loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vijana na matumaini ya Dk Mwinyi kuongeza ajira

WAKATI mikutano ya kampeni za mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Ali Mwinyi zikiendelea tayari amefanikiwa kuyafikia makundi mbali mbali ya kijamii yapatao 50 ikiwemo vijana tangu alipozindua kampeni zake Unguja na Pemba mwezi uliopita.

Ni mgombea pekee wa nafasi ya urais wa Zanzibar aliyefanikiwa kuyafikia makundi muhimu ya kijamii na kusikiliza matatizo yao na changamoto zinazowakabili ili akichaguliwa kuongoza Zanzibar iwe rahisi kuzipatia ufumbuzi.

Baadhi ya makundi yaliyofikiwa na Dk Mwinyi hadi sasa ni pamoja vijana waendeshaji pikipiki maarufu bodaboda, wakulima wa mazao ya viungo, wakulima wa karafuu, vijana wasomi katika vyuo vikuu vya Zanzibar, viongozi wa dini mbalimbali, wajasiriamali, mama lishe pamoja na wanawake ikiwemo wajane.

Dk Mwinyi amebeba matumaini makubwa kwa kundi la vijana kutokana na ahadi zake baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la ajira.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Zanzibar, Mussa Haji Mussa, anasema sera ya uchumi wa bluu ni tegemeo kubwa ambalo linatarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wakiwemo wavuvi kwa kuyafikia maeneo ya bahari kuu.

Mussa akizungumza na gazeti hili baada ya vijana kukutana na mgombea huyo wa CCM anasema hadi sasa eneo la bahari kuu halijatumiwa kikamilifu na wavuvi wetu kwa kuvuna rasilimali zilizopo huko.

Anasema meli za kimataifa zilizosajiliwa kuvua maeneo hayo na kuingiza kipato kikubwa ndizo zimekuwa zikifika huko.

Anasema kwa mfano wakazi wa kijiji cha Chwaka na majirani zao wa Marumbi na Uroa hadi Pongwe kwa asilimia 60 ni wavuvi ambao ni vijana wanaohitaji kuwezeshwa kwa ajili ya kuvua katika maeneo ya bahari kuu pamoja na maji madogo huku wakitumia zana zenye kulinda mazingira ya baharini. 

“Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umejenga matumaini makubwa kwa mgombea wa chama cha Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ambaye ameahidi ajira zipatazo 300,000 katika utekelezaji wa ilani ya CCM na miongoni mwa hizo zitatokana na uchumi wa bluu,” anasema.

Anasema juhudi kama hizo tayari zimeanza kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo kununua meli moja kubwa ya Sehewa ambayo tayari imeanza majaribio ya kuvua katika eneo la bahari kuu.

Aidha analitaja eneo jingine ambalo halijatumiwa vizuri na vijana huku likiwa chanzo cha ajira kuwa ni sekta ya kilimo cha aina mbali mbali ikiwemo mboga mboga pamoja na kilimo cha viungo.

Mussa anasema sekta ya kilimo inayo nafasi kubwa katika kuzalisha ajira kwa vijana hasa kwa kuzingatia kwamba kuna eneo kubwa la ardhi linalofaa kuzalisha bidhaa mbali mbali za chakula.

Anasema kazi kubwa inayotakiwa ni kuwakusanya vijana na kuwapatia elimu na mbinu za kuingia katika kilimo cha biashara.

Kwa mfano, anasema UVCCM imefurahishwa na kazi kubwa iliyofanywa na mgombea huyo wa CCM wakati alipowatembelea wakulima wa zao la mwani ambalo hulimwa kwa asilimia 90 na wanawake.

Anasema mgombea ameahidi kuwakaribisha wawekezaji mbali mbali nchini kuwekeza viwanda vitakavyosarifu kilimo cha mwani kwa ajili ya kuongeza thamani zao hilo.

''Tunayo matumaini makubwa kwamba bei ya zao la mwani itaongezeka katika kipindi kifupi baada ya juhudi za ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani bidhaa zinazotokana na mwani,'' anasema.

Mkulima wa mwani katika kijiji cha Kiwengwa mkoa wa Kaskazini Unguja, Fatuma Jadi (35) alimweleza mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kupitia CCM kwamba wanahitaji viwanda vya kusarifu mazao ya kilimo ili waongeze thamani ya mwani.

''Sisi wanawake vijana tumejikita katika kulima zao la mwani lakini changamoto kubwa ipo kwenye bei ambapo tunahitaji viwanda ambavyo vitaongeza thamani ya mwani na sisi wakulima kupata bei kubwa,'' anasema.

Akitoa taarifa yenye matumaini kwa wakulima wa zao la mwani, Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali anasema tayari mipango imekamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kusarifu bidhaa zinazotokana na mwani huko Chamanangwe mkoa wa Kaskazini Pemba.

Anasema eneo la Chamangwe limetengwa kwa ajili ya kuwakaribisha wawekezaji mbali mbali kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo ambavyo vitaongeza thamani kwa wakulima na kupata bei nzuri.

Kwa mfano, anasema wakulima wanayo nafasi kubwa ya kuzalisha mazao ya viungo na kuwa sababu ya kujiajiri.

''Wizara ya Biashara na Viwanda tayari imeweka mazingira mazuri kwa mabaraza ya vijana kujikita katika kilimo cha mboga mboga na viungo ikiwemo pilipili hoho, kungo ambacho bei yake ni nzuri katika soko la dunia,''alisema.

Akizungumza katika kongamano la vijana wasomi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Dk Hussein Ali Mwinyi alisema akichaguliwa anakusudia kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki kwenye tarakimu moja huku akijipanga kuongeza makusanyo ya kodi kwa wastani Sh bilioni 800.0 kwa mwaka 2019 hadi kufikia Sh trilioni 1.55 mwaka 2025.

Anasema seta ya utalii imepewa kipaumbele kwa ajili ya kuzalisha ajira ambapo kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imelenga kuongeza idadi ya watalii kutoka 538,264 kwa mwaka huu 2020 hadi kufikia 850,000 mwaka 2025.

Kwa mfano anasema anakusudia kukitangaza zaidi kisiwa cha Pemba kutembelewa na watalii mbali mbali ambapo utalii endelevu utakaozingatia mazingira na utamaduni utapewa kipaumbele cha kwanza.

''Kisiwa cha Pemba hakijatangazwa zaidi kuwa moja ya kivutio cha watalii mbali mbali kutembelea kutokana na kuwa na fukwe nzuri na majengo ya kale ya makumbusho... Tunakusudia kuongeza idadi ya watalii kutoka 30,000 kwa mwaka 2018 hadi kufikia 150,000 kwa mwaka 2025,'' anasema.

Juma Saidi, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) ambaye alishiriki katika kongamano hilo na mgombea urais wa CCM anasema wamejenga matumaini makubwa kwa Dk Mwinyi kutokana na kauli zake na ahadi pamoja na tathmini za kisayansi za kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi ikiwemo ajira kwa kundi la vijana.

Anaitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kuhakikisha mitaala yake ya masomo ikiwemo ya kilimo inajikita zaidi katika kutoa ajira kwa vijana wakimaliza masomo yao.

''Tunahitaji masomo ya uvuvi wa bahari kuu pamoja na sekta ya kilimo ili wahitimu wanapomaliza masomo yao basi waweze kwenda moja kwa moja kujiajiri katika sekta hizo kwa sababu tayari wanayo elimu ya kutoka katika maeneo hayo,'' anasema.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akizungumza katika mkutano wa kampeni huko Chwaka anasema amefurahishwa na staili za kampeni zinazofanywa na mgombea urais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi za kushuka chini kwenda moja kwa moja kwa wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili ili akishinda aweze kuzifanyia kazi.

Dk Shein amekuwa akiwataka wananchi wa Zanzibar kumchagua Dk Mwinyi kwa sababu ameonesha sifa ya kiongozi anayetafuta uongozi wa nchi kwa kwenda moja kwa moja wanapoishi wananchi na kusikiliza changamoto zao.

''Nimefurahishwa na mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazofanywa na mgombea wetu wa CCM, Dk Hussein Ali Mwinyi ambaye amekuwa akishuka chini na kwenda moja kwa moja kwa wananchi hadi vijijini na kusikiliza kero zao… hakuna mgombea wa urais hata mmoja aliyefanya hivyo isipokuwa yeye,''alisema.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi