loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Elimu ya mpigakura ni muhimu kwa wote

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni iliwataka wadau wa siasa nchini kuelimisha wapigakura kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Giveness Aswile, alisema wadau wa siasa wanatakiwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua rais, wabunge na madiwani siku hiyo ya uchaguzi.

Lengo la NEC ni kufanikisha uchaguzi mwaka huu uwe huru, wa haki, amani na wenye kuaminika na watu wote nchini na nje ya nchi kutokana na namna utakavyoendeshwa.

Tunaungana na NEC kutoa rai kwa wadau wote wa uchaguzi ikiwamo vyama vya siasa, wagombea, asasi zilizopewa jukumu la kutoa elimu hiyo na wengine kutumia kipindi hiki kilichobaki kabla ya kupiga kura, kujikita kuelimisha wananchi umuhimu wa kupiga kura ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuchagua viongozi wanaofaa.

Wadau hao wanapaswa kuwahamasisha wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni ya wagombea na vyama vyao inayoendelea wapate fursa nzuri ya kujua watakayoyasimamia na kuyatekeleza endapo watashinda ili siku ya kupiga kura waweze kupembua mchele na pumba.

Ni matumaini yetu kuwa wadau wa siasa watatekeleza wajibu wao katika kufanikisha uchaguzi mkuu kwa kuhamasisha umma kushiriki wakati huu wa kampeni na siku ya uchaguzi kupigakura kwa kutumia vitambulisho vyao.

Wadau hao wana wajibu mkubwa wa kuhamasisha makundi yote ya kijamii ikiwamo wanawake, vijana na wenye mahitaji maalumu kuwapima vizuri wagombea na vyama vyao ili waweze kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaoweka mbele maslahi ya umma na taifa.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wapigakura 29,188,347 wamejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambapo kati yao 29,059,507 wapo Tanzania Bara na 128,840 wa Tanzania Visiwani.

Aidha, kati ya waliojiandikisha kuna walemavu 13,211 ambao kati yao 2,223 ni wa ulemavu wa macho, 4,911 wana ulemavu wa mikono na 6,077 wana ulemavu wa aina nyingine.

Tume hiyo pia imeshawapatia wasimamizi wa uchaguzi na vyama vya siasa orodha ya wapigakura kwa ajili ya kuhakiki wapigakura waliowadhamini wagombea katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na vyama vya siasa vimepatiwa nakala tepe ya daftari hilo kwa ajili ya rejea wakati wa Uchaguzi Mkuu.

NEC imeshatangaza kuwa itatumia vituo 80,155 katika kupiga kura Oktoba 28, kati ya hivyo, Tanzania Bara itakuwa na vituo 79,670 na Tanzania Zanzibar itakuwa na vituo 485.

Vilevile tume Tume hiyo imeeleza kuwa itatumia vituo 1,412 vya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa upande wa Zanzibar, ambapo katika kila kituo kitakuwa na wapigakura wasiozidi 500 kwa ajili ya uchaguzi huo.

JUZI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi