loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Askofu Gamanywa: Tuchague mzoefu kulinda maslahi ya Taifa

Oktoba 7 mwaka huu, Askofu Sylvester Gamanywa alizindua kitabu chake kiitwacho Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka. Yafuatayo ni mahojiano maalumu baina ya mwandishi na askofu huyo kuhusu audhui ya kitabu chake.

SWALI: Wakati wa uzinduzi wa kitabu chako cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka, ulihutubia mkutano wa waandishi wa habari kwa kusema “haiwezekani kumtenganisha Rais Dk John Magufuli na Maslahi ya Taifa.” Ulikuwa na maana gani kwa kauli hiyo?

MAJIBU: Kabla ya kujibu swali lako naomba kwanza nitoe tafsiri sahihi kuhusu maana ya ‘maslahi ya taifa. Maana yake ni masilahi ya taifa kwa ujumla linaloshikiliwa kuwa chombo huru tofauti na masilahi ya maeneo ya chini, au vikundi na au mataifa mengine au vikundi vya kitaifa.

Kwa tafsiri ya Tanzania maslahi ya nchi ni ardhi, rasilimali za asili, kuanzia maji, mimea, wanyama na madini. Mambo mengine ambayo ni maslahi ya taifa ni haki za kiraia kwa raia wote pasipo upendeleo wala ubaguzi wa kwa maslahi ya maeneo ya kikanda, au vikundi, au mataifa mengine au vikundi vya kitaifa.

Sasa nijibu swali lako la msingi. Nilisema “hatuwezi kumtenganisha Rais Dk John Magufuli na maslahi ya Taifa” kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha katika kusimamia na kudhibiti usalama wa maslahi ya taifa pasipo kujali maslahi ya vikundi vya kisiasa, kidini na kimaeneo.

Ushahidi wa kitafiti kutoka vyombo vya kimataifa ndio umemthibitisha hivyo, na sisi watanzania ambao ni wazalendo tumethibitisha hivyo.

Maelezo ya kina kuhusu uzalendo na Maslahi ya Taifa nimevichambua ndani ya kitabu nilichokizindua cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka. Kila atakayekisoma atajua ukweli wa mambo ulivyo.

SWALI:  Unataka jamii iamini kwamba watu wasipomchagua Rais Magufuli hawajali maslahi ya Taifa?

MAJIBU: Kuna kuwepo kwa maslahi ya Taifa, na kuna kuwepo kwa mtu mwenye uwezo wa kusimamia, kudhibiti na kulinda maslahi ya Taifa. Kutokuwepo kwa Rais Magufuli madarakani kunamtegemea Mwenyezi Mungu aliyemteua tangu mwaka 2015 na kumpa mamlaka aliyo nayo.

Hata hivyo, hoja ninayotilia mkazo hapa ni jamii kupambanua mgombea wa urais kwa kigezo cha uwezo na uzoefu wa mgombea alionao katika kusimamia na kulinda maslahi ya Taifa kwa manufaa ya raia wote.

Pamoja na kuwepo kwa wagombea wa vyama vyote wanaojinadi ili wachaguliwe kushika mamlaka ya nchi, kwa wakati huu kila mtanzania ambaye ni mzalendo wa kweli, nina imani atapiga kura ya uzalendo kwa kumchagua kiongozi mwenye sifa na uwezo pamoja na uzoefu wa vitendo katika kusimamia na kulinda maslahi ya Taifa.

Maelezo ya kina kuhusu uzalendo na Maslahi ya taifa nimevichambua ndani ya kitabu nilichokizindua cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka. Kila atakayekisoma atajua ukweli wa mambo ulivyo.

SWALI: Askofu, kwa maneno yako na mtazamo wako unatafsiriwa kwamba mwaka huu umejiingiza kwenye siasa moja kwa moja na umeacha kuhubiri Injili. Unajiteteaje hapo?

MAJIBU: Mimi nimeshiriki chaguzi zote kuanzia awamu ya tatu, awamu na ya nne. Na kila awamu niliandika kitabu chake kama nilivyofanya mwaka huu.

Hata hivyo swali lako linatoa mtazamo kwamba mtumishi wa Mungu, “kujiingiza kwenye siasa” ni kuiacha imani na kuacha utumishi wa Kristo. Huu ndio mtazamo potofu ambao shetani ameutumia miaka yote kuwafanya watumishi wa Injili wakae kimya na kuchagua kutokuwa na upande wowote (neutrality), hata katika mambo yenye kuathiri maadili ya kiimani na kuharibu maslahi ya Taifa.

Majuzi tumetembelewa na Rais wa Malawi Mheshimiwa Razarus Chakwera ambaye ni Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kipentekoste la Assemblies of God, Malawi lakini leo ni Rais wa Malawi.

Je! Amerudi nyuma kiroho? Ameiacha injili ya Kristo kwa kuingia katika siasa? Je, hatusomi katika maandiko kwamba wafalme wa nchi huwekwa na Mungu mwenyewe na wametajwa kuwa nao ni “watumishi wa Mungu” (RUM.13:1-7)

Yesu Kristo alisema: “Sisi ni nuru ya Ulimwengu” kama taa inavyotoa nuru gizani. Muktadha wa maneno ya Yesu ni watumishi wa kweli wa Kristo kusema kweli ya kiinjili wakati ule ambapo sera za uongo na upotoshaji dhidi ya kweli ya Kristo zinapojitokeza.

Injili ya Kristo sio kuwafanya wenye dhambi kutubu kwenye mikutano ya hadhara. Lakini Yesu alitutuma wahubiri wa Injili kuwafuata wenye dhambi huko huko waliko kwenye majukwaa ya kijamii na kisiasa na kusema ukweli unaotakiwa wakiwa kama raia wazalendo katika jamii.

Injili ya Kristo haiishii kwenye kumfanya mwenyedhambi kutubu, bali inatakiwa kumfanya mwamini kuwa raia mwema na mzalendo kwa nchi yake.

Kwa taarifa yako, ninapohimiza jmaiii kupiga kura za uzalendo na sio kura za usaliti hii ni “huduma ya kichungaji kwa jamii”. Yesu alisema mchungaji mwema wa kondoo ni yule anayeona mbwamwitu wanakuja akaamua kuwalinda kondoo wake kwa kujitoa mhanga uhai wake.

Hii ndiyo kazi ninayoifanya kwa sasa kwa majira haya. Nawanusuru kondoo wa kijamii kulinda uraia mwema kwa kuepukana na wagombea na washabiki wa kisiasa ambao wamepania kubadilisha sheria za maadili mema ili kuifanya nchi ya mashoga.

Nimeyaeleza haya kwa kina kwenye kitabu changu kipya cha Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka.

SWALI: Je, wewe huamini kwamba kambi ya upinzani nayo pia inajali maslahi ya Taifa na ndiyo maana ilani za vyama vyao zimeahidi kuwaletea maendeleo ya watu moja kwa moja badala ya maendeleo ya vitu tu?

MAJIBU: Hapa si suala la mimi kuamini au kutokuamini. Ni suala la kuzitathmini ilani za vyama kwa kigezo cha maslahi ya Taifa yasiyohusisha viashiria vya kubomoa misingi ya utaifa wetu na kuturudisha kwenye maslahi ya vikundi na maeneo ya kikanda ambapo Tanzania tulikwisha kuvuka viwango vya ubaguzi wa kimaeneo na kimakundi katika jamii.

Kwa tathmini ya jumla ilani za baadhi ya wagombea wake wanapinga mambo ya msingi ya Maslahi ya Taifa pamoja na maendeleo ya kitaifa yanayoonekana waziwazi kwa macho, na badala yake wamejikita kwenye nadharia za maslahi ya kimakundi au itikadi za vikundi.

Kinachotisha zaidi ni dhana za baadhi ya wagombea wanaotangaza hadharani kwamba kama wakipewa kuongoza nchi wataweka rehani rasilimali za nchi ili kupata mikopo kutoka kwa matajiri wa nje wakifikiri hii ndiyo njia ya kuwaletea wananchi maendeleo ya moja kwa moja. Kwa lugha nyingine wakipewa mamlaka ya nchi hatua ya kwanza ni “kuuza nchi kwa mabeberu”!

Maelezo ya kina kuhusu uzalendo na maslahi ya Taifa nimevichambua ndani ya kitabu. Kila atakayekisoma atajua ukweli wa mambo ulivyo.

SWALI: Askofu, hebu tufafanulie kwa kina, ni nini maana sahihi ya maneno haya uzalendo na usaliti. Dhana hii umeitoa wapi?

MAJIBU: Kwanza suala la uzalendo na usaliti si dhana kama unavyoitafsiri wewe. Mimi ninaongelea uhalisia wa mazingira ya kisiasa yaliyoghubika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu wa 2020.

Tangu mwanzo nilipotaja maneno haya ya usaliti na uzalendo nilikwisha kuona waziwazi kwamba ushindani wa kisiasa uliopo hivi sasa sio wa ushawishi wa ubora wa ilani zenye kusimamia na kulinda Maslahi ya Taifa, bali ni maneno ya chuki, shutuma, tuhuma, na hisia zilizojaa hasira na vinyongo.

Lakini pia kuna upande mwingine wa kizalendo ambao unakiri na kupongeza juhudi za maendeleo ya kiuchumi yaliyofanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Tano na wenye kuhamasisha wapiga kura kupiga kura za uzalendo kwa ajili ya kumchagua kiongozi mwenye uwezo na uzoefu wa kulinda Maslahi ya Taifa kwa manufaa ya raia wote.

Mzalendo ni mtu anayedhihirisha kuwa anaipenda nchi yake na yuko tayari kuitetea na kuifanyia mema yote hata kuifia.

Mzalendo anapenda wakati wote kuiendeleza na kuitetea  nchi yake, viongozi, mipango yake na watu wake. Uzalendo pia unahusu utayari wa kila raia  kulinda uhuru wa nchi na mipaka yake, amani na utulivu kwa raia, pamoja na kuwa tayari kulinda  rasilimali za nchi kwa maslahi ya raia wote.

Uzalendo huambatana na tabia ya kutii na kuheshimu utawala na mamlaka za nchi.

Lakini usaliti ni “tendo la kutoa siri za mtu, kikundi, au nchi kwa adui wa mtu, kikundi au nchi.” Kwa hiyo, usaliti ni tendo. Msaliti ni mtu anayemsaidia adui wa mtu au taifa kwa kumpa taarifa za siri zitakazotumika kusababisha madhara kwa msalitiwa. Aidha, msaliti ni mtu yeyote anayekabidhi au kufichua siri au taarifa za usalama wa mtu au nchi kwa hila pasipo kujulikana kwa msalitiwa. 

Ziko aina za usaliti, kuanzia usaliti baina ya marafiki, familia na jamii lakini usaliti unaolengwa kwenye kitabu changu ni usaliti dhidi ya nchi.

Itaendelea...

 

VYAMA vingi vya michezo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi