loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Afya ya akili ni changamoto kwa vijana, jamii

JUZI Oktoba 10, ilikuwa siku ya kimataifa ya afya ya akili. Siku hii wataalamu huitumia kuamsha ari ya jamii kutambua tatizo la afya ya akili, kujua kinga na hata matibabu inapotokea mtu kupata tatizo la akili.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mtu mmoja hufariki dunia katika kila sekunde 40 kwa kujiua.

Pia shirika hilo linabainisha kuwa nusu ya matatizo yote ya akili duniani yanaanza katika umri wa miaka 14 na mengi hayabainiki wala kutibiwa, jambo linaloweka mustakabali wa vijana wengi njia panda.

WHO linasema mzigo wa matatizo ya akili miongoni mwa vijana barubaru unasababisha mambo makubwa matatu: msongo wa mawazo; kujiua ikiwa ni sababu inayoshika nafasi ya pili kwa vifo vya vijana kati ya umri wa mika 15 hadi 19; na tatizo linaloongoza ni matumizi mabaya ya pombe na mihadarati.

Athari za kutoshughulikia matatizo ya afya ya akili kwa vijana ni kubwa kwa mujibu wa shirika la afya duniani, na mara nyingi zinaendelea hadi ukubwani na kuwakosesha fursa ya kushamiri katika maisha yao.

Asilimia 20 ya vijana duniani kote wana shida ya afya ya akili, katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati karibu asilimia 15 wamefikiria kujiua.

Tatizo la shida ya afya ya akili siyo la kibinafsi, kwa maana ni la kijamii na kiuchumi pia. Bado afya ya akili ya watoto na vijana mara nyingi imekuwa ikipuuzwa katika mipango ya afya kitaifa na kimataifa.

Kuna watoto wachache sana ambao wanapata programu za kufundishia juu ya jinsi ya kudhibiti hisia ngumu. Hayo yamethibitishwa na Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani. Dk Ghebreyesus anaongeza kuwa, “watoto wachache sana wenye shida ya afya ya akili wanapata huduma wanazohitaji na hivyo suala hili lazima ibadilike.”

Afya ya akili ni dhana inayoweza kutazamwa kijamii na kutafsiriwa namna tofauti katika jamii tofauti, makundi, tamaduni, taasisi na wataalamu mbalimbali.

Wote hao wana njia tofauti ya kueleza asili, sababu, ustawi au uhalisia wa afya ya akili na utekelezaji unaofaa katika kuitunza au kutibu.

Kwa hiyo, afya ya akili inategemeana na mtazamo wa jamii, wataalamu ya afya ya akili hutibu matatizo au magonjwa ya akili kulingana na mtazamo wa mtu kutoka jamii husika.

Mfano, wengine hulinganisha muathirika na mazingira yake kama vile utamaduni wake, kipato chake, itikadi za kisiasa, kidini, na kijamii kwa ujumla wake. Kwa kufuata mtazamo huo inamsadia mtaalamu kuchagua njia sahihi ya kutibu matatizo ya akili

WHO linabainisha kuwa matatizo ya akili ni tatizo la maelfu ya watu katika kila sehemu ya dunia na yana matokeo mabaya juu ya maisha ya watu wanaowapenda. Mtu mmoja kati ya watu wanne hupatwa na tatizo la akili wakati fulani katika maisha yake.

Hata hivyo, japo watu wengi sana wana matatizo ya akili, matatizo hayo yanabaki yenye kufichwa, yenye kudharauliwa, na yenye kusemwa vibaya.

Afya yako ya akili inahusiana na jinsi unavyojihisi na akili yako inavyofanya kazi. Afya yako ya akili ni muhimu sana kwa sababu inaweza kuathiri afya yako ya kimwili na ustawi wako wote.

Wataalamu wanaeleza tafsiri ya tatizo la akili kuwa ni kutumika vibaya sana kwa akili ya mtu, kushindwa kuzuia namna anavyojisikia moyoni, na kushindwa kuzuia tabia zake. Mara nyingi, hali hiyo inazuia uwezo wa mtu wa kushughulika na wengine na kushughulika na mahangaiko ya maisha.

Kwa watu wengine dalili zinaweza kuwa nyingi na zinaweza kuoneshwa kwa muda mrefu, ikitegemea mtu, ugonjwa na hali. Matatizo ya akili yanaweza kuwapata watu wa namna zote, rika zote, desturi zote, rangi zote, dini zote, walio na elimu na wasio na elimu, matajiri na masikini.

Matatizo ya akili hayatokani na udhaifu wa mtu au tatizo katika hali ya mtu. Wakati mtu ana shida ya afya ya akili, inamaanisha ustawi wao wa akili hauko sawa kama vile mwili wako unapoumia.

Kuna sababu nyingi ambazo watu hupata matatizo ya akili. Wanaume wengine huzaliwa katika hatari kubwa zaidi na wengine wana hatari baada ya kukabiliana na mambo kama msongo wa mawazo au shida.

Wakati mwingine matatizo ya afya ya akili yanaweza kuwa madogo na kuisha kwa urahisi. Nyakati nyingine yanaweza kuwa mabaya na kufanya iwe vigumu kwa watu kufanya kazi kama kawaida.

Katika dunia tunayoishi, kila mtu anapenda maisha ya furaha. Na watu wanapopata misukosuko ya kimaisha siyo kwa sababu hawataki wafanikiwe, hivyo wengi hujikuta wakitawaliwa sana na wasiwasi na huzuni nyingi.

Ni kitu cha kawaida kupata wasiwasi mtu anapopatwa na changamoto, lakini endapo wasiwasi na hofu vinakufanya ushindwe kumudu maisha yako ya kawaida kama unavyopenda, unaweza kuwa una tatizo la afya ya akili linalojulikana kitaalamu kama anxiety disorder.

Wasiwasi ni hisia inayohusiana na hofu. Kila mmoja atasikia wasiwasi wakati fulani katika maisha yake. Wasiwasi unaweza kuwa suala la afya ya akili wakati linapotokea mara nyingi au unapohisi kama una hali hiyo wakati wote.

Mbali na wasiwasi, kila mtu huwa na huzuni wakati fulani, hiyo ni sehemu ya kawaida na ya afya kama mwanadamu. Lakini unapokuwa na huzuni na hali hiyo haiishi au kuanza kuathiri uwezo wako wa kuishi maisha yako ya kawaida basi ni tatizo la akili.

Kama ilivyo kwa wasiwasi, huzuni inaweza kuwa kitu ambacho watu wanazaliwa nacho na wengine huwatokea kutokana na sababu ya mambo katika maisha yao.

Wakati fulani rafiki yangu mmoja aliniambia “Ninapokuwa na huzuni hujitenga na wengine. Na nikialikwa mahali, ninatoa sababu za kutoenda. Mara nyingi watu wa familia yetu hawajui kwamba nina huzuni. Wao hufikiri niko sawa.”​

Nyakati nyingine, huenda ukajua sababu inayokufanya uhuzunike lakini huenda nyakati nyingine usijue. “Si lazima niwe katika hali mbaya ili niwe na huzuni,” anasema na kuongeza, “huzuni inaweza kutokea wakati wowote, hata wakati ambapo sina matatizo. Ni jambo lisiloeleweka, lakini ndivyo ilivyo!”

Aliyeathiriwa na tatizo hili hukosa hamu ya kuishi, hukosa kufanya mambo kwa makini na nguvu na hupata mabadiliko katika hamu ya kula na mpangilio wa usingizi. Watu hawa huwa na hali ya lawama. Ukosefu wa tumaini huwafanya kuwa na mawazo ya kujiua.

Jamii inapaswa kuwasaidia watu wa aina hii kuwa hakuna haja ya kuwa na aibu ikiwa unasumbuliwa na suala la afya ya akili. Ni jambo ambalo wanaume wengi wanasumbuliwa, hata kama hawazungumzi juu ya hili.

Unaweza kuanza kwa kuzungumza na marafiki au wapendwa wako kupata msaada. Wajulishe kwamba hujisikii vizuri. Ikiwa hujisikii kama unaweza kuzungumza na marafiki au hata kama utazungumza nao, unapaswa kuzungumza na mtaalamu wa afya kwenye zahanati karibu yako. Baadhi ya maswala ya afya ya akili yanahitaji ushauri au hata dawa.

Mkurugenzi wa Afya ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, Fileuka Ngakongwa, anasema sonona (depression disorder) ni chanzo kikuu cha magonjwa ya akili.

Dk Ngakongwa anasema magonjwa yanaongezeka na kwamba takwimu za wagonjwa wa akili kwa mwaka 2019/2020 zimepanda hadi kufikia watu 32,307 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2018/2019  ambapo wagonjwa walikuwa 29,166.

“Hospitali inahudumia wagonjwa wa ndani na nje ambapo kwa mwaka 2018/2019 wagonjwa wa nje walikuwa 20,571 na mwaka 2019/2020 wagonjwa wa nje walikuwa 21,183,” amesema.

Kwa upande wa huduma katika hospitali hiyo kubwa nchini, Dk Ngakongwa anasema zimeendelea kuboreshwa ambapo idadi ya watoa huduma na vifaa vya kisasa vimeongezwa pia.

Anasema upatikanaji wa dawa umesababisha wagonjwa wengi kupona na kurudi katika hali zao za kawaida.

 

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

 

 

BARAZA la Kiswahili la ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi