loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wazazi Chamwino na tuhuma za kuwaharibu mabinti zao

“MZAZI anadhani ni bora ampe mtoto wake vidonge vya kupanga uzazi au ampeleke zahanati akawekewe kipandikizi au kitanzi. Yaani anaona heri mtoto apate maradhi mengine kuliko mimba.”

Hayo yanasemwa na Mganga wa Kituo cha Afya Mpwayungu kilichoko Chamwino mkoani Dodoma, Ambaliche Boniface.

Anasema wazazi wamekuwa wakifika kituo cha afya kuomba watoto wao watumie uzazi wa mpango kama njia ya kuwakinga wasipate mimba wakiwa shulenina hivyo kukatisha masomo.

“Yaani hapa kituoni wazazi wanakuja kuleta watoto kuanzia miaka 14 na kuendelea kutaka wafungwe uzazi lakini sisi hatuna huduma hiyo. Hata tukiwaambia hatuna hiyo huduma wanabembeleza. Lakini tumekuwa tukiwaambia siyo salama sana kiafya kwa binti mdogo kuanza kutumia njia za kuzua mimba,” anasema

Mganga huyo anawataka wazazi kukaa na watoto wao na kuwaelimisha madhara ya kufanya mapenzi wakiwa na umri mdogo, tena bila kutumia kinga.

“Sisi tunaona kama wazazi wengi hawatimizi wajibu wao. Hawakai kwenye nafasi zao na ndio wanaona ni heri mtoto afuate uzazi wa mpango, na hivyo kama ni ngono ashiriki ru alimradi asipate mimba, akafukuzwa shule,” anasema.

Anasema ushauri huo wanautoa hata kwa wazazi wenye watoto wa kiume na vijana ambao wanajitegemea wakiwemo waendesha bodaboda waache kufuata mabinti walioko shule wakati kuna wanawake wengi mitaani.

Anasema wameanza kushauriana na viongozi wa vijiji ili watoe elimu kuhusu madhara ya mimba katika umri mdogo.

Muuguzi katika zahanati ya Manchali wilaya ya Chamwino, Gaudensia Mpokwa naye anakiri kwamba wazazi wamekuwa wakifika zahanatini kwao kuwaomba mabinti zao wawekewe vitanzi au vipandikizi lakini wamekuwa wakiwakatalia.

Gaudensia anakiri pia kwamba tatizo la mimba kwa watoto wa shule katika wilaya ya Chamwino ni kubwa linahitaji kufanyiwa kazi haraka.

“Mara nyingi shule inapoleta watoto hapa kwenye zahanati kupimwa hali zao, hawakosi watoto watano kugundulika wakiwa na ujauzito. Ni vyema sasa wasichukuliwe kama watoto bali wapewe elimu ili wajitambue,” anasema.

Mratibu wa dawati la mtoto kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai, anakiri watumishi wa kada ya afya katika wilaya hiyo kukumbwa na changamoto hiyo ya wazazi kutaka watoto wao wapewe huduma ya uzazi wa mpango.

“Cha msingi, wao wafuate maadili na miiko ya kazi zao, lakini pia wawashauri na kuwaambia madhara yake,” anasema.

Anasema ingawa zahanati na vituo vya afya vya serikali vinakataa kutoa huduma ya uzazi wa mpango kwa wanafunzi pengione wanaweza kupata huduma kwenye baadhi za zahanati na hospitali zinazokiuka maadili.

“Wanaweza wakakosa kwenye zahanati na vituo vya afya vya serikali na wakapata huduma hiyo kwenye hospitali binafsi. Jambo la muhimu ni wasichana wajitambue ili kuepuka mimba za utotoni,” anasema.

Katekista wa Kanisa la Anglikana kata ya Mpwayungu, Grace Omari anasema wazazi wanaogopa mimba kuliko tatizo zima la ngono zembe na ndio maana wanashauri watoto wao kutumia kipandikizi, kitanzi na vidonge vya uzazi wa mpango.

Anasema kila mzazi akisimama kwenye nafasi yake ipasavyo tatizo la mimba za utotoni litapungua.

Anasema wazazi wanatakiwa kuchukua jukumu la malezi kwa kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu ya maisha na sio kuwaacha watoto hao wakajilea wenyewe na hivyo kujiingiza kwenye ngoni mapema.

Mkazi wa Mpwayungu, Janeth Ndahani, anasema baadhi ya wazazi wamekuwa hawaoni umuhimu wa elimu na hivyo kushindwa kuhamasisha watoto wafanye vizuri darasani ili wakifeli wakaolewe.

“Mtoto ananunuliwa kioo, wanja, rangi ya mdomo, nguo mpya na vingine na anaambiwa usipofaulu nitakununulia vingi zaidi ya hivyo? Kwenye mazingira kama hayo mtoto ataona umuhimu wa shule kweli?” Anahoji.

Anasema ifike wakati jamii ione umuhimu wa kuwalinda watoto wa kike ili wawe salama na hatimaye kupunguza mimba za utotoni na kutumiza ndoto zao.

Shehe wa Kijiji cha Mpwayungu, Nurdin Mbawala anasema kuna mambo mengo yanayochangia watoto wa kike kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo.

Anasema baadhi ya wazazi wanawatumia watoto wao wa kike kuanzia darasa la nne kuuza pombe za kienyeji vilabuni, hali inayowaweka katika uwezekano mkubwa wa kushiriki vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo.

Kiongozi huyo wa dini anasema vitendo vya wazazi kupeleka watoto vilabuni vimekithiri sana licha ya mtendaji wa kijiji hicho, Selemani Kibakaya kutembea na fimbo kuwasaka wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto lakini jambo hilo limekuwa likiendelea.

Shehe Mbawala anawataka viongozi wa vijiji kuweka mikakati kuhakikisha hakuna mtoto anayekwenda kilabuni kuuza pombe.
“Mtoto mdogo wa kike ndio maziwa yanaanza kutoka tena yuko darasa la nne anashinda kilabuni kuuza pombe, huyo mtoto anajengewa mazingira gani, usalama wake ukoje?” Anahoji.

Anasema wazazi wamekuwa wakitumia watoto kama mitaji ya kuvuta walevi na utaona wengi wanapenda kuhudumiwa na watoto kama hao.
“Huo ni ukatili wa hali ya juu sana, hapo mzazi hawezi kuona shida kumuuza mtoto wake maana kuna watoto walishaulizwa kwa nini wanauza pombe wakasema mama zao waliwaambia kama watakataa kufanya biashara hiyo hawataweza kununuliwa sare za shule au madaftari,” anasema.

Badala ya wazazi kulinda watoto wao kwa vitendo vinavyoweza kuwaletea hatari ya kupata mimba za utotoni wamebuni njia ya kuwapeleka kuwapeleka watoto wao hospitali ili waanze kutumia njia ya uzazi wa mpango.

“Ni muhimu sana suala hili livaliwe njuga ili kuhakikisha watoto wa kike au hata wa kiume hawafanyi kazi ya kuuza pombe kwenye vilabu,” anasema.

Mwalimu Sane Nshashi wa shule ya Msingi Nagulo Mwitikila anasema wakati wa kutungwa kwa sheria ndogo ndogo suala la watoto kutumikishwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji liangaliwe na kutungiwa sheria.

Anasema tatizo hilo limekuwa na athari kubwa ka watoto wa kike kwani wanashinda vilabuni hadi usiku wa manane na kukosa muda wa kujisomea na hata kupumzika.

“Ni vyema wazazi wawekewe mipaka kisheria na iwe marufuku watoto kutumikishwa vilabuni na muda wa kuanza kuuza pombe na muda wa kumaliza kuuza pombe uwekwe wazi na sheria zisimamiwe.”

Pia anasema matukio ya ubakaji na ukatili yanapotokea viongozi wa dini wangekuwa wakishirikishwa.

"Tunaleana leana tu, viongozi wa dini wangekuwa wakishirikishwa haya yasingetokea mtu anakamatwa kwa ubakaji, mashahidi wapo ila mwisho wa siku anaachiwa lakini tungekuwa tunaitwa na kukaa kwenye vikoa na kuweka mikakati wabakaji wangefungwa,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpwayungu, Gabriel Hoya, anasema matatizo ya watoto yako mengi sio kwenye mimba tu hata suala la watoto kutumikishwa kwenye vilabu vya pombe ni suala  liangaliwe.

Pia anataka kuangaliwa suala la wazazi walevi ambao wamekuwa wakishinda na wakati mwingine kulala kwenye vilabu vya pombe na kushindwa kutimiza wajibu wao kenye malezi ya watoto.

“Mzazi anashinda kilabuni, wakati mwingine harudi nyumbani, watoto wanajilea wenyewe wanakwenda shule bila viatu, mavazi yamechanika, hawajala hili ni tatizo kubwa,” anasema.

Anasema jamii inatakiwa kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake ili kuweza kupunguza mimba za utotoni.
Ofisa Ustawi wa jamii katika wilaya ya Chamwino, Tegemea Ngulwa anawataka wazazi na walezi kuwa walinzi namba moja wa watoto wao ili waweze kujiepusha na ukatili na mimba za utotoni.

Ngulwa anasema kumekuwa na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wakati wazazi wana jukumu la kulinda watoto dhidi ya vitendo hivyo kwa kuwa karibu nao na kuwafuatilia na hata mtoto anapofanyiwa ukatili waripoti matukio hayo katika mamlaka husika.

Anasema kesi nyingi za ukatili zimekuwa zikikosa nguvu kutokana na baadhi ya wazazi kumalizana chini kwa chini na watuhumiwa bila kesi hizo kufika mamlaka husika.

Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Women Wake Up (WOWAP) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society linatekeleza mradi wa kutokomeza ukatili kwa kupunguza mimba na ndoa za utotoni.

Mratibu wa Shirika hilo, Nasra Suleiman anasema jambo la msingi ni kuona jamii inashiriki katika kulinda watoto kutokana na vitendo vingi vya ukatili vinafanyika ndani ya familia ikiwemo kulazimishwa kuwekewa njia za uzazi wa mpango.

Anasema watoto wengi hawakubali kwa hiari yao bali ni kwa matakwa ya wazazi.

“Mpwayungu na maeneo mengine wazazi wameamua kuwafunga vitanzi, vipandikizi watoto wao wa kike ili wasipate mimba wakiwa shuleni na sasa inaonekana kama jambo la kawaida,” anasema.

Anasema ni vyema serikali ikalisemea hili kwani limekithiri sana.

Pia anaitaka jamii kila mtu kwa nafasi yake aone anafanya nini katika kupunguza mimba na ndoa za utotoni kwani lengo kubwa ni kuona watoto wengi wanatimiza malengo yao.

Anasema wakiozwa au wakipata mimba katika umri mdogo wanashindwa kutumiza ndoto zao.

BAADA ya Dodoma kuwa rasmi Makao ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi