loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi akaribisha Diaspora kuipaisha Zanzibar

WAZANZIBARI wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) wametakiwa kulitangaza vizuri jina la Zanzibar kimataifa na wawe tayari kushirikiana na serikali kwa ajili ya kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo kwa faida ya wananchi.

Mgombea urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi alitoa wito huo jana Mji Mkongwe wakati akizungumza na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi.

Alisema akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar anakusudia kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa kushirikiana na Wazanzibari wote wakiwemo wanaoishi nje ya nchi ili kuyafikia matarajio ya wananchi.

“Nikichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar azma yangu pamoja na chama changu ni kuleta mageuzi makubwa kwa maslahi ya taifa, nipo tayari kufanya kazi na jamii ya Diaspora,'' alisema.

Dk Mwinyi aliwataka Diaspora ambao wapo tayari kurudi nyumbani wafanye hivyo haraka kwani taifa linahitaji watu wenye uwezo na ujuzi.

“Tunahitaji ujuzi na utaalamu wa wana Diaspora waliopo nje ya nchi kuja nchini na kutoa huduma mbalimbali, tunawakaribisha kwa mikono miwili,'' alisema.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji wataalamu kuwa ni sekta ya afya katika fani za kibingwa na utafiti wa mafuta na gesi na kwamba, Zanzibar ipo katika mchakato wa utafiti wa kazi hizo.

Alitoa mfano kuwa, Zanzibar inahitaji hospitali kubwa katika fani ya kutibu maradhi ya moyo kama ilivyo kwenye Taasisi ya Jakaya Kikwete Tanzania bara.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Ushirikiano na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchiAdila Hilali Vuai alisema lengo la diaspora ni kushirikiana na serikali kuleta maendeleo.

Alisema Wazanzibari wengi wanaoshi nje ya nchi katika nchi za Oman, Uingereza, Canada na Denmark ambao wote kwa nyakati tofauti wameonesha mashirikiano na serikali katika kuitikia wito wa kuja nyumbani na kusaidia maendeleo.

''Mheshimiwa mgombea katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Dk Ali Mohamed Shein mafanikio makubwa yamefikiwa kwa upande wa wenzetu Diaspora...wamekuwa karibu na sisi katika kushirikiano na kutoa misaada mbalimbali kwa wananchi wa Unguja na Pemba.''alisema Vuai.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi