loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusijisahau kabisa tahadhari ya corona

JAPOKUWA watanzania wamekuwa wakiendelea kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuwalinda dhidi ya ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) unaoendelea kuitikisa dunia, bado kuna haja kubwa ya kuendelea kuchukua tahadhari.

Ikumbukwe kwamba baadhi ya mataifa jirani tunayoingiliana nayo bado kuna matukio ya wagonjwa wapya na tusisahau pia kwamba watu wetu wanasafiri kwenda nje huku pia tukipokea wageni kutoka nje. Tuendelee kuiangalia corona mithili ya magonjwa ambayo yamepungua sana nchini mwetu au yanaelekea kutoweka kama polio, lakini hilo halitufanyi tujibweteke kabisa.

Baada ya shule na vyuo nchini kote kufunguliwa, shughuli mbalimbali za kimichezo kuendelea sambamba na mikusanyiko mikubwa ya watu kwenye mikutano ya kampeni za siasa zinazoendelea kote nchini kwa sasa bado suala la watu kuchukua tahadhari ni la muhimu.

Pongezi za pekee zimwendee Rais John Magufuli ambaye tofauti na mataifa mengine duniani yaliyoamua kuwafungia ndani watu wao kama mojawapo ya mbinu za kuzuia kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo, yeye aliamuru shughuli zote za kiuchumi kuendelea huku Watanzania wakichukua tahadhari.

Uamuzi huo si tu uliliacha taifa kubaki imara kiuchumi katika kipindi hiki kigumu, bali pia ulisaidia kuwaondoa hofu wananchi na hivyo kuwajengea ujasiri wa kuendelea na shughuli zao mbalimbali za kujikimu kimaisha, huku serikali nayo kwa upande wake ikiendelea kupanga na kutekeleza mipango na miradi yake kwa maslahi ya taifa.

Ni muhimu pia kumshukuru Mungu kwa kulikinga taifa letu na corona lakini ikumbukwe kwamba katika historia ya dunia mwanadamu amekuwa akipambana na maradhi mapya na ni nadra kuyatokomeza kabisa na hivyo tusijisahau kama vile dunia nzima sasa haina corona.

Kumbuka katika zama hizi za maendeleo makubwa ya teknolojia dunia ni kama kijiji. Licha ya tiba na mbinu mbalimbali za kinga kugunduliwa na wataalamu wa afya, magonjwa kama malaria, kipindupindu, surua na mengineyo yamekuwa yakiendelea kuua wanadamu kote ulimwenguni na hatua mbali mbali za kupambana na magonjwa hayo zimeendelea kufanywa.

Hebu tujiulize tangu kugundulika kwa ugonjwa huu mwezi Desemba 2019 nchini China; hali ingekuwaje hasa hapa nchini kwetu iwapo shughuli zote zingesimama na watu kujifungia ndani kwa kipindi chote hicho kama yalivyofanya baadhi ya mataifa? Bila shaka hali ingekuwa mbaya sana na huenda hata madhara ya hofu ya kujifungia ndani (lock down) na kusimamishwa kwa shughuli zote za kijamii na zile za kiuchumi yangekuwa makubwa kuliko hata madhila halisi ya ugonjwa wenyewe!

Tukumbuke wakati wa gharika ya Nuhu pale ndani ya Safina alitumwa kunguru ili alete habari kama maji ya gharika yamepungua lakini hakurudisha jibu, pengine kwa sababu ya kunogewa na kula mizoga; hadi alipotumwa njiwa aliyeleta habari njema za kupungua kwa maji kwenye uso wa dunia.

Je, sisi watanzania tungemtuma nani tukiwa kwenye safina ya ‘lock down’ majumbani ili atupe taarifa sahihi juu ya kuongezeka au kupungua kwa maambukizi ya Covid-19? Katika ulimwengu huu uliojaa ‘kunguru’ waliotamani kula mizoga yetu ambayo walitaraji itokane na corona, tungewezaje kweli kupata taarifa sahihi kama zile za yule njiwa wa kipindi cha Nuhu aliyekuja na jani bichi lenye ujumbe wa kutia moyo kama ule ujasiri aliotupa Rais wetu Magufuli?

Hata hivyo, hilo lisitufanye tubweteke bali tuendelee kuomba na kumshukuru Mungu kwa kutunusuru na janga hili, huku pia tukiwa na ujasiri tuliojengewa na kiongozi wetu wa nchi kwa kuzidi kuchukua tahadhari zaidi na zaidi ili kuzuia maambukizi mapya.

Ni katika muktadha huo, tunapaswa kuendelea kujikumbusha kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha mikusanyiko mikubwa kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi sanjari na kwenye mechi za mpira wa miguu za ligi kuu ya soka nchini. Ni vyema pia kuendelea kuwa na ufahamu wa namna ugonjwa huo unavyoambukizwa, mbinu za kujikinga nao hadi dalili zake.

Kwa kukumbushana tu, mtu anaweza kupata covid-19 kwa kuambukizwa virusi vya corona kutoka kwa watu walioambukizwa kupitia majimaji kama mate, kamasi kutoka kwenye pua au mdomo wa mtu aliyeathirika na kisha kujigusa macho, mdomo au pua. Dalili za covid-19 ni pamoja na kuwa na homa kali, uchovu na kikohozi kikavu huku dalili kuu na inayotisha ikiwa ni kushindwa kupumua vizuri (kukosa pumzi) ingawa dalili hiyo humtokea mtu mmoja kati ya sita walioambukizwa.

Hata hivyo, asilimia 80 ya walio na virusi vya corona huweza kupona bila kuhitaji matibabu. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wazee na watu wenye magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari na matatizo ya figo ndiyo walio kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha pale wapatwapo na virusi vya corona.

Njia za kujikinga na ugonjwa huo ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka kila wakati na sabuni au dawa za kuua vijidudu. Lakini uchunguzi unaonesha kwamba sasa hivi hata katika maeneo mengi ambayo kumetayarishwa maji kwa ajili ya kunawa, watu hawajali tena kunawa.

Lakini kwa kujenga utamaduni wa kunawa hautukingi na corona pekee bali pia dhidi ya magonjwa ya kuhara. Kaa umbali angalau hatua mbili na mtu anayeweza kupiga chafya ama kukohoa na tunapopiga chafya na kukohoa tusiache kujikinga kwa viwiko vya mkono.

Hii haitukingi na corona pekee bali pia mafua au magonjwa mengine ya mfumo wa hewa. Tuendelea kuepuka kushika macho, pua au mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono hugusa sehemu nyingi na ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi hata kama si corona. Bado tuna dhima ya kufuatilia taarifa za afya kuhusu Covid-19 na namna ya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya virusi vya ugonjwa huo.

Kimsingi huna cha kupoteza kama utaendelea kuvaa barakoa ama kubaki nyumbani ikiwa unajihisi hujisikii vizuri ama una mafua makali au kikohozi. Kwa wenzetu Ulaya ambao mafua ni ugonjwa ‘mkubwa’ mtu akiwa na mafua hujitahidi kadri inavyowezekana kujitenga na wengine (kijikarantini). Lakini la muhimu zaidi ni kuwahi hospitali ikiwa unahisi kushindwa kupumua vyema.

Pengine mtu anaweza kujiuliza kwa nini watu wanawekwa karantini pindi wanapohisiwa kuwa na dalili za covid-19. Kwa kifupi neno karantini ni kuwa chini ya uangalizi kwani watu wanaotokea maeneo ambayo yana maambukizi makubwa hulazimika kutengwa kwa muda ili kufuatilia kwanza afya zao kwa karibu.

Hadi sasa hakuna chanjo wala tiba dhidi ya virusi vya corona lakini kwa sababu dalili zake zinashabihiana na mafua makali na homa, kumekuwa na mchanganyiko wa tiba ambazo walau zimekuwa zinatumika kupunguza makali ya athari za virusi hivyo.

Hivyo basi ni vyema wananchi tukaendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata na kuzingatia maelezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi mapya ya corona hasa katika kipindi hiki cha mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu na hata kwenye michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania inayoendelea kote nchini.

Tusisahau pia kula vizuri hususani vyakula vyenye vitamini nyingi na madini kama mboga na matunda ili kuweka miili yetu katika hali nzuri dhidi ya magionjwa bila kutupilia mbali tiba zetu mbadala kama ‘kupiga nyungu’ (kujifukiza) na kunywa mchanganyiko wa vitunguu swaumu, vitunguu maji, limao, tangawizi na pilipili kichaa.

Ni jambo jema na la kuvutia kwa sasa kuona kila katika taasisi ya umma na watu binafsi bado kumeendelea kuwekwa vyombo vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni maalumu, utamaduni ambao unapaswa kuendelezwa wakati wote licha ya kupungua kama si kumalizika kabisa kwa maambukizi ya virusi vya corona hapa nchini.

Shime basi kwa pamoja kila mmoja kwa nafasi yake Tanzania bila Covid-19 Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano

INASIMULIWA kuwa miaka takribani 1000 iliyopita, eneo hili Ugogo ambalo ...

foto
Mwandishi: Fazel Janja

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi