loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Majaliwa awataka Mtwara kumpa kura JPM

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wana Mtwara wawe makini kuamua wanataka kiongozi wa aina gani kwani zimebakia siku sita tu kabla ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania.

Majaliwa ambaye yuko mkoani Mtwara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Newala Vijijini, Maimuna Mtanda na mgombea udiwani wa Kata ya Kitangari, Mfaume Ladda.

Alisema wananchi wanapaswa kuamua aina ya kiongozi wa kumchagua ili alete maendeleo ya haraka. “Maendeleo hayana chama sababu tukijenga shule watasoma watoto wetu wote. Kwa hiyo, nawaomba tumchague Dk Magufuli ili aje aendeleze mazuri aliyoyaanzisha,” alieleza.

Kuhusu uboreshwaji wa miundombinu, Majaliwa alisema upanuzi wa bandari ya Mtwara unaendelea ambako Sh bilioni 170 zilitolewa na serikali ili ujenzi wa kitako kikubwa cha kuweka mizigo na magari zaidi ya 600 ufanyike.

“Vile vile Sh bilioni 50 zimetolewa kwa ajili ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara ili uweze kupokea moja kwa moja ndege kubwa kutoka Ulaya bila kulazimika kutua kwanza Dar es Salaam,” alisema Majaliwa.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami, Majaliwa alisema serikali ilitoa Sh bilioni 89 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 210 ambayo itaunganisha wilaya nne na itaanzia Mtwara Vijijini - Nanyamba - Newala - Masasi.

Kuhusu zao la korosho, alisema mfumo wa mnada ulisaidia bei ya korosho ipande na kufikia Sh 4,000 lakini msimu uliopita bei ilizorota kwa sababu ya ugonjwa wa covi 19.

Majaliwa ambaye awali alisimamishwa na wananchi wa Kata ya Mkwiti, alisema serikali imetoa Sh milioni 600 kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Mtama hadi Tandahimba kupitia Mkwiti ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Mtama hadi Tandahimba kutasaidia kuboresha biashara na usafiri baina ya maeneo hayo na Jiji la Dar es Salaam,” alieleza.

Pia alimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk Magufuli na kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Tandahimba kwa tiketi ya CCM, Katani Ahmad Katani na mgombea udiwani wa Kata ya Mkwiti, Ismail Said.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Newala

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi