loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Samia: Taasisi za fedha, sekta binafsi shirikianeni

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa taasisi za kifedha nchini, kushirikiana na wadau wa sekta binafsi ili kukuza mitaji yao na kuongeza ushindani wa kibiashara dhidi ya wenzao kutoka nje.

Samia alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwenye mkutano maalumu ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) jijini Dar es Salaam ili kumpongeza Rais John Magufuli kwa jitihada zake katika kuiboresha sekta  hiyo katika kipindi cha miaka mitano.

“Pamoja na ubora wa sera zinazoongoza sekta binafsi bado serikali tunaamini kwamba weledi kwenye utoaji wa huduma za kifedha nchini bado ni nguzo muhimu katika kufanikisha ustawi wa sekta ya binafsi. Niyaombe sana mabenki yetu tusaidiane kwenye hili,’’ alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Angelina Ngalula alimpongeza Rais Magufuli kwa uimara aliouonesha katika kipindi cha miaka mitano katika kuisaidia sekta hiyo. Pia, alizipongeza taasisi za fedha nchini kwa namna zinashirikiana na sekta binafsi katika kukuza mitaji ya wadau hao.

“Baadhi ya  taasisi hizi zimekuwa haziishii katika kutoa mikopo tu, bali pia zimekuwa zikitusaidia katika kufanikisha mikakati yetu ikiwemo mikutano muhimu inayolenga kujadili fursa na mipango muhimu kwa ustawi wetu,’’ alisema na kuzipongeza taasisi hizo ikiwemo Benki ya NBC ambayo ni moja ya wadhamini wakuu wa mkutano huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa  NBC, Theobald Sabi alisema benki hiyo imejipanga zaidi kushirikiana na sekta binafsi na serikali ili kusukuma maendeleo ya sekta hiyo. Aliweka wazi baadhi ya mikakati na huduma, ambazo benki hiyo inazitoa kwa wadau wa sekta binafsi.

Alisema ustawi wa sekta binafsi nchini, unategemea huduma bora za kifedha zinazoendana na mahitaji halisi ya wadau hao.

“Ndio maana benki ya NBC tumekuwa karibu sana na wadau wa sekta binafsi si tu katika kutoa huduma, bali pia kushirikiana nao katika kufanikisha mikakati yao mbalimbali, kwa kuwa tunaamini kupitia ushirikiano na ukaribu huu tunaweza kufahamu zaidi mahitaji yao hatua inayotuwezesha pia kubuni huduma zinazoenda sambamba na mahitaji yao,’’ alisema Sabi ambaye benki yake hiyo ilikuwa ni moja wa wadhamini wakuu wa mkutano huo.

Alitaja baadhi ya huduma na mikakati ya benki hiyo katika kuwasaidia wadau wa sekta binafsi kuwa ni uendeshaji wa kliniki za biashara kwa wafanyabiashara wakubwa na wa kati kupitia ushirikiano baina ya benki hiyo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na utoaji wa mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali.

“Pia tumekuwa karibu zaidi na wadau wa sekta ya kilimo kupitia huduma yetu ya ‘NBC Shambani’ ambapo tumetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wadau wa sekta hiyo. Pia tumekuwa tukitoa mikopo isiyo na dhamana kwa wazabuni wa makampuni makubwa nchini ili kuwasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kuwa na uwezo wa kifedha kuhudumia zabuni zao kwenye makampuni hayo,’’ alitaja.

Aliishukuru serikali kwa jitihada ilizoonesha katika kipindi cha miaka mitano hususani kwa kubuni sera ambazo zimeiwezesha sekta ya kibenki nchini kuwa imara zaidi licha ya changamoto za kiuchumi zilizotokana na athari za ugonjwa wa corona.

Hali hiyo imeziwezesha taasisi hizo kuendelea kutoa huduma kikamilifu bila kutetereka.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi