loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bodi ya Ligi ratiba isipanguliwe ovyo

BODI ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) wiki hii ilibadili ratiba ya mechi ya Ligi Kuu kati ya Yanga na Simba kwa kuahirisha mchezo huo uliopangwa kufanyika Oktoba 18 na sasa utafanyika Novemba 7.

Kwa mujibu wa taarifa ya bodi hiyo iliyotolewa wiki hii, mabadiliko hayo yametokana na uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa vikwazo katika usafiri wa kimataifa baada ya kukamilika kwa michezo ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) jambo linaloweza kuathiri vikosi vya klabu hizo mbili.

Pamoja na sababu hiyo na nyingine, lakini bado mchezo huo ungeweza kuchezwa Oktoba 18 na mambo mengine yote kisoka yangeenda vizuri bila kuathiri mambo mengine.

Bodi hiyo ya Ligi inatakiwa kuwa makini zaidi inapopanga ratiba ya mechi za Ligi Kuu na kabla ya kupanga ratiba hiyo iwe inajaribu kuangalia kwa undani ratiba za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Fifa na hata zile za Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) au ligi kubwa za Ulaya kama England, Hispania, Italia na hata Ujerumani.

Ratiba za Ligi Kuu za Ulaya ni muhimu zikaangaliwa kwani soka la Tanzania sio kisiwa kwani mashabiki wengi nchini wamekuwa wakifuatilia kwa karibu ligi hizo na wana timu zao, ambazo wanazishabikia sana.

Hatukatai kubadilika kwa ratiba za ligi, lakini kufanyike pale tu inapobidi au kunapotokea jambo lisilozuilika, lakini si kuingiliana na ratiba ya mechi za kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) au zingine zozote.

Licha ya kusogezwa hadi Novemba 7 bado kuna mkanganyiko wa ratiba, kwani Tunisia inatarajiwa kumenyana na Stars Novemba 13, mwaka huu ugenini nchini Tunisia mchezo wa kufuzu kwa Afcon bado wachezaji wa Stars wanahitaji muda zaidi wa maandalizi ya mchezo huo.

Watendaji wa Bodi ya Ligi wanatakiwa kuumiza vichwa ili kupanga ratiba nzuri, ambayo huko mbele haitakuwa na maswali mengi na majibu machache kutoka kwa wadau wa soka, ambao mara kwa mara wamekuwa wakiitupia lawama bodi hiyo.

Pia bodi hiyo iangalie na ligi nyingine kubwa Ulaya na Afrika zinafanyaje ili kuhakikisha ratiba zao haziingiliani na zile za kimataifa tofauti na ligi ya kwetu, ambayo kila wakati inakuwa na mgongano na ratiba zingine.

Mabadiliko hayo ya ratiba ya mechi ya Yanga na Simba yamepita, lakini hatutarajii kuona Bodi ya Ligi ikibadilisha badilisha ratiba tena kwani kabla ya kuitangaza, ifanyiwe kazi na kujiridhisha kuwa haina tatizo.

JUZI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi