loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaonyonyesha waelimishwa kulisha watoto

“KATIKA Mkoa wa Iringa tulikuwa na changamoto ya mila na desturi kwani wazazi walikuwa wakishinikizwa na wanafamilia yaani bibi au majirani kwamba, mtoto akilia anapaswa kupewa uji au hata maji kwa madai kuwa maziwa ya mama pekee hayatoshi, lakini kwa sasa wengi wameelewa na utekelezaji ni karibu asilimia 100.”

Ndivyo alivyosema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Dk Jesca Leba wakati akizungumza katika kongamano la ‘Mothers Meet Up Event’ maalumu kwa akinamama wanaonyonyesha lililoandaliwa na mradi wa ‘USAID Tulonge Afya’ kuwakumbusha malezi bora ya watoto wao.

Aliwataka akinamama wanaojifungua kufuata maelekezo ya wataalamu kwa kutowaongezea chakula chochote watoto wao hadi watakapofikisha miezi sita ili kulinda afya zao.

Kwa mujibu wa Dk Leba, watoto wanapozaliwa hawapaswi kupewa chakula kingine chochote tofauti na maziwa pekee ya mama kwa kuwa nyongeza hiyo ya chakula huathiri afya na ukuaji wao kimwili na kiakili.

Kutokana na kuwapo kwa baadhi ya mila na desturi zisizo sahihi, Dk Leba alisema awali kampeni hiyo ilisuasua, lakini kwa juhudi za serikali na wadau kutoa elimu zaidi, jamii imeelewa na kuanza kufuata utaratibu wa kunyonyesha watoto kwa miezi sita ya kwanza bila kuwapa chakula au kinywaji kingine chochote.

Alisema kwa mujibu wa takwimu walizonazo, kwa sasa unyonyeshaji bila nyongeza ya chakula kwa miezi sita unakaribia asilimia 100.

Katika kongamano hilo, Theresia Joseph ambaye ni mzazi wa watoto wawili alisema: “Nilipojifungua ndani ya kipindi cha wiki mbili, mtoto wangu wa kwanza alikuwa analia sana; ndipo nikaambiwa nimwongezee chakula kwa madai kuwa maziwa yangu yalikuwa hayatoshi.”

Anaongeza: “Lakini nilikataa na kuendelea kumnyonyesha mwanangu mpaka alipofikisha miezi sita ndipo nikaanza kumwongezea vyakula na mpaka sasa ana afya njema.”

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa Manispaa ya Iringa, Sezaria Andrew, alisema pamoja na hamasa iliyofanywa na serikali kuhakikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita unazingatiwa, mchango wa wadau si wa kubezwa katika mafanikio yaliyofikiwa kwenye kampeni hiyo.

“Tunawashukuru wadau wetu USAID Tulonge Afya kwani wamekuwa kiungo kikubwa katika kampeni hii hata kutufikisha kwenye mafanikio haya. Tunawaomba waendelee kutuunga mkono ili tuendelee kupambana kwa ajili ya ustawi wa mtoto wa Kitanzania,” alisema Sezaria.

Mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa yenye udumavu wa watoto ukiwa na asilimia 47 licha ya kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi. Hali hii inadaiwa kutokana na mila na desturi mbaya.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Iringa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi