loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Simba, Azam zabeba wapinzani

MZUNGUKO wa nane wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulikuwa wenye ushindani mkubwa na mgumu kwa vigogo Simba, Azam waliopoteza michezo yao, furaha ikihamia kwa wapinzani wao waliong’ara na kupanda nafasi za juu.

Simba ilipoteza dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0 sawa na Azam FC iliyopoteza kwa mara ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar kwa kipingo kama hicho.

Licha ya kupoteza kila mmoja anaendelea kubaki kwenye nafasi yake, Azam ikiwa kinara kwa pointi 21 na Simba nafasi ya nne kwa pointi 13.

Kupoteza kwao kumewapa faida Mtibwa Sugar iliyokuwa nafasi ya 14 kwa pointi nane kupanda hadi nafasi ya 10 kwa pointi 11 na Ruvu Shooting iliyokuwa nafasi ya 10 kwa pointi tisa kupanda hadi nafasi ya saba kwa pointi 12.

Kupoteza kwa vigogo hao kunazidi kuwapa presha katika harakati za kuwania taji, bingwa mtetezi Simba ni mechi ya pili inafanya vibaya huku Azam FC ikiingia kwenye hofu ya kushushwa katika nafasi ya kwanza iwapo itashindwa kwenye mechi zake zijazo pengine wanaweza kushuka kidogo kutoka nafasi waliyopo.

Kwa upande wa Yanga licha ya kushinda  mchezo uliopita dhidi ya KMC kwa mabao 2-1 bado imeendelea kusalia nafasi ya pili ingawa pointi zimeongezeka hadi kufika 19.

Mpaka sasa unaweza kusema Yanga ndio timu pekee yenye ukuta imara baada ya kufungwa mabao mawili na kufunga mabao 10, ikifuatiwa na Azam iliyoruhusu kufungwa mabao matatu ikifuatiwa na Simba iliyofungwa mabao manne.

Timu zilizoweka rekodi ya ajabu ni JKT Tanzania iliyoshinda mabao 6-1 katika mchezo mmoja uliopita dhidi ya Mwadui FC. 

Ushindi huo ni mkubwa tangu kuanza kwa msimu huu na uliifanya timu hiyo kupanda nafasi moja juu kutoka 16 hadi 15.

Mbeya City iliweka rekodi baada ya kushinda mchezo wa kwanza katika mzunguko huu tena ikiwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 2-1.

Ushindi huo uliifanya timu hiyo iliyokuwa ikishika mkia kupanda nafasi moja juu kutoka 18 hadi 17. 

Timu nyingine iliyopanda ni Tanzania Prisons iliyoshinda mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji bao 1-0 na kupanda kutoka nafasi ya tisa hadi ya tano wakifikisha pointi 12.

Walioshuka kidogo ni Kagera Sugar kutoka nafasi ya 15 hadi 16 baada ya kupoteza dhidi ya Mbeya City, Namungo kutoka nafasi ya nane hadi ya 11 baada ya kupata sare dhidi ya Ihefu 0-0, Polisi Tanzania kutoka nafasi ya saba hadi ya tisa baada ya kupoteza dhidi ya Biashara kwa bao 1-0.

Wengine ni Mwadui FC kutoka nafasi ya 12 hadi 14, KMC kutoka ya sita hadi ya nane, Dodoma Jiji kutoka ya tano hadi sita, Gwambina kutoka nafasi ya 11 hadi 12 huku Coastal ikiendelea kusalia nafasi ya 13.

MSANII mkongwe nchini Saidi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi