loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi aahidi makubwa Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Ali Mwinyi amewaomba wananchi wa kisiwa cha Pemba kumpa kura nyingi za ndiyo awatumikie wananchi wake kwa sababu tayari anazifahamu changamoto zote zinazowakabili kwa sasa.

Dk Mwinyi ambaye ameahidi kufanya mambo  makubwa kisiwani Pemba na Zanzibar kwa jumla, alishukuru na kupongeza mapokezi makubwa aliyopata katika mikutano ya hadhara, akisema dalili za ushindi ameziona mapema.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni katika uwanja wa Gombani ya Kale huko Chake Chake Pemba, alisema amefanya mikutano ya hadhara 15 na mikutano ya ndani 60.

Pia alisema amekutana na makundi mbali mbali na kusikiliza changamoto zao, ambapo alisema amezisikia na yupo tayari kuzifanyia kazi.

''Wananchi wa Pemba nawaombeni nipeni kura nyingi za ndiyo ambazo zitaniwezesha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na dalili ya ushindi nimeziona mapema sana,''alisema.

Alisema kitendo cha mapokezi makubwa ya shangwe katika kisiwa hicho, kimempa ari kubwa na moyo wa kuwa tayari kuwatumikia wananchi endapo watampa ridhaa ya kuwa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Alisema, ''Wananchi wa kisiwa cha Pemba sasa nipo tayari kuwatumikia kwa sababu nazifahamu changamoto zote zinazowakabili ikiwamo za vijana...naomba kura zenu ifikapo Oktoba 28 mwaka huu ili nitimize matakwa yenu''alisema.

Alisema akichaguliwa anatarajia kujenga upya uchumi wa Zanzibar ambao ni wa buluu, kwa kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu, kuwafanya wavuvi kuvua katika maeneo yenye kipato kikubwa.

Dk Mwinyi alisema wavuvi wa Kisiwa cha Pemba, watawezeshwa kwa kupewa zana za uvuvi zitakazowawezesha kuvua samaki wengi na kupata kipato kikubwa na kufikia hatua ya sekta hiyo kuchangia pato la taifa.

''Tunataka kujenga uchumi wa kisasa wa buluu ambao utawawezesha wavuvi kuvua katika eneo lenye kina kikubwa cha maji pamoja na wavuvi wa kawaida kuwezeshwa kwa kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu sana,''alisema.

Kuhusu wastaafu na wazee, alisema akichaguliwa anakusudia kuongeza kiwango cha pensheni jamii kadri hali ya kifedha itakapokuwa nzuri.

''Naitambua pensheni jamii wanayopatiwa wazee ya  shilingi 20,000 kwa mwezi...nikifanikiwa kuingia madarakani nitaongeza pensheni hiyo kadri hali ya fedha itakapokuwa nzuri''alisema.  

Awali, Mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan aliwataka wananchi wa Pemba wamchague  Dk Hussein ambaye ndiye mwenye uwezo wa kufanya kazi na Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli.

Alisema wagombea wa CCM katika nafasi hizo, ndio wenye uwezo wa kulinda Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,  ambao umeasisiwa na viongozi wakuu.

Samia ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema wapinzani hawautambui Muungano wala Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo wamekuwa wakiyabeza huku wengine wakiwa na ndoto ya kuwa na muungano wa serikali tatu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Sadala alisema ameridhishwa na maandalizi ya mikutano ya hadhara katika kisiwa cha Pemba. Alieleza kwamba sasa wananchi wapo tayari kukiunga mkono CCM kwa dhati.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imeweza ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Chake Chake

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi