loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Mtangazaji TBC, Elisha Elia azikwa Tukuyu

MAZIKO ya aliyekuwa Mwandishi na Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Elisha Elia (39) yalifanyika jana katika makaburi ya Kijiji cha Mano Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Ibada ya kumuaga Elisha ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mano ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema alipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Elisha na kutoa pole kwa wanafamilia, uongozi wa TBC na wadau wote wa tasnia ya habari. 

Alisema kifo cha Elisha ni pigo kwa TBC na tasnia nzima ya habari kwa kuondokewa na mmoja wa wanahabari makini, mwaadilifu, mzoefu mchapakazi na mwenye mchango mkubwa katika kuhabarisha na kuelimisha umma.

“Hili ni pigo kwa TBC na tasnia nzima ya habari kwa kuondokewa na mmoja wa mwanahabari makini, mwadilifu, mzoefu na mchapakazi mwenye mchango mkubwa katika kuhabarisha na kuelimisha umma,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema Elisha atakumbukwa kwa kipaji chake adhimu cha utangazaji na uandaaji wa vipindi ikiwemo kipindi maalumu kilichokuwa kinazungumzia utekelezaji wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kilichojulikana kama ‘Hiki ni kishindo cha Awamu ya Tano.’

Katika uhai, Elisha alipata tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya kuimarisha diplomasia ya uchumi wa nchi ambayo ilitolewa Desemba, 2019 na Shirika lisilo la Kiserikali la Kuinua Diplomasia ya Uchumi Tanzania (TEDEF).

Elisha (39) alifariki dunia Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam wakati akiwa anapatiwa matibabu.

foto
Mwandishi: Dativa Minja

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi