loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Magufuli kutumia siku 30 kutafuta ushindi wa kishindo’

KATIBU wa Itikati na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema watatumia siku 30 za mwisho za kampeni, kutafuta ushindi wa kishindo na wanapanga kuongeza nguvu, kwa kuwatumia marais na mawaziri wakuu wastaafu.

Pia amelitaka Jeshi la Polisi kushughulikia kwa haraka vitendo vya uvujifu wa amani na mauaji, vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya vyama vya upinzani. CCM leo inaanza siku 30 za mwisho za kampeni kwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kufanya mkutano Iringa mjini katika Uwanja wa Samora.

Polepole jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa, kesho Magufuli atakwenda Mbeya akipitia Makambako mkoa wa Njombe na atafanya mikutano njiani. Septembe 30 atawasili mkoani Mbeya na kufanya mkutano mkubwa kuomba kura.

“Tutaongeza ‘injini’ mpya kwa kuwatumia marais wastaafu, mawaziri wakuu wastaafu na makada waandamizi, watakaofanya mashambulizi mapya kila kona ya nchi”alisema.

Alisema Magufuli atazitumia siku hizo kutoa maelezo yaliyosheheni takwimu sahihi, maono yake kwa Watanzania na kueleza yaliyomo kwenye ilani ya chama hicho. “Zitakuwa ni siku 30 kuu, tutakwenda kujibu hoja za uongo zinazotolewa na mgombea wa chama cha Mbowe, na akiendelea kueneza uongo huo tutabainisha madudu yao ili wananchi wajue ni watu wa aina gani hao.”alisema Polepole.

Alisema tayari Katibu Mkuu wa chama hicho, Profesa Bashiru Ally ametoa maelekezo kwa wagombea udiwani na ubunge na viongozi wengine wa CCM, kutoacha uongo kubaki katika maeneo yao.

Polepole alisema siku zilizobakia, mgombea wa CCM atakuwa na ajenda kuu mbili ya kueleza maono yake jinsi alivyopangwa kuipeleka nchi na pia kueleza sera za CCM kupitia ilani ya CCM.

“Rais ana maono yake kwa nchi, atawaeleza wananchi lakini pia atatumia Ilani ya CCM ambayo imesheheni mambo mengi. Wananchi wengi wamekuwa wakijiuliza akimaliza awamu yake ya uongozi Rais Magufuli nani anaipokea nchi na kufanya makubwa kama yaliyofanyika.

“CCM imejibu hilo kwa kuandaa Ilani yenye mambo mengi, yatakayokamilishwa ndani ya miaka mitano, katika kipindi cha pili cha Rais hatakuwa na muda wa kulala.”

“Watanzania wajiandae kupokea ujumbe wa amani, siku zilizobaki tutaongeza injini mpya katika kampeni, Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan, Mjumbe wa Kamati Kuu Kassim Majaliwa, mawaziri wakuu wastaafu na makada mbalimbali watatumika kushambulia kila kona, tunakwenda kuwamaliza wapinzani” alisema.

Alisema zitakuwa ni siku 30 za kueleza namna ya kuibadilisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Dodoma na Tanzania yote. Alisema zitakuwa ni siku za maangamizi kwa upinzani.

Aidha, Polepole alitumia fursa hiyo kukanusha taarifa zilizotolewa na mmoja wa wagombea urais wa upinzani kwamba Rais John Magufuli amewaita Wakurugenzi wa Halmashauri mjini Dodoma na kufanya nao vikao vya siri.

“Ni taarifa za uzushi, uongo zenye kuwafitinisha Watanzania, tunaiomba Tamisemi watolee ufafanuzi wa suala hili. Nawaomba Watanzania tumpuuze Tundu Lissu, ana lengo baya na taifa hili, kwani kutoa kauli za uchochezi siyo mara yake ya kwanza, amewahi kusema kuwa viongozi wa nchi wanatoka jalalani, amewahi kusema majaji wetu na viongozi wetu hawajui lugha ya Kiingereza” alisema.

Kuhusu mauaji na kauli za uchochezi, Polepole alilaani mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Vyuo Vikuu mkoani Iringa, Emmanuel Mlelwa, anayedaiwa kuuawa na watu wasiojulikana na kulitaka jeshi la polisi kushughulikia kwa haraka vitendo viovu.

Alisema CCM wana taarifa za waliohusika na kifo cha Mlelwa, hivyo Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi na kuwakamata waliohusika.

“Mwili wake ulikutwa eneo la Kibena Bwawani ukiwa umeumizwa na amefariki, nitoe rai kwa Jeshi la Polisi lihakikishe ukweli unafahamika na hatua kali zinachukuliwa kwa wote waliohusika na tukio hilo, kijana huyu alikuwa na ndoto zake,” alisema na kuongeza;

“CCM hatukubaliani na hali hii, tunataka Jeshi la Polisi kutenda haki kwa watu walioumizwa na kuuawa, na ni vyema kushughulikia hayo haraka na kubainisha wahusika ili jamii itambue.”

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi