loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Abbasi: Hakuna usiri wowote fedha za miradi

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi amesema fedha zote za miradi inayotekelezwa nchini, zipo kwenye bajeti na zinapitishwa na Bunge kila mwaka na hakuna usiri wowote kwenye miradi hiyo ukiwamo wa fedha.

Amebainisha kuwa hadi sasa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani umeshatumia Sh trilioni 1.432. Utagharimu Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika 2022.

Dk Abbasi alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Kituo cha Redio cha Times FM na kusema wakati wanasiasa wakiendelea na kampeni za Uchaguzi Mkuu, serikali inaendelea na kazi mbali mbali kama zilivyopangwa. Alisema sheria za nchi zipo na wasemaji wa nchi nao wapo, kuzungumzia masuala yote yanayohitaji ufafanuzi.

“Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea, serikali iko kazini inaendelea kazi ya maendeleo, wasemaji wako, kama ukitugusa na uongo wako tutakujibu,” alisema Dk Abbasi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alisema miradi yote nchini inayotekelezwa, fedha zake zipo na zimetengwa kwa mujibu wa sheria na zilipitishwa na Bunge. Alitoa mfano wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliopo kwneye kwamba ulitengewa fungu 2005 na mradi wenyewe ni namba 4281 kwenye sekta ya uchukuzi na Bunge ndilo lililopitisha.

“Pamoja na nchi kuwa katika kipindi cha kampeni, lakini kuna wageni wengi nchini kwa sasa kwa hiyo tuwavumilie, mtu anahoji hela za SGR hazijulikani zinatoka wapi, nataka tuamini yeye ndio hajulikani ametoka wapi na anataka nini, anayehoji hii fungu 2005, mradi namba 4281 kwenye Sekta ya Uchukuzi aone kila mwaka Bunge liliidhinisha shilingi ngapi kwa miradi ya SGR kuanzia mwaka 2017/18,” alisema Dk Abbasi na kuwataka Watanzania kuwapuuza waropokaji wanaoumizwa na maendeleo yanayotokea.

Alisema miradi inayoendelea mikubwa na midogo, imelenga kuboresha maisha ya Watanzania na iko kwenye hatua nzuri na kuwa serikali itaendelea kutoa takwimu za kila mara kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.

Akijibu hoja kuhusu usiri katika ujenzi wa reli ya SGR na Mradi wa Umeme Rufiji na fedha zinakotoka, Dk Abbasi alisema taratibu zote zilifuatwa kwa kushindanisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.

“Hakuna usiri wowote kwenye miradi hii, vipande vyote vya ujenzi wa reli ya SGR na Mradi wa Umeme wa Rufiji vilishindanisha wataalamu wa ndani na nje. Mfano, Mradi wa SGR-Dar kwenda Moro walijitokeza washindani zaidi ya 40, na Moro kwenda Makutupora walijitokeza washindani takribani 36,” alibainisha Dk Abbasi.

Alisema na tayari kuna zabuni ilitangazwa Agosti mwaka huu ya ujenzi wa kipande cha reli hiyo kutoka Mwanza kwenda Isaka.

Kuhusu Mradi wa Umeme Rufiji, alisema zabuni ilitangazwa wazi na takribani kampuni nne zilishiriki kutoka mataifa ya Afrika, Ulaya na Asia.

Akizungumzia fedha za ununuzi wa ndege, Dk Abbasi alisema suala hilo limeshatolewa ufafanuzi mara nyingi na kusema ununuzi wa ndege hizo umeshatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 400 za moja kwa moja na mapato yatokanayo na uwepo wake yameongezeka kutoka Sh bilioni  2.5 kwa mwezi hadi Sh bilioni 15 kwa mwezi.

Kuhusu madai kuwa ununuzi wa ndege hizo umefanywa kwa usiri na bila kuwepo kwa bajeti yake, Dk Abbasi alisema ununuzi ulifanywa kwa mujibu wa Kifungu kipya cha 65A cha Sheria ya Ununuzi wa Umma (marekebisho ya 2016) ambayo inaruhusu kwa nia ya kupata bei bora na thamani ya fedha, taasisi ya ununuzi kununua moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji wa bidhaa husika badala ya mawakala wanaopandisha bei.

“Kama kuna mtu alikuwa na wakala wake mfukoni katika ununuzi wa hizi ndege imekula kwao, Serikali imenunua moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wanaojulikana kimataifa kama Boeing na Bombardier na sheria inaruhusu hivyo na ilipata bei ya chini kuliko hata zile zilizoainishwa kwenye tovuti zao,” alieleza.

Alisema bajeti za mwaka 2016/17, 2017/18 na 2019/20 kutoka Fungu 2006 na mradi namba 4294 (Ununuzi wa ndege mpya - ATCL), takribani miaka minne mfululizo, serikali imekuwa ikitenga wastani wa Sh bilioni 500 kwa mwaka.

Alisema fedha hizo zinajadiliwa na zinapitishwa na Bunge kupitia fungu hilo, na kushangaa wanaodai kuwa fedha za ndege hazijulikani zinatoka wapi kama ni watu wanaoishi Tanzania au ndio wamekuja nchini juzi kushangaa.

Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mambo makubwa yenye kuwanufaisha Watanzania na kuwataka wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao na kuwakataa mabeberu na mawakala wao.

 

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi