loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Jerry Silaa aahidi kuleta madaktari kutoka Korea

MGOMBEA ubunge Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jerry Silaa amesema akichaguliwa mkakati wake wa kwanza ni kuboresha Hospitali ya Mama na Mtoto Chanika kwa kuleta madaktari na wauguzi kutoka Korea ili watoe huduma kwa wananchi.

Mgombea huyo alitoa ahadi hiyo wakati akifanya kampeni katika kata ya Chanika alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo kutoka CCM, Ojambi Masaburi na kumuombea kura mgombea urais wa CCM, John Magufuli.

Alisema wakati akiwa Meya wa Ilala, hospitali hiyo ilijengwa kwa ufadhili wa serikali ya Tanzania na Korea Kusini, hivyo atazungumza na nchi hiyo  kwa ajili ya kuipatia madaktari bingwa.

"Nitakapo chaguliwa kuwa Mbunge wa Ukonga mikakati yangu ni kuwaleta madaktari na wauguzi kutoka Korea waje kutoa huduma Hospitali ya Mama na Mtoto Chanika ambayo ilijengwa na serikali pamoja na ufadhili wa serikali ya Korea Kusini wakati nikiwa Meya, sasa hivi naomba ridhaa niwe Mbunge wenu ili niweze kuleta maendeleo," alisema Silaa. 

Alisema mikakati yake mingine ni kuwawekea mipango mizuri wafanyabiashara kwenye jimbo hilo kwa kuwasimamia wasinyanyaswe kwa kuwa kuna fursa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Silaa, maeneo yote katika jimbo hilo ambayo yamekosa umeme kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndani ya miaka mitano atahakikisha umeme huo umewafikia.

Kwa upande wake, Masaburi alisema akichaguliwa mkakati wake wa kwanza ni kuwawezesha vijana, wanawake na wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya serikali ili waweze kujishughulisha na miradi na kujenga barabara zote za mitaa.

Alitaja mikakati mingine ni kujenga shule mbili ili watoto wasome karibu na maeneo wanayoishi na pia ataboresha sekta ya afya kwa manufaa ya wananchi.

Alisema pia atasimamia makundi ya wazee wa kata ya Chanika katika fedha za mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) ili kuwawekea utaratibu maalumu wasisumbuliwe.

Aliwataka wananchi wa Chanika wajitokeze kwa wingi Oktoba 28 kumpigia kura Magufuli na Silaa ili waweze kupata maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa CCM ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kampeni katika kata hiyo, Makongoro Nyerere, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam na Jimbo la Ukonga kuipigia kura CCM ili waweze kushika nafasi ya kwanza.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi