loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wachimbaji wadogo wa madini wapewa neno

MAKATIBU Wakuu wa Wizara ya Madini, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Katiba na Sheria, wamewataka wachimbaji wadogo wa madini na wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali kuyatambua mambo mengi yaliyofanywa na serikali ikiwemo kurekebisha Sheria ya Madini ili wanufaike na rasilimali hiyo.

Akizungumza jana katika Kongamano la Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara kwa wachimbaji wadogo na wajasiriamali kwenye Maonesho ya Tatu ya Kimataifa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye sekta ya madini mkoani Geita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema serikali imefuta kodi nyingi zilizokuwa kikwazo kwa wachimbaji wadogo nchini.

Alisema hata mrahaba wa asilimia sita ambao wachimbaji wadogo wanatoa siyo kodi, bali ni shukrani kwa Watanzania wenzao kutokana na kuchimba na kuuza rasilimali ya madini inayomilikiwa na Watanzania wote.

“Hata ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 siyo kodi ila ni mchango ambao mchimbaji mdogo anautoa kwa jamii inayomzunguka ili nayo inufaike na madini hayo, lakini pia mwananchi kuishi juu ya ardhi ambayo chini kuna madini haimpi uhalali wa kumiliki madini kwa kuwa wamiliki wa madini hayo ni Watanzania wote,” alisema Profesa Msanjila.

Kauli hiyo ya Profesa Msanjila kuhusu umiliki wa madini ilikuja baada ya Katibu wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) mkoani Geita, Evelyne Bwire kuiomba serikali kuwatambua watu ambao chini ya miji yao kuna madini ili wapewe asilimia 25 ya faida ya kiasi cha madini kitachopatikana badala tu ya ama kufukuzwa, au kulipwa fidia kidogo.

Kutokana na hoja hiyo, Profesa Msanjila alisema sheria ya ardhi inampa haki Mtanzania yeyote kuishi juu ya ardhi wakati sheria ya madini inamtaka kila Mtanzania kutambua kuwa rasilimali zilizopo chini ya ardhi katika eneo analoishi siyo mali yake, bali maliya Watanzania wote, na kinachotakiwa ni kulipwa fidia na kupisha shughuli za uwekezaji ziendelee.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki, alisema kuwa Serikali chini ya Rais John Magufuli imeboresha mazingira ya wafanyabiashara nchini wakiwemo wanaouza au kuagiza bidhaa nje ili biashara zao ziwe na tija kwao na kwa taifa.

Profesa Shemdoe alisema baadhi ya taasisi zipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) yenye jukumu la kusajili kampuni zikiwemo za madini ziwe ndogo, za kati au kampuni kubwa ili kufanikisha uwekezaji kwenye sekta ya madini.

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Geita

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi