loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

ACT wavurugana, Chadema kujieleza kwa Msajili

WAKATI ukiwa umebaki mwezi mmoja na siku kadhaa kumaliza kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Chama cha ACT-Wazalendo kimeanza kuvurugana baada ya viongozi wake kukinzana kuhusu mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hali hiyo imejitokeza baada ya Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kumnadi mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akieleza kuwa anaamini ndiye atakayeshinda urais wakati wanaye mgombea wao, Bernard Membe.

Sambamba na hilo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekiandikia barua ya kujieleza Chadema kwa kitendo chake cha kumnadi Maalim Seif wa ACT Wazalendo, jambo ambalo ni kwenda kinyume cha sheria.

Pamoja na hayo, ofisi hiyo imeeleza bayana kuwa kwa sasa hakuna chama chochote cha siasa kinachoweza kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu, na endapo vitafanya hivyo vitakuwa vimefanya makosa ya kisheria.

Akiwa katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Mpira wa Mwanakombo Jimbo la Mahonda Wilaya ya Kaskazini B Unguja juzi, Maalim Seif alisema hana wasiwasi kuwa Lissu atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Imani yangu Lissu atakuwa Rais wa Tanzania na mimi nitakuwa wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, Membe aliandika kuwa yeye ndio mgombea urais wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo.

“Mimi ndiyo Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT- Wazalendo. Mimi ndiye niliyekabidhiwa Ilani ya Chama hicho kuinadi kote nchini kwenye uchaguzi huu. Taarifa zinazosambaa kuwa tayari tumejiunga na Chadema katika ngazi ya Urais siyo za kweli,” aliandika Membe ambaye Agosti 5, mwaka huu Mkutano Mkuu wa ACT ulimpitisha kuwa mgombea wa nafasi hiyo.

Septemba 8, mwaka huu, Membe pia aliandika kwenye twitter yake kuwa wanaodhani atajitoa katika kugombea nafasi hiyo wanaota ndoto za mchana.

 

“Hatoki Mtu Hapa! Wale wote wanaodhani kuwa nitajiondoa katika kinyang'anyiro cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT Wazalendo, wanaota ndoto za mchana. Kimbunga kitakachoanza Septemba 15, 2020 hadi Oktoba ni kimbunga kumba-kumba! Watanzania kaeni chonjo!” aliandika Membe.

Pamoja na hayo, kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto naye aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa unahitajika uamuzi mgumu na wa kishujaa wa viongozi wa vyama vya upinzani ili kumshinda mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli.

“Kumtoa Magufuli kunahitaji maamuzi magumu na ya kishujaa kutoka viongozi wa vyama vya upinzani. Bila kuunganisha nguvu hatoki,” aliandika Zitto.

Aidha, kupitia kipindi cha AMKA na BBC katika mahojiano yake jana asubuhi, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Nassor Mazrui alisema kuna mazungumzo yanaendelea baina ya chama hicho na Chadema kuhusu namna ya kushirikiana kuelekea Oktoba 28, mwaka huu, siku ambayo kura za kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani zitapigwa.

Hatua ambayo hata hivyo, inapingwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambaye alieleza kuwa kwa sasa haiwezekani kwa vyama vya siasa kushirikiana na endapo vitafanya hivyo, vitafanya makosa ya kisheria lakini pia kuonea vyama vingine vilivyobaki.

Nyahoza alisema kutokana na kosa kama hilo, tayari ofisi yake imekiandikia Chadema barua ya kukitaka kujieleza kwa kitendo chake cha kumnadi Maalim Seif Zanzibar na Zitto Kigoma. “Tunataka wajieleze huo ushirikiano ukoje na ACT,” alieleza.

Alisema kwa mujibu wa sheria vyama hivyo kama vilitaka kushirikiana vilitakiwa kufuata utaratibu kabla ya uchaguzi kwa maana ya kufanya mkutano wa makubaliano, waingie mkataba wa makubaliano na kuukabidhi mkataba huo wa makubaliano kwa msajili miezi mitatu kabla ya uchaguzi.

 

“Wakishirikiana kwa sasa itakuwa si tu ni makosa bali si vizuri hata kwa wenzao walioajiandaa na kujinadi halafu wao ghafla tu waanze kushirikiana,” alifafanua.

 

Sheria inayoruhusu kushirikiana kwa vyama vya siasa ni Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 11 (a).

Tafsiri ya sheria hiyo inaeleza kuwa kifungu cha 11 (a) vyama viwili au zaidi vya siasa vilivyosajiliwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria vinaweza kushirikiana kabla au baada ya Uchaguzi Mkuu na vinatakiwa kuwasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa makubaliano ya ushirikiano huo.

Kifungu hicho pia kinabainisha kuwa uamuzi wa kushirikiana lazima ufanyike kupitia mkutano mkuu wa kila chama cha siasa kinachotaka kushirikiana na makubaliano yafanyike kimaandishi.

Aidha, kinafafanua kuwa makubaliano ya ushirikiano yatakayofanyika kabla ya uchaguzi yanatakiwa kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa angalau miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu, wakati yale makubaliano yatakayofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu yatawasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ndani ya siku 14 baada ya kusainiwa.

Agosti 5, mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam, vyama vya siasa vya upinzani vilisema haviwezi kuiondoa CCM madarakani bila nguvu ya pamoja katika kusimamisha wagombea akiwemo wa urais wa Tanzania na urais wa Zanzibar.

Viongozi wa vyama hivyo walisema wapo tayari kuunganisha nguvu katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili kuiondoa CCM madarakani na wakakiri kuwa, kama hawatashirikiana wasahau ushindi.

Katika mkutano huo Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Haji Ambar alisema Katiba ya chama hicho inaeleza kuhusu ushirikiano wa vyama na kusisitiza kuwa wapo tayari kwa hilo.

Mwakilishi wa Chauma, Mohamed Masoud Rashid alisema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na kuvitaka vyama viungane.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu alisema chama hicho kinaamimi vyama vya siasa vitakwenda kwenye kushirikiana na si kuungana.

 

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi