loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lipumba: Uchaguzi usiwe chanzo uvunjifu wa amani

MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema uchaguzi huu usiwe chanzo cha uvunjifu wa amani ya Tanzania.

Lipumba alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wake wa hadhara wa kuomba kura katika uwanja wa Changarawe uliopo mjini Kayanga, Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera na kusema: “Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kwa kipindi kirefu, hivyo Watanzania wana wajibu wa kuhakikisha amani hiyo inadumu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi”.

Alisema kuwa vyama vya siasa vinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhubiri amani na kuomba Tume ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inasimamia vyema ili uwe huru na haki, suala litakalowezesha nchi kuendelea kudumu katika amani kwa kuwa haki inatendeka.

“Amani hii tuliyonayo, tunapaswa kuilinda na kuhakikisha inadumu, niiombe Tume yetu ya Uchaguzi ihakikishe uchaguzi unakuwa huru na wa haki na ikifanya hivyo, hakika amani yetu itaendelea kustawi katika misingi tuliyoasisiwa. CUF tunaamini katika amani na sera yetu imejikita katika haki sawa kwa wote,”alisisitiza.

Profesa Lipumba aliongeza kuwa anatambua pia wananchi wa Wilaya ya Karagwe wana changamoto nyingi, ikiwemo kero sugu ya maji pamoja na migogoro ya ardhi inayosababisha wengi wao kupoteza haki, hivyo kuwaomba wananchi wa Karagwe kumchagua ili aweze kuwasaidia kutatua kero hizo kwa muda mfupi.

Naye mgombea udiwani Kata ya Kihanga wilayani humo kupitia chama hicho, Anastella Kibake alimuomba Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho na mgombea urais iwapo atapewa ridhaa na Watanzania kuiongoza nchi, awasaidie wanawake wajane na watoto yatima kwa kuwa wamekuwa wakidhulumiwa haki zao.

Anastella aliongeza kuwa wananchi wa kata hiyo wanakabiliwa na changamoto ya huduma za afya, hasa wajawazito kwa kutozwa fedha nyingi wanapokwenda kujifungua hali inayosababisha wanawake hao kuhatarisha maisha yao pamoja na watoto wao kwa kuwa wamekuwa wakijifungulia majumbani kwa kuogopa gharama.

Akijibu hoja hizo, Profesa Lipumba kwanza aliwaomba wananchi wa Kihanga kumchagua diwani huyo kwa kuwa ana maono na hasa matatizo yanayowakumba wanawake na yeye atahakikisha anamsaidia.

Lipumba alisema katika kipindi chake cha uongozi endapo atachaguliwa huduma za afya zitakuwa karibu na wananchi na kuwa rafiki lakini pia kupata ufumbuzi wa kudumu kuhakikisha wananchi wananufaika na mema ya nchi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Karagwe

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi