loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakulima wa Kisarawe wafunzwa elimu ya korosho

WAKULIMA wa zao la korosho na maofisa ugani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, wamepatiwa elimu mbalimbali kwa vitendo kwenye zao hilo, ikiwemo elimu ya maua ya mkorosho inayozalisha korosho.

Katika mafunzo hayo, pia imetolewa elimu juu ya mchakato mzima wa kilimo hicho cha korosho kama vile hatua ya kuanza kuandaa shamba, upandaji, mbegu bora, upuliziaji na matumizi sahihi ya viuatilifu, aina ambalimbali za wadudu wanaoathiri mikorosho.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyohusu kilimo bora cha zao la korosho na ubora wake, yalifanyika mjini Kisarawe. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo hapa nchini (TARI) Naliendele.

Akitoa elimu hiyo katika shamba lililopo eneo la Sanze Kazimzumbwi wilayani humo, mtaalamu kutoka TARI Naliendele, Stella Mfune alisema kuna aina tatu za maua ya korosho ikiwemo ua tasa, dume na jike.

Alisema kati ya hayo, ua linalotakiwa ni dume na jike. Ua hilo lina mchanganyiko wa maua mawili ikiwemo dume na jike ndiyo yanayoweza kuzaa. Ua jike likishapata mbegu za kiume lina uwezo wa kuzaa, lakini kwenye mti likiwa dume pekee wadudu au upepo watachukua mbegu na kuja kuliweka au kuchangisha kwenye ua jike ndipo korosho inaweza kuzaa.

Mti ukiwa na maua dume mengi, unakuwa haufai kwa sababu hautazalisha korosho. Kwa kawaida siku tatu mpaka nne maua yanakuwa tayari yameshakauka, yakiwa ni dume na jike. Siku ya kwanza ndiyo muhimu kwani mti unakuwa tayari umeshapata chamvua na kuweka korosho. Una uwezo wa kupokea mbegu dume kuanzia siku ya kwanza hadi siku ya pili.

Elimu hiyo ya maua kwa mkulima ni muhimu, kwani  itasaidia kujua mkorosho bora na ule usio bora. Mikorosho mingine inatangulia kutoa madume pekee na baadaye yanakuja kutoa majike. Lakini, pia kuna mkorosho mwingine kila unapotoa maua, huwa unatoa madume tu, kwa hiyo mkorosho huo haufai na mingine hutoa madume na majike na ndio unaofaa.

Mdhibiti Ubora wa Korosho kutoka Bodi ya Korosho nchini (CBT) Tawi la Dar es Salaam, Joseph Merere alisema matarajio yao ni kuona baada ya mafunzo hayo, zao hilo linafikia malengo yanayotarajiwa. Alisema korosho inaweza bora endapo watafuata maelezo ya wataalamu hao.

“Maofisa ugani muwe karibu sana na wakulima na mhakikishe mnawafikia mahali popote walipo. Pia vyama vya msingi vihakikishe wakulima wanapopeleka korosho ghalani watunze korosho kama inavyotakiwa na lengo la uzalishaji ni kufikia tani milioni moja ifikapo 2025,”alisema Merere.

Baadhi ya wakulima, akiwemo Saidi Abdallah,  wakiwa shambani hapo walisema kuwa baada ya mafunzo hayo, wataondokana na kilimo cha awali kwani kuna vitu walikuwa hawavifahamu ikiwemo elimu hiyo ya maua. Walisema sasa watajua aina ya maua yanayofaa kuzalisha korosho.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imeweza ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Kisarawe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi