loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kisiwani Irugwa miaka 5 iliyopita, yajayo yanafurahisha

ILANI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 imeelekeza serikali kuboresha usafiri wa majini hususani katika kisiwa cha Irugwa, wilayani Ukerewe katika mkoa wa Mwanza.

Hii ni sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa alipohutubia mkutano wa kampeni kisiwani Irugwa.

Inanikumbusha  safari ya kisiwani Irugwa niliyoshiriki miaka mitano iliyopita wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na namna wananchi walivyotamani kupata usafiri wa uhakika.

Safari ilianzia mjini Mwanza kwa pantoni binafsi  tangu saa nne usiku na kuwasili kisiwani Irugwa kesho yake alasiri.

Kutokana na hitilafu kwenye injini moja, pantoni ililazimika kwenda mwendo wa pole hivyo kulazimika kutumia muda mwingi kabla ya kufika.

Wakati huo (mwaka 2015), kisiwa hicho chenye vijiji viwili, kilikadiriwa kuwa na wakazi wapatao 10,000. Kilikuwa na shule mbili za msingi na moja ya sekondari.

Tulielezwa ni miongoni mwa visiwa vipatavyo 30 vinavyounda wilaya ya Ukerewe ambacho wakazi wake wanajishughulisha na uvuvi pamoja na kilimo hususani cha mihogo.

Ziara kisiwani humo ilitajwa kuwa ya kihistoria kutokana na  kile kilichoelezwa na wenyeji kwamba, hakijawahi  kutembelewa na viongozi wa juu kwa miaka mingi.

Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mwanza, Anthony Dialo, ni miongoni mwa waliokiri juu ya hilo. Alisema, wananchi katika kisiwa hicho chenye vijiji viwili, walikuwa na zaidi ya miaka 30 bila kuona kiongozi wa kitaifa.

Wananchi walimtajia jina la mkuu wa mkoa wa mwisho kufika kisiwani humo kuwa alikuwa ni Nangwande Sijaona aliyeongoza enzi za serikali ya awamu ya kwanza chini ya  Mwalimu Julius Nyerere.

Miongoni mwa kero zilizowasilishwa kwa Kinana ni ukosefu wa usafiri wa uhakika. Walisema wamekuwa wakitegemea mitumbwi isiyo salama kwenda Nansio au Majita.

Kutokana na kukosekana vyombo vya usafiri majini, tulielezwa kwamba mara ya mwisho gari kufika Irugwa ni miaka zaidi ya mitano.  Wenyeji walisema, kulikuwa na gari moja aina ya Pick up lililokuwa likisafirisha abiria kati ya eneo la Ngera na Nabweko Mchangani.

Umbali kati ya vijiji hivyo ni takribani dakika 50 kwa gari. Gari hilo liliharibika hivyo kufanya huduma za usafiri kutoweka. Wenyeji walisema usafiri unaotegemewa ndani ya kijiji ni baiskeli na pikipiki.

Walikiri kwamba, watoto wengi na hata baadhi ya watu wazima walio katika vijiji viwili vinavyounda kata hiyo ya Irugwa, magari walikuwa wakiyasikia.

Ujio wa Kinana ulichukuliwa kwa uzito wa aina yake kwani licha ya kuwa kiongozi wa juu wa chama kufika kisiwani humo baada ya miaka mingi, bado uliwezesha watoto kuona magari mengi yaliyofika kwa pantoni.

Hata hivyo haikuwa rahisi kwa magari yote ya msafara kuingia kijijini kutokana na kuzuiwa na mchanga wa mwaloni.  Magari matatu pekee ndiyo yalimudu kupenya hadi kijijini.

Wenyeji ambao wengi ni jamii ya Wakerewe, Wajita na Wakara walikiri kuwa ziara iliandika historia si tu ya magari zaidi ya moja kuingia kijijini, bali pia kufika kwa pantoni kubwa iliyobeba vyombo hivyo vya usafiri. 

Wakizungumza na Kinana, miongoni mwa kero walizoomba zipatiwe utatuzi ni ukosefu wa usafiri salama na wa uhakika katika Ziwa Victoria. Walitamani kupata usafiri wa kuwaunganisha na Majita, Ukara na Nansio yalipo makao makuu ya Wilaya ya Ukerewe.

Walisema usafiri wanaotumia ni mitumbwi ambayo huhatarisha maisha yao majini.

Baada ya kutembelea Irugwa na kushiriki ujenzi wa jengo la wodi ya kituo cha afya lililogharimu Sh milioni 36.9, msafara wa Kinana ulikwenda pia kisiwa cha Ukara ambako pia wananchi waliomba vyombo vya usafiri wa uhakika.

Ni jambo la kufurahisha kwamba sasa kilio cha wananchi  hao kimefanyiwa kazi kwani serikali imedhamiria kujenga kivuko  na wakati huo huo kununua boti ya kwenda Irugwa.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa  aliyefika Irugwa hivi karibuni, alitoa taarifa hiyo katika mkutano wa kampeni.

Waziri Mkuu, Majaliwa aliwaeleza wananchi matarajio ya serikali ya CCM ya kujenga kivuko sambamba na kununua boti itakayokwenda Irugwa.

Majaliwa alisema chama kitakaposhika madaraka kipindi kingine, serikali itajenga vivuko vingine vya Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya, wilayani Ukerewe.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, imeelekeza serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya vinane katika mikoa tofauti kikiwamo cha Irugwa - Murutanga (Ukerewe). Imeelekeza pia ununuzi wa boti kati ya Irugwa na Ukara.

Huu ni ukombozi mkubwa kwa wakazi wa visiwa hivi. Hata mgombea ubunge wa Ukerewe kupitia CCM, Joseph Mkundi, alipozungumza kwenye mkutano huo wa kampeni wa Majaliwa, alikiri kuwa huo ni ukombozi.

Alisema kivuko cha Irugwa kitakuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hilo ambao watoto wao hawajawahi kuona gari likipita katika kisiwa hicho kutokana na ukosefu wa kivuko. Kwa ahadi hii iliyoingizwa kwenye ilani ya chama, ni dhahiri miaka mitano ya utekelezaji wake endapo CCM kitashinda uchaguzi, yajayo kisiwani Irugwa yanafurahisha.

KATIKA kipindi cha miezi michache iliypopita, dunia ...

foto
Mwandishi: Stella Nyamenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi