loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaotafuta ubunge kupitia kwa waganga wahadharishwa

ASKOFU wa Kanisa la Pentecostal Holiness Association Mission Tanzania, Kanda ya Kati, Julias Bundala amesema nafasi za ubunge hazipatikani kupitia kwa waganga wa kienyeji.

Kiongozi huyo alitoa onyo hilo wakati wa mahuburi katika ibada ya kuweka wakfu viongozi mbalimbali wa kanisa hilo watakaotumikia kwa miaka minne, iliyoambatana na semina ya siku nne ya wanawake wa kanisa hilo iliyofanyika Makole Jijini hapa.

Alisema Watanzania wana imani kubwa kwa Mungu, hivyo viongozi watakaochaguliwa wawe wale wenye kunadi sera zao kwa ajili ya maendeleo ya nchi na sivyo vinginevyo.

Bundala alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kuna baadhi ya wagombea wanaotafuta sera zao kwa waganga wa kienyeji ili waweze kuchaguliwa kwenye nafasi wanazoziomba.

"Tunataka kuwaambia kuwa kura za haki zinapatikana kutokana na sera zitakazowahamasisha Watanzania kuwachagua na siyo huko wanakokwenda kwa waganga wa kienyeji ili wapatiwe viungo vya binadamu," alisema.

Bundala alisema hayo na kuwapongeza Watanzania wanaoendelea kuombea uchaguzi huo ili uweze kuwapata wagombea wacha-Mungu lakini akaomba pia uchaguzi huo kufanyika kwa haki, huru na amani.

Alisema Tanzania tegemeo lao kubwa la kuwapata viongozi lipo kwa Mungu na ndiyo maana viongozi wetu wa serikali kwa kushirikiana na makanisa wamekuwa wakisisitiza kuombea uchaguzi huo utakaofanyika mwaka huu wa 2020.

Askofu Bundala pia alisema kanisa hilo halitawavumilia viongozi wa namna hiyo wanaojihusisha na nguvu za giza, ambao badala ya kunadi sera na mikakati ya maendeleo wao mawazo yao wanawategemea washirikina.

"Tumekuwa tukishuhudia katika kipindi cha uchaguzi yanatokea mambo mbalimbali ya kusikitisha baadhi ya wagombea kujihusisha na imani potofu za ushirikina ili waweze kuzipata nafasi hizo za uongozi, sasa sisi kama kanisa tutahakikisha tunamwomba Mungu nafasi wanazoziomba kamwe wasizipate hata kama wamepitishwa," alisema.

Aidha Askofu Bundala aliwataka wagombea wa vyama hivyo vya siasa kwenye kampeni zao kutumia nafasi hizo kueleza sera zitakazowashawishi Watanzania ili kuchaguliwa badala ya kujinadi kwa lugha chafu, vitisho, kejeli kwa kuwa Watanzania wanahitaji maendeleo na sivyo vinginevyo.

 

Aidha Askofu huyo pia aliwaomba Watanzania kuhakikisha wanawachagua viongozi ambao wanaoonesha nia za dhati kulitetea Taifa hili juu ya rasilimali zake zilizopo kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote.

“Tanzania tunazo rasilimali nyingi na za kutosha, kwa sasa kuna wagombea wengi ambao wananadi sera zao lakini nawaomba Watanzania wasikilizeni wagombea wote na chagueni watu ambao kimsingi wanaonesha nia ya kusimamia haki na maendeleo ya watu ili kuweza kuwafanya watanzania wote wawe wanufaika na rasilimali zilizopo.

Askofu Bundala alivitaka vyombo vyote vya usalama pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha inatenda haki kwa vyama vyote bila kupendelea chama chochote cha siasa ili kuepusha malalamiko ambayo yanaweza kujitokeza.

Alisema ili kuiweka nchi katika usalama ni lazima haki itendeke kwa vyama vyote na yule ambaye ataonekana kuwa ameshinda kwa kupigiwa kura atangazwe, na vyombo vya dola vya kulinda usalama wa raia na mali zake ili kutenda haki kwa vyama vyote kwa kutimiza sheria, taratibu na kanuni zao za kazi.

BODI ya Korosho nchini (CBT) imesema taarifa zinazogaa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi