loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uoto mpya sasa unarejesha wanyamapori bonde la Ihefu

HATIMAYE jitihada za serikali za kurejesha uoto wa asili katika bonde la Ihefu lililo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha zimeanza kuzaa matunda. Haya ni matokeo chanya na ya kufurahisha kwa kuanza kuonekana kwa wanyamapori waliolikimbia bonde hilo lililowahi kuvamiwa na watu.

Hadi kufikia mwaka 2008 hali ya bonde la Ihefu ilikuwa ya kusikitisha kutokana na uharibifu mkubwa uliokuwa umefanyika kutokana na kushamiri kwa shughuli za kibinadamu.

Wanyama walilazimika kukimbia kwa kuwa eneo hilo halikuwa tena na mazingira rafiki kwao. Wanyama walijikuta maisha yao yakiwa hatarini wakati wote.

Ni katika muktadha huo, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha shughuli za kibinadamu kwenye eneo hilo ikiwemo kilimo na ufugaji. Ililazimika pia kuhamisha baadhi ya vijiji vilivyokuwa vinaathiri vibaya bayoanui na ikolojia ya bonde hilo oevu.

Haikuwa kazi rahisi lakini kwa jitihada na ushirikiano wa uongozi wa wilaya ya Mbarali chini ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, Hawa Ngurume, na vyombo mbalimbali vya dola shughuli ilifanikiwa.

Makundi ya mifugo yalihamishwa kutoka kwenye bonde hilo na kisha likaingizwa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Shughuli za binadamu pia zilikuwa zikihatarisha uwepo wa Mto Ruaha Mkuu kutokana na ukweli kwamba awali eneo hilo oevu na chanzo kikubwa cha maji ya mto huo.

Kwa sasa uoto wa asili wa eneo hilo na ardhi yake oevu imerejea kama mwanzo na hivyo sasa waweza kusema wenyenyumba yao, yaani wanyama baada ya kuona makazi yao sasa yako salama wameanza kurejea na kufurahia maisha kwenye makazi yao ya asili.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi Tanzania (Tanapa) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye makao yake makuu katika mji wa Rujewa wilayani Mbarali,

Pius Mzimbe anasema baada ya eneo hilo kufanywa sehemu ya Hifadhi ya Ruaha uoto wa asili umezidi kurejea katika hali yake ya awali hatua inayoonekana kuzidi kuwavutia upya wanyama.

Aliyasema hayo alipozungumza na wanahabari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET) waliofanya ziara wilayani hapa kwa lengo la kufuatilia na kujionea kurejea kwa Ikolojia ya asili ya Bonde hilo la Ihefu.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwen delezo wa JET katika kufuatilia ikolojia ya bonde hilo kwa kuwa kazi za wanachama wake ndizo ziliwafumbua macho wadau wa mazingira baada ya kuripoti namna uharibifu mkubwa ulivyokuwa unafanyika katika bonde hilo.

Mzimbe anawataja wanyama waliorejea na sasa wanapatikana kwa wingi kwenye bonde hilo kuwa ni pamoja na tembo wanaoonekana sasa wakiwa katika makundi, nyati, pofu, twiga, viboko na simba.

Pia kuna wanyama wadogowadogo ambao kwa kiasi fulani walibaki lakini kwa sasa nao wameongezeka sana kama vile swala, digidigi, sungura na ndege kama kware na kanga.

“Ilifika wakati hauwezi kuwakuta wanyama hawa katika bonde hili kwa kuwa walihama kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwao. Hata walipoonekana basi jua walikuwa wakipita wakitoka sehemu ya Ruaha upande wa hifadhi kwenda mapori mengine lakini si kwa kuishi ndani ya bonde.

“Lakini baada ya mpango wa Serikali wa kuliingiza bonde lote katika eneo la hifadhi na kuhamisha mifugo iliyokuwa imelivamia, kadiri uoto wa asili unavyorejea ndivyo na kasi ya wanyama kurejea inaongezeka.

Sasa imekuwa kawaida kuwaona wanyama na hakika tunakoelekea ni kuzuri zaidi maana sasa bonde ni oevu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.” Kurejea kwa wanyama hawa kwenye maeneo yao ya asili kumeibua changamoto nyingine kwa baadhi ya vijiji jirani kuanza kuvamiwa na wanyama.

Sasa ni kawaida wanyama kuonekana vijijini na kuna wakati wanaleta madhara kwa kula mazao, mifugo au hata mauaji ya binadamu. Lakini Mzimbe anasema kimsingi si wanyama wanaovamia vijiji bali vijiji ndivyo vilivyovamia maeneo ya mapito ya wanyama yaani shoroba.

Anasema kwamba baada ya wanyama kukimbia, watu walianzisha vijiji wasijue kiuasilia maeneo hayo ni miliki za wanyama. Kutokana na uwepo wa mazingira rafiki ya hifadhi, Wanyama wanayakumbuka pia  Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa),Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Pius Mzimbe akizungumza na wanahabari kutoka Chama cha waandishi wa habari za Mazingira (JET) katika ofisi za mamlaka hiyo mjini Rujewa, Mbarali.

 Ilifika wakati hauwezi kuwakuta wanyama hawa katika bonde hili kwa kuwa walihama kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwao. Hata neo jirani waliyokuwa wakiyatumia miaka ya nyuma.

“Wanyama kama tembo wana asili ya kutosahau mapito yao. Hata ipite miaka mingi. Vinaweza pita vizazi lakini ipo siku kama sehemu ilikuwa njia yao watakuja tu kupita.

Kwa eneo hili wapo wanyama wanaoonekana wakisafiri kutoka sehemu ya hifadhi kwenye mapori tengefu yaliyopo jirani ikiwemo Uturo. “Lakini pia kwa kuwa ndani ya hifadhi, hasa upande huu wa bonde la Ihefu, nyakati za masika kunapokuwa na mvua nyingi maji hujaa.

Hali hii inaonekana kuwafanya wanyama watoke bondeni kutafuta maeneo yenye miinuko na hapo ndipo wanajikuta wameingia kwenye maeneo ya wananchi ikiwemo vijijini na kwenye mashamba,” anasema.

Baadhi wa wakazi wa vijiji vya jirani na hifadhi hiyo nao wanakiri wanyama kuanza kuonekana tofauti na miaka kadhaa iliyopita ambapo waliadimika kutokana na uharibifu uliofanyika ndani ya bonde kutokana na shughuli za kibinadamu za kilimo, ufugaji na uwindaji haramu.

Wakazi wa vijiji vya Igava, kata ya Igava na Itipingi kata ya Mawindi, wanasema sasa baadhi ya wanyama wanaonekana kutoishia hifadhini pekee wakiwemo tembo bali wanafika hadi kwenye vijiji vyao.

“Mwaka jana hapa kijijini jirani tu na shule walipita tembo wanne wakubwa na wengine wadogowadogo. Tuliwatoa nje wanafunzi wakapanga mstari kwa mbali… Walikaa kimya ilikuwa wawaone na kujifunza kwa vitendo.

Wanafunzi na walimu tulikaa kimya mpaka walipoondoka kwa kuwa tulikuwa tumeelekezwa kuwa tembo hawapendi kelele hasa ya yanayomchanganya,” anasema Mkuu wa wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Mawindi, Mwalimu Mawazo Ndanzi. Mwalimu Lucas Mtimwa anasema: “Hata leo hii usiku tunaambiwa kuna kundi la tembo limepita hapa kijijini.

Wengine hatukuwaona lakini tumepata taarifa asubuhi hii kuwa leo usiku tulitembelewa na wageni tembo walioonekana wako safarini lakini hawajaleta madhara yoyote.”

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Mtipingi, kata ya Mawindi kilichopo umbali wa kilometa 30 kutoka hifadhini anasema ni muhimu baaada ya wanyama kurejea bondeni, elimu ya uhifadhi kuendelea kutolewa kwa wakazi wa vijiji jirani.

“Ushirikiano baina ya wahifadhi na wananchi uwe wa karibu. Wananchi waeleweshwe kuwa wanyama wana haki yao ya kuishi,” anasema. Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, anasema Serikali itaendelea kutekeleza azma yake ya kusimamia ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ikiwemo bonde la Ihefu katika kuhakikisha inakuwa endelevu kwa kuimarisha ulinzi na ushirikiano baina ya vyombo vya dola na wakazi wa vijiji jirani.

Mafanikio yaliyofikiwa ili kuwa endelevu ni muhimu pia kukawa na mikakati ya kudumu ili kutolirejesha bonde hili katika historia ya uharibifu ya mwaka 2008.

Ni muhimu wadau wote wakatambua wajibu wao kwenye kulinda Bonde la Ihefu na Hifadhi ya Ruaha kwa ujumla. Julai 2017, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala alipofanya ziara kuona maendeleo ya kurejeshwa uasili wa eneo hilo, moja ya changamoto zilizowasilishwa kwake ni pamoja na mbolea zinazotumika kwenye mashamba ya mpunga katikaa bonde la Usangu wilayani Mbarali.

Mbolea hizo zilitajwa kusababisha nyasi ndani ya hifadhi ya Bonde la Ihefu kurefuka kupita kawaida na kusababisha ugumu wa kudhibiti mioto isiyotarajiwa inapotokea.

Kwa mujibu wa Mhifadhi msaidizi wa Hifadhi ya Ruaha aliyeshiriki ziara hiyo, Alexander Haguma kwa asili uoto wa Bonde la mto Ihefu ni wa nyasi fupi lakini mbolea zinazotumika kwenye mashamba ya mpunga ambazo husombwa na maji hadi ndani ya bonde hilo imesababisha nyasi kurefuka kupita kiasi.

“Hili linakuwa ni tatizo pale unapotokea moto usiotarajiwa. Inakuwa vigumu namna ya kuudhibiti,” alisema mhifadhi huyo.

BARAZA la Kiswahili la ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Mbarali

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi