loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wajane walipotoa machozi kukutana na mgombea urais 

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, amekuwa akiendelea na mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu kwa njia tofauti kwa kuyatembelea makundi maalumu ya watu.

Anapozuru makundi hayo husikiliza kero zao zinazowakabili ili akifanikiwa kuwa rais iwe rahisi kuzifanyia kazi sambamba na kuwaeleza mikakati yake na alivyojipanga kutekeleza ilani ya chama chake.

Makundi ambayo tayari yamefikiwa katika kipindi cha wiki mbili za kampeni za mgombea ni walemavu, wajasiriamali pamoja na wajane.

Unaweza kusema haijawahi kutokea kwa kiongozi yoyote aliopo madarakani kukutana na kundi la jumuiya ya wajane na kusikiliza changamoto zao ili kuona namna ya kuzitatua.

“Sikuamini nilipoambiwa sisi kundi la wajane tujiandae kukutana na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi... Ni faraja na dalili ya kuzipatia ufumbuzi changamoto tunazopitia,” anasema Fatuma Haji, mjane aliyeondokewa na mumewe miaka mitano iliopita.   

Dk Hussein Mwinyi alipokutana na jumuiya ya wanawake wajane na kuzungumza, aliahidi kuwatambua na kuona namna ambavyo itawezekana kuwaingiza katika mfuko wa hifadhi ya jamii na kupata mikopo itakayosaidia kuwakwamua kimaisha na kupiga hatua kimaendeleo.

Akizungumza na wanawake hao katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Mwinyi anasema akichaguliwa kuwa rais anakusudia kutafuta mwarubaini wa kunyanyua kiuchumi makundi maalumu ikiwemo walemavu, wazee pamoja na wanawake wajane.

Katika mkutano, kundi la wajane ndilo lilionekana kuhamasika zaidi huku baadhi yao wakitoa machozi kuona kuna mtu ameamua kuwakumbuka na kuahidi kuona namna ya kuwasaidia.

Moja ya hatua ambazo Mwinyi anafikiria kuchukua ni pamoja na kuyapatia makundi hayo mikopo isiyokuwa na riba huku serikali yake ikichukua jukumu la kulipa riba katika taasisi za fedha.

“Nazitambua changamoto kubwa zinazowapata wanawake walioachwa na waume zao na hivyo kuishi katika mazingira magumu... 

Nikichaguliwa nitalichukua suala hilo kwa kuyaingiza makundi maalumu katika mfumo wa kupata mikopo isiyokuwa na riba na kupata fedha kwa ajili ya kufanya miradi midogo midogo ili kuondokana na hali ngumu ya maisha,” anasema.

Anasema anakusudia pia kuangalia sheria ili kuona kama kuna udhalilishaji wowote wanaofanyiwa wanawake wakati wanapopewa talaka waume zao huku wengine wakijikuta wakiachiwa mzigo wa familia ikiwemo watoto.

Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wajane, Tabia Makame anasema wakati umefika kwa makundi maalumu ya wanawake ikiwemo wajane kutambuliwa na hata kuingizwa katika vyombo vya maamuzi ikiwemo kutunga sheria ili sauti zao zisikike na maslahi hao kulikana.

Tabia anasema kutokana na jinsi yao wajane wamekuwa wakidhalilishwa na kunyanyaswa na jamii baada ya kufiwa waume zao.

Anasema wanawake wajane na wanaotalikiwa wanakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo kuachiwa mzigo wa familia na watoto na hivyo kushindwa kumudu majukumu ya kutunza watoto katika kuwapatia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, chakula bora, matibabu na mavazi.

Anasema hivi sasa kuna wimbi kubwa la talaka ambazo hutolewa na nyingine kwa njia ya simu za mikononi na kwamba talaka za holela ni chanzo cha utelekezaji wa watoto baada ya kukosa matunzo ya wazazi wawili.

“Tunakuomba mheshimiwa ukifanikiwa kuingia madarakani sisi wanawake wajane (na waliotalikiwa) tunahitaji tupatiwe ufumbuzi wa matatizo yetu ikiwemo suala la udhalilishaji wa kijinsia kwa kuachiwa malezi ya watoto wakati hatuna uwezo wa kifedha,” anasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya wanawake wajane ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma anasema wameanzisha taasisi hiyo kwa ajili ya kujikomboa dhidi ya umaskini kutokana na kukabiliwa na mzigo mkubwa wa maisha.

Anasema wajane, mbali ya kutakiwa kujihudumia, huku wengi wakiwa hawana vyanzo vya uchumi, pia huwa na mzigo wa kutunza watoto.

 

 

 

Anasema baadhi ya sheria zinahitaji kufanyiwa marekebisho zaidi ili ziwabane wanaume katika suala la matunzo kwa watoto wakati wazazi wawili wanapotengana ili ziwawezeshe watoto kupata matunzo ya uhakika.

“Nawaomba wanawake wajane waitumiye jumuiya hii kwa ajili ya kuunganisha nguvu zao na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ikiwemo kupewa jukumu la malezi ya watoto na wanaume waliowapa talaka,” anasema.

Waziri wa Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Wazee, Moudline Castico anakiri kuwepo kwa matatizo mbali mbali kiuchumi na kisheria yanayowakabili wanawake, hususani wajane na watoto ambayo chanzo chake kikubwa ni talaka.

Kwa mfano, anasema hadi sasa mwanamke anapewa talaka na kuondoka katika nyumba aliyoishi na mumewe kwa muda miaka mingi bila ya kuwa na kianzio cha maisha yake mapya huko anapokwenda.

''Bado wanawake wajane wanadhalilika sana katika maisha yao... Wapo wengine wanapopewa talaka hufukuzwa katika nyumba walizoishi na waume zao kwa zaidi ya miaka kumi huku wakiwa wamezaa watoto na wengine kwa ajili ya umri wa mtoto huondoka nao huku wakiwa hawapati matunzo,” anasema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Wazee Fatma Gharib Bilali anasema wapo tayari kutoa ushirikiano wa dhati kwa jumuiya hiyo ili kuona malengo yake yanafikiwa katika kuzipatia majibu changamoto zinazowakabili wanawake wajane (na waliotalikiwa).

“Wizara ya Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Wazee tupo tayari kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanawake na kuona malengo na matarajio yao yanafikiwa na hatimaye wanawake wajane wanakuwa salama zaidi,” anasema.

Khadija Ismail, mkazi wa Mikunguni anasema amefurahishwa na uamuzi wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo pamoja na malengo yake ambayo yamejikita katika kuwakomboa wanawake na madhila wanayoyapata baada ya kuachwa na waume zao.

“Niliposikia jumuiya hii inaanzishwa, sikusita nilijiunga nayo mara moja kwa sababu, kama ilivyo kwa wanawake wengi tunaoachwa au kufiwa na waume, tunakuwa na changamoto nyingi zingine zikiwa nje ya uwezo wa mtu mmoja mmoja,” anasema.

Kuhusu hatua ya mgombea urais kuamua kukutana na wajane hao, Khadija anasema ni jambo ambalo hakulitegemea na ndio maana baadhi walimwaga machozi ya furaha.   

Jumuiya ya Wanawake Wajane (ikihusisha pia waliopewa talaka) ilianzishwa mwaka jana ikiwa na jumla ya wanachama 60. Malengo yao makubwa nan i namna ya kujikimu kimaisha na matunzo ya watoto.

BARAZA la Kiswahili la ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi