loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Adaiwa kutumia likizo ya covid-19 ‘kuoa’ msichana kidato cha pili

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Ikungi mkoani Singida inamshikilia mfanyabiashara wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za sufuria mwenye asili ya Kiasia, Ashrafali Mohamed (51), mkazi wa Upanga Dar es Salaam kwa tuhuma za kubaka na kumweka kinyumba mwanafunzi wa kidato cha pili wakati wa likizo kutokana na ugonjwa wa covid-19.

Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni alisema mfanyabiashara huyo ambaye pia ni Ofisa Masoko wa Kampuni hiyo, anadaiwa kutoweka na mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16 wa Shule ya Sekondari Dadu iliyopo katika Kijiji cha Kipumbuiko wilayani humo na kwenda kuishi naye Dar es Salaam tangu Juni 14, 2020 mwaka huu wakati akiwa likizo ya lazima kutokana na kuwapo kwa maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (covid-19).

Alisema taasisi hiyo ilifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa akiwa kwenye nyumba moja ya kulala wageni iliyopo Mji Mdogo wa Puma alikofikia na mwanafunzi huyo wakiwa njiani kurejea nyumbani kwa wazazi wa msichana huyo kwa minajili ya kwenda kutekeleza ahadi yake ya kumjengea nyumba ya mabati 32 ili asifikishwe kwenye vyombo vya sheria.

“Baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, tangu Juni tumekuwa tukimtafuta. Tunawashukuru ndugu, jamaa na wakazi wa Kijiji cha Kipumbuiko kwa ushirikiano wao uliowezesha kumnasa mtuhumiwa,”alisema Nyoni.

Makamu Mkuu wa Shule, Mario Msengasi na Mwalimu Maria Ntandu anayefundisha kidato cha pili "B" katika shule hiyo, walisema watampokea mwanafunzi ili aendelee na masomo iwapo tu ataonesha nia ya kuendelea na elimu yake huku wakieleza namna alivyotoweka.

“Awali, mwanafunzi huyu alikuwa akihudhuria vema masomo kabla ya shule kufungwa kutokana na corona, lakini zilipofunguliwa, hakurudi tena. Tukawa tunapokea taarifa kwamba alitoweka baada ya kurubuniwa na mtu mmoja aliyefika kijijini hapo kuhudhuria sherehe ya familia, wakati huo akiwa na uhusiano wa kimapenzi na mama mdogo wa mwanafunzi huyo,”alisema Mwalimu Ntandu.

Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kutokana na upelelezi wa suala hilo kukamilika. 

BODI ya Korosho nchini (CBT) imesema taarifa zinazogaa ...

foto
Mwandishi: Abby Nkungu, Ikungi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi