loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Malipo ya fedha yakwamisha wakandarasi maji Mpwapwa

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, imeomba serikali kutoa fedha za malipo ya hati za wakandarasi mapema ili miradi ya maji itekelezwe kwa haraka wilayani humo.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mpwapwa, Cyprian Warioba alisema hayo juzi. Alisema changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo ni ucheleweshaji wa kupeleka fedha za malipo ya hati za malipo kwa wakandarasi.

Wakati mwingine hati za malipo ya wakandarasi zinachelewa kwa zaidi ya miezi sita, hivyo kufanya utekelezaji wa miradi ya maji kwenda taratibu na kusababisha upatikanaji wa huduma ya maji kuchelewa.

Alisema kutokana na changamoto hiyo ,Ruwasa imekuwa ikiwasiliana na Wizara ya Maji na Ruwasa mkoa, kupeleka fedha za malipo ya wakandarasi wa miradi ya maji kwa wakati ili kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji.

Alisema menejimenti ya mkoa na wilaya, imeweka utaratibu wa kutembelea miradi ya maji ambayo haijakamilika na haitoi huduma ya maji, ili kutatua changamoto ya miradi kutokamilika.

Katika kutatua changamoto hizo, pia walifanya vikao na wakandarasi Agosti 13-15 mwaka huu na walizungumza na wakandarasi hao kuhakikisha miradi ya maji inayowezekana kuanza kutoa huduma, wafanye hivyo na ianze.

Wakandari hao wakiwamo wa miradi ya maji ya Mima, Seluka, Iramba, Kibakwe na Kidenge- Luhundwa-Mpwanila, walikubaliana kuangalia changamoto zilizopo ili waharakishe kukamilisha miradi hiyo na watu waanze kupata maji.

Kupitia vikao hivyo tayari changamoto mbalimbali zilizokuwa zinasubiri ufumbuzi, zinaweza kutatuliwa na maelekezo yameweza kutolewa kwa wakandarasi ambao miradi yao haijakamilika na wameanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa, kwa kufanya kazi zinazofanya huduma za maji zianze kupatikana. Miradi 10 ya maji inatekelezwa katika wilaya hiyo.

Lakini changamoto imekuwa wakandarasi wanacheleweshewa fedha na hivyo inachelewa kutekelezwa. Wilaya ya Mpwapwa ina jumla ya vyanzo 240 vya maji ikiwemo 32 vya mtiririko, visima virefu 46 na visima vifupi 144, matekeni ya kuvunia maji 43, vyanzo vya asilimia 28.

Hata hivyo, vyanzo 114 ndivyo vinavyofanya kazi. Idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama hadi Julai mwaka huu ni 187,750 sawa na asilimia 58.51 ya makadirio ya watu wapatao 320,891 waishio vijijini.

Huduma ya maji Mjini Mpwapwa inasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mpwapwa (MPWUSSA) inayosimamiwa na Bodi ya Maji Mjini Mpwapwa iliyoanzishwa mwaka 2003.

Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Ruwasa inaendelea kusimamia utekelezaji wa jumla ya miradi mbalimbali katika vijiji vya Iyoma, Mima, Iramba, Kidenge-Luhundwa-Mpwanila na Kibakwe. Pia, inasimamia ukarabati wa miradi kadhaa katika vijiji vya Seluka na Chogola.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi