loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tunapoingia kwenye uchaguzi na wosia wa Mwalimu Nyerere

“NAJUA nitakufa, sitapona ugonjwa huu… Nawaacha watanzania wangu, najua watalia sana nami nitawaombea kwa Mungu, Naondoka nikiwa nimewaachia Taifa moja, lenye umoja na amani. Wosia wangu kwao waipende nchi yao kama wanavyowapenda mama zao. Wajue hawana nchi nyingine zaidi ya Tanzania”.

Huu ni ujumbe wa mwisho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kabla ya kuaga dunia Oktoba 14 mwaka 1999 kwenye Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza.

Leo, wananchi wa Tanzania wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 21 tangu kufariki kwa Rais wa kwanza na Baba wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Nyerere.

Nikiri wazi kuwa mimi sikupata bahati ya kuwa karibu na Mwalimu Nyerere zaidi ya kumsoma vitabuni na kumwona kwenye vyombo vya habari na pengine ni miezi minne kabla ya kifo chake ambapo Mwalimu alikuja Kalenga mkoani Iringa kushiriki mazishi ya aliyekuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Adam Sapi Mkwawa tarehe 28 Juni 1999.

Nadhani kwa kuwa lilikuwa tukio la msiba niliweza kubahatika kumshuhudia Mwalimu Nyerere kwa umbali wa takribani mita 20 hivi ambapo aliongea kwa kifupi sana kusikitishwa na kifo cha Adamu Sapi Mkwawa.

Kwa mujibu wa wasifu wa Mwalimu uliotolewa wakati wa mazishi yake, kabla ya kujitosa katika masuala ya kisiasa alikuwa ni mwalimu, tasnia ambayo ilimpa jina ambalo alitambulika nalo kote duniani.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la udhamini na Kamati ya nne ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.

Mzee Phillip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara akiwa mkoani Singida hivi karibuni alimwelezea Mwalimu Nyerere kwamba alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania  baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomng’oa Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

Tarehe 5 Februari 1977 Mwalimu aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Afro Shirazi Party na kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa mwenyekiti wake wa kwanza.

Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiari yao baada ya kutawala kwa muda mrefu akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi na akiwa bado ana nguvu.

Alipostaafu urais mwaka 1985 na kumpisha Ali Hassan Mwinyi kuliongoza taifa la Tanzania, alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Hata hivyo, aliendelea kuongoza CCM hadi mwaka 1990 na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.

Kati ya mafanikio makubwa ya Nyerere kuna: kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe "kisiwa cha amani".

Ni kutokana na mafanikio hayo Kanisa Katoliki lilianzisha mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa mwenye heri na hatimaye Mtakatifu.

Baadhi ya wanasiasa wakongwe na viongozi waliopata kufanya kazi enzi za Mwalimu wamemwelezea Mwalimu Nyerere kuwa  alikuwa ni mtu wa upendo mkubwa, siyo tu kwa nchi yake, bali  na mataifa yote ya Afrika.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi anamwelezea kama kiongozi aliyefanikiwa kutoa mchango mkubwa kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile Zimbabwe Afrika Kusini, Namibia, Angola na Msumbiji na kwamba katika miaka ya 1958 Mwalimu alilikabidhi Taifa la Tanzania kwa Mama Bikira Maria, mama wa Yesu Krito.

Rais John Magufuli ni miongoni mwa viongozi ambao wameonekana kwa namna ya pekee kufuata nyayo na misingi ya  Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika masuala kadhaa aliyatoa kwenye hotuba zake kuanzia kwenye  maeneo ya siasa, uchumi, na dini.

Katika suala la uongozi Mwalimu alisisitiza nidhamu na maadili ya uongozi.  “Inatakiwa ukiulizwa swali kwamba huyu atapiga vita rushwa? Jibu litoke ndani ya moyo kwamba ndiyo, anaweza…Nchi yetu ni maskini bado haijawa ya matajiri hivyo tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wetu na matatizo ya wananchi, tunataka nchi yetu ipate kiongozi safi,'' alisisitiza  Mwalimu.

Tumeshuhudia katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli ikikemea kwa nguvu zote  mafisadi na wala rushwa, wengi wao wamepandishwa  mahakamani na kuzilipa.

Kwenye suala la ujinga, maradhi na umaskini, Mwalimu Nyerere alisisitiza juu ya mambo haya makuu matatu, ambapo alisema kama Tanganyika na baadaye Tanzania itafanikiwa kuyamaliza basi itakuwa miongoni mwa nchi itakayoendelea zaidi duniani.

Rais Magufuli ameelekeza fedha nyingi kwenye maeneo ya kimkakati kama ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli, ununuzi wa ndege na utoaji elimu bure huku wigo wa mkopo kwa ajili ya elimu ya juu ukiongezeka.

Ndoto ya Mwalimu Nyerere ya kuhamishia utawala wa Tanzania mjini Dodoma imetimia katika kipindi hiki.

Mwalimu alipenda Muungano, katika vitu ambavyo alikuwa akitamani sana kufanya ni kuunganisha nchi za Afrika mashariki na kuwa na uongozi wa pamoja. Ingawa hakufanikiwa katika hilo, alifanikiwa katika kuunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Rais Magufuli amekuwa ni muumini wa  kuungana si tu kwa Afrika Mashariki bali Bara zima la Afrika na tumeshuhudia mwishoni mwa mwaka jana Rais Magufuli akifanya ziara kwenye nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe, lengo likiwa kuwa na muungano na ushirikiano wa kiuchumi ulioimarika ili kuwa na nguvu za pamoja.

Suala la udini na ukabila ni mambo nyeti ambalo Mwalimu Nyerere aliyazungumzia katika hotuba nyingi alizowasilisha ambapo katika kipindi hiki Rais Magufuli amewaunganisha waumini na viongozi wa dini na madhehebu yote hasa katika kipindi cha ugonjwa wa covid-19 kwa kufunga na kumwomba Mwenyezi Mungu ili kuondokana na ugonjwa huo.

Akihutubia katika kampeni Kinyerezi jijini Dar es Salaam hivi karibuni Rais Magufuli alisema taifa la Tanzania limesimamia misingi iliyoachwa na baba wa taifa na ambapo alisisitiza kuwa Tanzania inamwamini mwenyezi Mungu.

“Tanzania ina Mungu kwa sababu anatusikia. Na katika kipindi cha corona uchumi wetu ulizidi kupaa hata kutangazwa kuwa nchi ya uchumi wa kati. Hongereni watanzania kwa kushikamana,” aliongeza Rais Magufuli.

Ni Rais Magufuli pekee katika dunia hii ambaye aliliweza hilo licha ya hila za kila aina za mabeberu na mashirika makubwa duniani kutaka kumyumbisha kwenye msimamo huo lakini baadaye wamekuwa wakimuunga mkono kwa aibu baada ya kushindwa.

Nyerere alikemea suala la ukabila kila wakati alipopata nafasi ya kuzungumza na hakutaka kabisa kuwe na maswali kama wewe ni kabila gani? Ni katika hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, si kwa kawaida nchini Tanzania kuulizana kuhusu masuala ya ukabila.

''Mambo haya ya kuchochea chuki za dini yakianza na tukayapa nafasi hayana simile, na ikifika wakati yakashika kasi hakuna wa kuzuia,'' alisisitiza Mwalimu.

Hayo ni baadhi tu ya mambo aliyokuwa akisisitiza sana Mwalimu Nyerere katika hotuba zake, hii leo Watanzania tunaadhimisha miaka 21 ya kifo cha Baba wa Taifa letu, lakini bado falsafa zake zinaendelea kuishi.

Lakini jambo kubwa zaidi ni hili, falsafa zake zinaendelea kuishi katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wa kuchagua Rais, wabunge na madiwani ambapo ifikapo Oktoba 28 wananchi watapiga kura kwa  viongozi ambao watawaongoza kwa miaka mingine mitano 2020-2025.

Wakati  leo  tunamuenzi  na kukumbuka  miaka  21 ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni muhimu kwa wapigakura kujua thamani yao ya kutumia haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo huku wakikumbuka wosia wa  Baba wa Taifa alioutoa  katika kipindi kifupi  kabla ya kuaga dunia Oktoba 14 mwaka 1999 kwenye Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza.

 

VYAMA vingi vya michezo ...

foto
Mwandishi: John Mapepele, Singida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi