loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

ATCL yashauriwa kuanzisha safari za Geita-Dar

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imesema maonesho ya tatu ya kimataifa ya teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini mkoani Geita yamewasaidia kuwafikia wateja wa Kanda ya Ziwa wakiwemo wafanyabiashara ya madini ambao wamevutiwa na huduma ya usafiri wa kampuni hiyo.

Akizungumza na HabariLEO kwenye maonesho hayo jana, Mkuu wa ATCL Kituo cha Mwanza, Hamid Mwikombe alisema watu wengi wakiwemo wafanyabiashara ya madini wameitaka ATCL kuanzisha haraka safari za moja kwa moja kutoka Geita hadi Dar es Salaam ili kurahisisha biashara yao ya madini.

Mwikombe alisema baadhi ya wafanyabiashara ya madini wamesema kukosekana kwa usafiri wa moja kwa moja wa ndege kati ya Geita na Dar es Salaam kunawafanya kuchukua muda mrefu kufika Dar es Salaam na kuunganisha ndege kwenda Dubai ambako kuna soko kubwa la dhahabu.

“Tumeyapokea maoni yenu na tutayafanyia kazi mapema, lakini kwa sasa tungependa pia wajue safari tunazofanya ndani na nje ya nchi; ndege za ATCL zinafanya safari kati ya Dar es Salaam-Bukoba, Dar es Salaam-Mwanza na Dar es Salaam-Mbeya,”alisema Mwikombe.

Alizitaja safari nyingine ambazo ATCL inazifanya ni pamoja na Dar es Salaam-Iringa, Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza na kurudi, Dar es Salaam-Kilimanjaro-Zanzibar, Dar es Salaam-Katavi, Dar es Salaam-Kigoma na Dar es Salaam-Dodoma.

Mwikombe alisema kwa barani Afrika ndege za ATCL zinafanya safari kati ya Dar es Salaam na Bujumbura, Dar es Salaam-Entebbe, Dar es Salaam-Comoro, Dar es Salaam-Lusaka-Zimbabwe na kurudi.

“Nje ya Afrika, ndege za ATCL zinafanya safari za Dar es Salaam-Mumbai nchini India,”alisema.

 

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Geita

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi