loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Usiruhusu simu ianike faragha zako

UMEWAHI kushuhudia watu/mtu kwenye chombo cha usafiri wa umma akizungumza kwa sauti ya juu ama na mtu mwingine au kwa simu akianika mambo yake kwa kadamnasi? Kama hujawahi, basi subiri ipo siku utashuhudia.

Siyo tu kwenye vyombo vya usafiri, bali watu hao hushuhudiwa pia kwenye mikusanyiko mingine ya watu kama vile kanisani, sokoni au shuleni. Watu wa aina hiyo hugeuka kikwazo kwa watu wengine kutokana na kuzungumza kwa sauti ya juu faragha zao kana kwamba wanahutubia.

Baadhi huzungumza mambo nyeti kuhusu ofisini, familia ikiwa ni pamoja na kujadili majina ya watu hadharani bila kujali waliowazunguka.

Huwa haiingii akilini kuona mtu ndani ya daladala anazungumzia watu wengine kwa kutaja majina yao, nyadhifa na ofisi zao bila kufikiri kwamba miongoni mwa kadamnasi inawezekana wamo ndugu, jamaa na marafiki.

Wengine hudiriki kuanika masuala ya fedha na biashara mbele ya watu bila kujali kuwa inaweza ikawa njia mojawapo ya kukaribisha huduma dhidi yao.

Wakati mwingine, watu wa namna hiyo hugeuka kichekesho kwa kusema mambo ya uongo au kupotosha juu ya mambo wanayozungumza kwa sauti ya juu bila kufahamu kuwa wapo watu wanaofahamu sawia.

Pamoja na kwamba watu wa namna hiyo hawavunji sheria yoyote ikizingatiwa kwamba katiba inatoa uhuru wa kujieleza, lakini ipo haja ya kuelimishwa faida na hasara za upayukaji ama wakati wa kuzungumza kwenye simu au ana kwa ana na mtu mwingine.

Ifahamike upayukaji bila kuzingatia faragha yako au wengine si ustaarabu. Lakini pia ni kitendo kinachoweza kuanika siri zako na za wengine na kuhatarisha usalama wako na mali zako.

Wapo baadhi ya watu waliojikuta mikononi mwa matapeli, wezi na wahalifu wengine kutokana na kuanika mambo yao kwa njia hiyo ya kuzungumza hovyo kwenye kadamnasi.

Katika semina ya hivi karibuni kwa wanachama wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Ofisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi alikumbusha umuhimu wa kuwa na mipaka ya kuanika mambo binafsi.

Mabel alihadharisha pia juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuanika taarifa nyeti, akisema kunatoa fursa kwa matapeli au wezi kutekeleza uhalifu kwa mhusika.

Wakichangia mada hiyo, baadhi ya washiriki walisema wapo watu wanaoponzwa na ushamba, uelewa mdogo au ulimbukeni kiasi cha kutuma picha na taarifa zao zote kwenye mitandao.

Ndiyo maana TCRA imeendelea kuelimisha jamii juu ya suala zima la faragha hususani upande wa mawasiliano kwa simu za mkononi. Katika kitabu chake cha mwongozo kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano, TCRA inasisitiza watumiaji wa simu kuzingatia faragha yao na watu wengine.

“Chukua tahadhari ya wale walio karibu nawe wasisikie mazungumzo yako kwani waweza kupata taarifa zako za siri usizokusudia wao kuzifahamu,” mwongozo unasisitiza.

Inasisitizwa mtumiaji kuepuka kupayuka anapokuwa kwenye mkusanyiko wa watu, mfano benki, maeneo ya ibada na tafakuri, hospitali, kwenye mikutano, darasani.

Mwongozo unasema kwa kawaida, sauti ya mtu anapozungumza na simu inakuwa ni ya juu tofauti na mazungumzo ya ana kwa ana.

Hivyo inashauriwa mtumiaji akitaka kutumia simu kwenye hadhara, akae mbali na watu wengine, angalau hatua nne kutoka mtu wa mwisho kwenye mkusanyiko huo au kama ni kwenye chumba, ni vyema zaidi akitoka nje ya chumba husika.

Vidokezo vingine muhimu ambavyo TCRA inasisitiza watumiaji wa simu kuzingatia ni kuweka mlio wenye staha na heshima kwenye simu kwa kuzingatia maadili ya hadhara/jamii inayokuzunguka. Inashauriwa kutotumia simu kwenye maeneo hatarishi yanayoweza kukufanya mtu asahau anachofanya.

Kwa mfano, wakati wa kuendesha gari au mitambo, jikoni, kutembea barabarani. Lakini pia inashauriwa kutotumia simu katika mazingira yanayoweza kuwapa nafasi watu wenye nia mbaya kufanyia mhusika uhalifu.

Mamlaka inasisitiza watumiaji kuzingatia masharti ya matumizi ya simu, kwa mfano wakiwa ndani ya ndege, maeneo nyeti n.k. Mtumiaji anafundwa kutopigia watu simu au kuwatumia meseji muda ambao kijamii unakubalika kuwa ni usiku sana au asubuhi sana, isipokuwa tu kama kuna dharura.

 

stella.nyemenohi@tsn. go.tz

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi