loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tunapongeza mwenendo wa kampeni kuendeshwa kwa utulivu

WATANZANIA kupitia vyama mbalimbali vya siasa, wapo katika mchakato wa kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 28, 2020.

Wagombea wa vyama mbalimbali na wapambe wao, wanaendelea ‘kuchanja mbuga’ wakinadi sera ili kuwambia Watanzania wameifanyia nini Tanzania, na wanataka kufanya nini wakipewa ridhaa kuongoza Tanzania.

Wahenga walisema: ‘Mkono mtupu haulambwi’ ndiyo maana, waliokwishalifanyia taifa hili mambo yenye tija, wanatoa orodha ndefu ya mambo hayo mema na kuahidi kuyaendeleza na kuongeza mengine, lakini ambao hawajafanya chochote cha mfano, wanaendelea kutoa maneno matupu.

Tunapenda kuwapongeza wanasiasa na vyama vyote vya siasa wanaojihusisha katika mchakato huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, kwa namna wanavyofanya kampeni ambazo Watanzania wengi walikuwa wanazitaka tofauti na miaka ya nyuma.

Tunasema kuwapo kwa kampeni za kistaarabu zinazoendelea, ni ishara kuwa Tanzania imepikwa na kuiva kimaadili na kidemokrasia kiasi kwamba, kila upande unajua unapaswa kufanya kazi moja, kuomba ridhaa ya wananchi ama iwe ni ngazi ya udiwani, ubunge au urais.

Ustaarabu unaoonekana katika kampeni hizi, ndio uliomfanya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima wakati akizungumza kuhusu Siku ya Amani Duniani, kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kuonesha ukomavu na usawa katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka huu.

Alinukuliwa akisema safari hii polisi hawajasika wala kuripotiwa popote kuwa wametumia nguvu ya ziada katika kutekeleza majukumu yao tangu mchakato huu wa kampeni uanze na kwamba, hawajaonesha kuegemea upande wowote badala yake, wanatoa huduma sawa kwa wagombea na vyama vyote.

Pia katika habari tulizo nazo katika gazeti la leo, moja inamkuu mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu akipongeza jeshi hilo kwa kazi nzuri.

Lissu anasema: ‘Polisi wametupa ushirikiano mkubwa sana, msafara wangu umekuwa ukisindikizwa na polisi kila mahali’ na hii inayoonesha kwamba, katika uchaguzi wa mwaka huu, tofauti na chaguzi zilizotangulia, jeshi la polisi limetekeleza wajibu wake vizuri kwake, karibu kwenye mikutano yote ya kampeni zaidi ya 20 aliyofanya hadi sasa.

Hii nayo, ikamfanya Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini ambaye pia ni mgombea Urais kupitia chama cha Ada-Tadea, John Shibuda kuwapongeza polisi akisema ukimya wa polisi unaoonekana katika kampeni, ni ishara kwamba mambo yanakwenda vizuri, lakini asiwepo mwanasiasa wa kuutumia ukimya huu, kudhani ni udhaifu wa polisi na hivyo, eti akaanza ‘chokochoko.’

Katika hili, tunasema: “Hongera wanasiasa na vyama vyote vinavyozingatia maslahi ya taifa na kujikita katika kampeni za kistarabu maana wanatuma salamu na ujumbe maalumu kwa wasioitaki mema Tanzania.”

Hata hivyo, katika msafara wa mamba, kenge hawakosekani hivyo, tunasema Watanzania kwa nafasi mbalimbali na umoja wao, wahakikishe hawampi nafasi mwanasiasa yeyote kutumia kampeni kwa matusi, kejeli, uchochezi na kashfa dhidi ya wenginena kutaka kuvuruga amani.

Tunasema akipatikana wa namna hiyo, basi apuuzwe na kujulikana moja kwa moja kwamba hawatakii mema Watanzania ndiyo maana, anakwepa kueleza sera na mikakati, anakimbilia kashfa, kejeli, uchochezi na matusi.

Sisi tunasema, hatukatazi mtu au chama kufanya ukosoaji dhidi ya upande mwingi pale mambo yalipokwenda vibaya, bali tunahimiza ukosoaji kama upo, basi ufanyike kwa ungwana na kistaarabu ili amani hii inayowafanya polisi kupongezwa, iendelee.

Iijulikane kuwa mwanasiasa anayetaka madaraka kwa gharama ya usalama na amani ya watu na bila kuonesha atakavyoleta maendeleo na kudumisha amani na, hana tofauti na kibaya kinachojitembeza ndiyo maana sisitunasema: ‘Tunapongeza mwenendo wa kampeni za utulivu.

TANZANIA itakuwa na ugeni mkubwa wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi