loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Mchungaji: Chagueni wenye hofu ya Mungu

ZIKIWA zimebakia siku sita kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Rais, madiwani na wabunge, Watanzania wametakiwa kuchagua viongozi bora na wenye hofu na Mungu ambao watatatua changamoto mbalimbali za nchi na kuzidi kuimarisha amani na kuimarisha uchumi wa nchini.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mchungaji Kennedy Aseno Wangusu wa Kanisa la Wasabato Kitete lilipo katika Manispaa ya Tabora alipokuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake.

Alisema kuwa waumini wa kanisa hilo wameanza maombi ya kufunga ambayo yanafanyika kila siku ya Jumatano na Ijumaa ili kuliombea taifa lipate viongozi bora ambao watajali maslahi ya taifa na kufanya taifa lizidi kusonga mbele kimaendeleo na kudumisha amani.

"Watanzania tunapaswa kuwa makini na hawa wanasiasa wanaoomba ridhaa ya kuongoza nchi pasipo kuwa na hofu ya Mungu, sikilizeni sera zao ili mfanye uchaguzi sahihi tarehe 28 Oktoba mwaka huu ili tupate wale watakaolinda amani yetu na wenye hofu na Mungu," alisema.

Aliwataka wanasiasa kuacha kutumia lugha chonganishi na za ubaguzi wa makabila katika majukwaa ya kisiasa badala yake waeleze hoja za msingi zitakazosaidia nchi.

"Unaposikia mataifa mengine kwenye machafuko mara nyingi zinasababishwa na wanasiasa ambao wanafanya siasa za kujenga nchi na badala yake wanafanya nchi kutaka kuingia kwenye machafuko,"alisema.

Alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa amani inahusu makundi yote na inapopotea ni gharama kubwa kuirudisha, hivyo ni vyema kuitunza.

Alisema kuelekea Uchaguzi Mkuu  mwaka huu, kanisa limekuwa likitoa elimu ya mpigakura kwa watu wote, ikiwemo wenye mahitaji maalumu ili kutambua umuhimu wa kupiga kura, na kuchagua viongozi wanaowaona wanaweza kuwaongoza na kuwatetea kupata haki zao za msingi.

Mzee wa kanisa hilo, Dk Felix Kasika aliwaasa vijana kutojihusisha katika vurugu zozote katika kipindi hiki cha kampeni na hata siku ya kupiga kura na hata wakishawishiwa aliwataka kutokubaliana na wanasiasa wa namna hiyo.

“Mungu ni mwema kwa kila mtu na mwenza kwa kila kitu kwani yeye ndiye aliyeumba wanadamu wote, tujitahidi kumlilia Mungu ili kupata viongozi bora na wenye kumcha Muumba ili wawe suluhisho kwa changamoto za Watanzania wote kwani wakati wa kubaguana haupo, sasa ni muda kuchagua viongozi wa kutuletea maendeleo.

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi