loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mgombea wa DP Bunda kununulia wanafunzi chakula

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya chama cha DP katika Jimbo la Bunda mkoani Mara, Abubakar Makene amesema moja ya kipaumbele chake akichaguliwa, ni kutumia fedha za mfuko wa jimbo kununua chakula kwa wanafunzi shuleni. 

Makene alisema mbali na kutumia fedha hizo kununulia chakula cha wanafunzi shuleni pia akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu, fedha za mfuko wa jimbo pia atazitumia kufanya kazi ya maendeleo.

“Mimi vipaumbele vyangu ninavyo vingi iwapo mkinichagua kuwa mwakilishi wenu bungeni, lakini kipaumbelee changu kimojawapo ni kutumia fedha za mfuko wa jimbo kwa shughuli za maendeleo, lakini pia fedha hizo nitazielekeza kwenye chakula cha wanafunzi shuleni,”alisema Makene.

Alisema kuwa iwapo chama hicho kikishika dola, kitahakikisha mikopo inayotolewa na serikali inakopeshwa kwa mtu mmoja mmoja na siyo vikundi kama wanavyofanya sasa.

Alisema pia serikali ya chama hicho itafuta vyama vya ushirika na kuwa wakulima watauza mazao yao popote  wapendapo hususani zao la pamba kama ilivyokuwa zamani.

Alifafanua kuwa zao la pamba ni kama vile limekufa kwani zamani kupitia zao hilo wananchi walikuwa wakipata ajira na kulipwa ujira na wenye viwanda na kujiongezea kipato, hata  baadhi yao walikuwa wakijenga nyumba na kusomesha watoto kutokana na zao hilo.

Makene alisema kuwa utaratibu wa sasa wa kuuza pamba kwenye vyama vya ushirika na fedha kuzichukulia kwenye benki mjini Bunda, baadhi ya wakuliwa wamekuwa wakiibiwa fedha zao na wezi. 

Chama hicho kilizindua kampeni zake katika jimbo hilo la Bunda Mjini mkoani Mara juzi, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zinazoendelea ambapo vyama vya siasa vimesimika wagombea katika nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Chama hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu Taifa, Abdul Mluya kilizindua kampeni za mgombea ubunge wake katika jimbo hilo kwenye viwanja vya stendi ya zamani mjini Bunda.

Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiongozwa na Mluya, mkurugenzi wa uchaguzi taifa, Hamkisi Urembo na Mwenyekiti wa DP, Mkoa wa Mara, Chrisant Nyakitita waliwaomba wananchi kumchagua.

foto
Mwandishi: Ahmed Makongo, Bunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi