loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaunga mkono mpango wa NBC

SERIKALI imeunga mkono mpango wa Benki ya NBC kuwasafirisha wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa sekta ya madini nchini katika mataifa yanayofanya vizuri kwenye sekta madini.

Watapelekwa kwenye nchi za Zimbabwe, Ghana na Msumbiji ili kujifunza na kutafuta namna bora zaidi ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kwa kiwango cha kimataifa.

Akizungumza wakati alipotembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya Dhahabu na Teknolojia yanayoendelea katika viwanja vya Mombambili mkoani Geita, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema, serikali ipo tayari kushirikiana na benki hiyo kufanikisha ziara hizo ikiwa ni pamoja na kushauriana na wadau wote wakiwemo wachimbaji hao ili kuongeza tija.

Ili safari hizi ziwe na tija zaidi kwa walengwa, serikali ipo tayari kushirikiana na pande zote wakiwemo wachimbaji ili kufahamu nchi sahihi zilizofanya vizuri katika sekta hii, ili walengwa wapate wasaa wa kujifunza mambo yatakayowasaidia zaidi hivyo nawapongeza NBC kwa mpango huu, alisema.

Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Binafsi wa NBC, Elibariki Masuke, alisema mpango huo umetokana na mafunzo maalumu ya siku tatu yaliyotolewa na benki hiyo kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali katika sekta ya madini yaliyofanyika katika maonesho hayo.

Malengo ya safari hizo hasa ni kutusaidia sisi sote yaani Benki ya NBC na wateja wetu kwenye sekta ya madini ili kwa pamoja tukabadilishane uzoefu na wenzetu ambao pia wanafanya vizuri kwenye sekta hii, alisema.

Akaongeza: Kupita safari hizo, tunatarajia makundi haya mawili ya wachimbaji yatajifunza namna mpya na bora zaidi ya kuendesha biashara zao ikiwemo namna ya kulifikia soko.

Alisema kupitia mafunzo hayo, benki hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wamebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wadau hao, hivyo kuwajengea uelewa wa namna ya kukabiliana nazo wao wenyewe huku pia benki hiyo ikiahidi kutumia changamoto hizo katika kubuni huduma mahususi zinazolenga kuziondoa kabisa.

NBC ipo katika hatua za mwisho kuzindua huduma maalumu kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini nchini ambayo kwa kiasi kikubwa inalenga kujibu changamoto zilitajwa na wachimbaji wadogo pamoja na wajasiriamali wakati wa mafunzo yetu, alisema.

Kwa mujibu wa Masuke, wakati huduma hiyo mpya kwa wadau wa sekta ya madini ikiwa katika hatua za mwisho kabla ya kuzinduliwa, benki hiyo imeendelea kuwahudumia wadau hao kupitia huduma zake.

Kupitia klabu ya biashara, tumekuwa tukiandaa safari za ndani na nje ya nchi, ikiwemo China ambapo wateja wetu wamekuwa wakikutanishwa na wawekezaji mbalimbali, hivyo kuanzisha uhusiano wa kibiashara uliowaletea tija katika shughuli zao, alisema.

MCHICHA ni aina nyingine za ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Geita

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi