loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Masoko kuongeza mikopo kwa wachimbaji wa madini

SERIKALI imesema uanzishwaji wa masoko ya madini hapa nchini imekuwa ni moja ya njia muhimu itakayoongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo huku ikiipongeza Benki ya NBC kwa namna ilivyojipanga kuwasaidia wachimbaji hao kupitia mafunzo ya kiutendaji na fursa ya mikopo.

Akizungumza  kwenye Kongamano la Fursa za Uwekezaji na Biashara kwenye Maonesho ya Madini na Teknolojia yanayofanyika mkoani Geita, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kupitia masoko hayo, wachimbaji hao wanauza madini kwa uwazi huku taarifa za mienendo ya biashara zao zikitoa fursa kwa taasisi za fedha kuwapatia mikopo.

“Tunaamini uwepo wa taarifa za mienendo ya biashara za wachimbaji wadogo kwenye masoko yetu ya madini utazisaidia sana taasisi zetu za kifedha ikiwemo Benki ya NBC ambayo imeonesha nia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo  ili waweze sasa kupata mikopo hususani baada ya kuwafanyia mafunzo kupitia maonesho haya,’’alisema.

Zaidi, aliitaka migodi yote nchini kuhakikisha inatoa ushirikiano na taasisi za fedha katika masuala ya huduma za kibenki pamoja na kuwasaidia wazabuni wa migodi hiyo kupata nyaraka muhimu zitakazosaidia taasisi za kifedha kuweza kuwapatia mikopo wanapohitaji ili kuboresha huduma wanazotoa kwa wateja wao.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema hatua ya taasisi za kibenki kuanza kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo ni dalili nzuri kuelekea mabadiliko ya kiuchumi kwa wachimbaji hao pamoja na serikali kwa ujumla kwa kuwa kupitia mikopo hiyo si tu inawaongezea mitaji wachimbaji hao, bali pia inaambatana na mafunzo maalumu yanayowawezesha kufanya shughuli zao kwa ubora zaidi.

“Mfano mzuri ni mafunzo yaliyotolewa na Benki ya NBC kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali. Tafsiri yake hawa watu si tu watajengewa uwezo kifedha, bali pia watakuwa na uelewa wa kutosha katika kufanya shughuli zao,’’alisema Gabriel huku pia akitoa angalizo kwa taasisi za kifedha kufanya uchambuzi wa kina katika utoaji wa mikopo hiyo.

Akiwasilisha mada kuhusu uwekezaji kupitia benki katika kongamano hilo, Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje aliiomba serikali itoe msukumo zaidi  kwa migodi mikubwa nchini kuhakikisha inatoa mikataba ya uhakika kwa watoa huduma wake ili iwe rahisi kwa taasisi za kifedha kutumia mikataba hiyo kama dhamana ya mikopo kwa watoa huduma hao.

“Benki ya NBC tuna huduma ya utoaji wa mikopo isiyo na dhamana kwa wazabuni wa makampuni mbalimbali ila tunachohitaji ni kuona kwamba huyu mzabuni tunayempatia mkopo anathibitisha uhalali na thamani ya zabuni yake kupitia mkataba na ndio maana tunaomba sana uongozi wa migodi utusaidie katika hili sababu hawa wazabuni wanapojengewa uwezo wa kifedha wanaboresha pia huduma zao katika migodi husika,’’alifafanua.

Bitababaje aliipongeza serikali kwa kusimamia vema uanzishwaji wa masoko ya madini nchini huku akibainisha kuwa pamoja na masoko hayo kuwasaidia wachimbaji wadogo katika biashara zao za madini uwepo wa masoko hayo pia unarasimisha mienendo ya hali ya kifedha ya wachimbaji hao taarifa ambazo zinaweza kuwa msaada mkubwa kwa taasisi hizo katika utoaji wa mikopo.

foto
Mwandishi: Mwandishi wetu, Geita

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi