loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana watakiwa kuchangamkia fursa Uwanja wa Ndege Songwe

VIJANA katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwanja mkubwa wa ndege wa Songwe kwa kuwekeza katika kilimo cha mazao ya bustani ili wanufaike na uwanja huo kipindi ndege kubwa za mizigo zitakapoanza kutua na kupeleka mazao nje ya nchi.

Ofisa Kilimo Mkuu, Wizara ya Kilimo, Merius Nzalawahe alitoa ushauri huo alipofunga mafunzo ya wiki mbili ya mbinu bora za kilimo cha mazao ya bustani kwa watoa huduma binafsi 50 kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi (LSPs) yaliyotolewa na TRI Uyole kwa kushirikiana na HORTI Tengeru.

Watoa huduma hao binafsi ni miongoni mwa watoa huduma 100 watakaopewa mafunzo na wakishapata elimu hiyo watakwenda kutoa elimu na kuwaongoza wakulima wa kilimo cha mazao ya bustani kwenye maeneo yao kupitia Mradi wa Kilimo Bora cha Mboga na Matunda (Kibowavi) ulioandaliwa na Shirika la Helvetas Tanzania kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya.

Nzalawahe alisema wakati serikali ikiendelea na jitihada za kuuimarisha uwanja wa Songwe ili ndege kubwa na za kimataifa ziutumie si wakati wa wakazi wa mikoa hiyo kubweteka bali waige utaalamu kutoka kwa wenzao wa ukanda wa kaskazini wanaoutumia Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kusafirisha mazao ya mboga, matunda na maua kwenda nje ya nchi na kujipatia kipato kikubwa.

Aliwataka kuchangamkia fursa za miradi yenye kutoa utaalamu wa kilimo cha mazao ya bustani kuwa chanzo cha kuwajengea msingi wa kuanza kujikita kwenye mazao hayo aliyosema yana faida kubwa kiuchumi zaidi ya yale ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele kwa muda mrefu.

Nzawahale aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kutokuwa wachoyo watakapokuwa kwenye maeneo yao ila waisambaze elimu waliyoipata ili jamii yote inayowazunguka iweze kunufaika na kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Alitaja uwepo wa mazingira rafiki kwa kilimo ikiwemo ardhi yenye rutuba na yenye kutosheleza, hali ya hewa nzuri na maji kuwa chachu ya kuwezesha mpango mkakati wa kilimo cha bustani unafanikiwa kwenye mikoa ambayo mradi wa Kibowavi utatekelezwa kwa miaka minne.

Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Mradi wa Kibowavi kutoka Shirika la Helvetas, Daniel Kalimbiya alisema Umoja wa Ulaya unagharamia asilimia 90 ya mradi kwa kutoa euro milioni tano.

Kalimbiya aliwataka wahitimu hao kwenda kutumia uelewa waliopata ili wakulima kwenye maeneo yao waweze kuzalisha kwa tija na kuondokana na kilimo cha mazoea sambamba na kuwa na matumizi sahihi ya kipato wanachokipata kutoka kwenye shughuli zao za uzalishaji mali.

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Mbeya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi