo walivyojiandikisha, yaani katika vituo watakavyofanyia kazi.

Fomu hizo zinapaswa kujazwa na kukabidhiwa mapema kabla ya siku ya uchaguzi na lazima zisainiwe na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

Fomu Na. 18 ina sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza itajazwa na mtendaji wa uchaguzi (msimamizi wa kituo, wasimamizi wasaidizi wa kituo au karani mwongozaji) au wakala wa upigaji kura kwa kuandika taarifa zake binafsi. Sehemu ya pili ya fomu hiyo itajazwa na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwa kuweka sahihi yake na kugonga muhuri.

Fomu hiyo itakuwa halali kama tu imesainiwa na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi pamoja na kugongwa muhuri, na ikiwa fomu hiyo haitasainiwa na wahusika waliotajwa au kutogongwa muhuri itakuwa batili na hivyo hataruhusiwa mtu huyo ambaye fomu yake haijasainiwa au kupigwa muhuri wa msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kupiga kura.

Wakati wa kupiga kura fomu hizo watamkabidhi msimamizi wa kituo ambapo atazikagua na kuzihifadhi sehemu husika na kuwapa karatasi za kura wahusika ili wapige kura.

Hata hivyo, ikiwa mtendaji wa uchaguzi au wakala anafanya kazi katika kituo chochote cha kupigia kura kilichopo ndani ya kata aliyojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ataruhusiwa kupiga kura ya Diwani, mbunge na rais.

Ikiwa mtu huyo yupo nje ya kata aliyojiandikisha basi hatapiga kura ya diwani na badala yake atapiga kura ya mbunge na rais tu.

Vivyo hivyo kwa upande wa wagombea watapaswa kujaza fomu Na. 19 ili waweze kupiga kura nje ya vituo walivyojiandikisha.

Aidha, mgombea udiwani ataruhusiwa kupiga kura ndani ya kituo chochote katika kata anayogombea na kuchagua diwani, mbunge pamoja na rais. Mgombea udiwani hataruhusiwa kupiga kura nje ya kata anayogombea.

Mgombea ubunge ataruhusiwa kupiga kura katika kituo chochote ndani ya jimbo analogombea. Ikiwa mgombea huyo atapiga kura katika kituo kilichopo ndani ya kata aliyojiandikisha atapiga kura ya kumchagua diwani, mbunge pamoja na rais.

Ikiwa mgombea ubunge atapiga kura katika kituo kilichopo nje ya kata aliyojiandikishia hatoruhusiwa kupiga kura ya diwani na badala yake atapiga kura ya mbunge na rais tu. Mgombea ubunge pia hataruhusiwa kupiga kura nje ya jimbo analogombea.

Aidha, mgombea urais ataruhusiwa kupiga kura ya kumchagua diwani, mbunge na rais ikiwa atapiga kura ndani ya kituo chochote kilichopo katika kata aliyojiandikisha.

Ikiwa atapiga kura katika kata ambayo hakujiandikisha lakini ndani ya jimbo alilojiandikisha ataruhusiwa kupiga kura ya mbunge na rais tu, hatoruhusiwa kupiga kura ya diwani.

Kama mgombea urais atapiga kura nje ya jimbo alilojiandikisha hataweza kupiga kura ya diwani wala mbunge bali atapiga kura ya rais tu.

Ni muhimu kwa kila mpigakura kukagua mapema orodha ya wapigakura katika kituo alichojiandikisha mara Tume itakapoweka wazi orodha hiyo vituoni, ili kufahamu mahali atakapopigia kura. Pia kila mpigakura anawajibika kutunza kadi yake ya kupigia kura ili aweze kutekeleza haki yake ya kikatiba Oktoba 28, 2020.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

 

 

foto
Mwandishi: Subira Kaswaga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi