loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mikakati maalumu inatakiwa kudhibiti vipigo na mauaji ya wanawake

VIPIGO na mauaji kwa wanawake nchini na duniani ni matukio yanayozidi kushika kasi kila siku kiasi ambacho kila wiki si jambo la ajabu kusikia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa kuna tukio la mwanamke kupigwa au kuuawa.

Kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo, jamii imekuwa ikihamasishwa kuchukua hatua mbalimbali za kupinga na kukabiliana na unyanyasaji huo wa kijinsia ambao siku hizi angalau taarifa ama habari zinasikika kutokana na watu kupata msukumo kwa kutoa taarifa na ni hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo hili linaloonekana katika kukita mizizi.

Lakini kinachosikitisha taarifa nyingi zinatokana ama kujulikana baada ya madhara kutokea na siyo wakati mhusika ama wahusika wakiwa katika kupitia hali hizo ama vitendo hivyo.

Kukithiri kwa vitendo hivyo kumesababisha kuwanyima haki ya msingi ya kuishi wanaouawa lakini pia wale wanaopata vipigo kupata matatizo ya kisaikolojia na kukosa kujiamini.

Miaka ya karibuni, elimu imekuwa ikitolewa katika ngazi mbalimbali ya kuitaka jamii kukemea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanywa na asasi na vyama mbalimbali vya kutetea usawa wa kijinsia.

Hata hivyo, bado hali badala ya kupungua imekuwa ikiongezeka, hivyo ni vema ikaandaliwa mikakati madhubuti ikiwemo mijadala kuanzia ngazi za chini katika shule za msingi na sekondari kuhakikisha elimu na ushauri unatolewa kwa jinsia zote.

Wanaume ndiyo msingi mkubwa wa unyanyasaji huo, kwani wengi wanaona kumpiga mwanamke pale anapokoseaau kwenda kinyume na masuala fulani katika jamii na familia ni kumpiga bila kukaa naye na kuzungumza kujua kiini cha matatizo hayo.

Naamini kwa kutumia majukwaa mbalimbali ni vema sasa yakatumika kutoa elimu kwa wasichana na wavulana kukabiliana na tatizo hili kwenye jamii, kwani likiachwa likaendelea linaweza likawa gumu kukabiliana nalo hapo baadaye na matokeo yake wanawake wengi wakauawa kwa sababu zisizo na msingi.

Ni lazima tufahamu kuwa mapenzi kwa mke au mtu kwenye mahusiano ni furaha na amani iwe kwa mwanaume au mwanamke.

Mfano kama mwanaume ambaye kwa hiari yake ameoa na wana watoto inashangaza kuona anadiriki kumfanya ngoma ya kumpiga mkewe kila wakati mpaka kufikia kumjeruhi au kumuua.

Hakuna binadamu aliye mkamilifu, kwa hiyo hata wanawake kama binadamu wanakosea na wanaweza kurekebishika kwa kujadiliana na kushauriana, kama mwanaume unaona huyo mwanamke hakufai ni vema kuachana kwa amani ili kuhakikisha kila mmoja anaendelea na mambo yake lakini kipigo na mauaji si jawabu hata kidogo.

Lakini kubwa zaidi ni wanawake walioko katika ndoa na mahusiano, si jambo jema kuvumilia vipigo na ukatili ambao mwisho unakuja kukatiza maisha yako halafu ndio ndugu na marafiki wanaeleza mateso uliokuwa ukipitia katika ndoa.

Tena wako wanawake wengine wamekuwa wakitishiwa kuuawa mara kwa mara na wenza wao lakini wakaamini ni maneno tu na matokeo yake wanakuja kuuawa, lakini pia ndugu, jamaa na marafiki tutumie hekima na busara badala ya kushinikiza ama kumlazimisha mwanamke anayepitia manyanyaso ya vipigo na vitisho avumilie, halafu likitokea la kutokea tunabakia kusema alikuwa anateseka sana wakati huyo keshapoteza maisha na kaacha familia na watoto wake.

Wako wanawake wengine pia wamekuwa wakivumilia vipigo na mnyanyaso kwa kile wanachosema akiondoka katika ndoa ama mahusiano ya manyanyaso watoto hataweza kuwalea, lakini lipi bora watoto wako waishi wakikuona au wakuone umepoteza maisha au umebakia mwenye ulemavu na baba yao akiishia jela na wakabakia kulelewa na ndugu pekee.

Wanawake tutumie hekima tuliopewa na Mungu, manyanyaso na vipigo sio mahusiano yenye furaha na amani, chukua hatua, jamii na serikali uwepo mkakati madhubuti wa kukemea na kupinga ubabe na vipigo wanavyofanyiwa wanawake ili kuokoa uhai wao na jamii kwa ujumla.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi