loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

RC: Utulivu watawala Mtwara, wengi wajitokeza kupiga kura

HALI ya usalama na utulivu vimeendelea kutawala huku wananchi wengi wakiwemo wazee, vijana na wamama wakijitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo mbalimbali mkoani  Mtwara.
 
Akiongea na wanahabari mara baada kupiga kura katika kituo cha 'Government Rest House' Mtaa wa Shangani Jimbo la Mtwara Mjini, Mkuu wa Mkoa Gelasius Byakanwa amesema kwa Mkoa mzima hali ya vituo vyote iko katika usalama na utulivu na kwamba wananchi wamejitokeza kwa wingi sana kupiga kura.
 
Amesema wananchi wanapiga kura na kuondoka kwenda majumbani kwao na kuendelea na shughuli nyingine huku wakisubiria matokea ya kura walizopiga
 
"Kama mnavyoona hali ya upigaji kura ni ya utulivu mkubwa sana, mnafika kituoni mnapewa maelekezo alafu unafuata taratibu zote mpaka unamaliza kupiga kura," amesema.
 
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuwa watulivu huku wakifuate utaratibu na  kumalize kupiga kura warudi majumbani na kusubiria matokeo.
 
"Ni Imani yangu kwamba tumeanza katika hali ya utulivu na tutamaliza katika hali ya utulivu, na hii ndio hulka ya watanzania huu ndio utanzania wetu kwa maana ya kwamba tunafuata utaratibu na hatutaki vurugu katika maeneo ya kupigia kura," amesema 
 
"Na niendelee kuomba hali hii ya utulivu idumu hadi mwisho wa uchaguzi na tukubali matokeo yatakapokuwa yametangazwa," amesema.
 
Katika uchunguzi uliofanywa na Mwaandishi wa Habari hizi katika vituo mbalimbali vya kupigia kura Jimbo la Mtwara Mjini na Vijijini mkoani hapa, hali ilikuwa ya utulivu huku wananchi wakijitokeza kupiga kura na kuondoka kwa utulivu.
 
Katika vituo vya  Magomeni na Mbezi matopeni wananchi wakijitokeza kwa wingi na wengi wao kuzungumziwa hali ya usalama na kukiri kuwa ni ya utulivu sana tofuauti na chaguzi zilizopita.
 
Hidaya Ibrahim mkazi wa Magomeni Matopeni ameshukuru kwa kuwepo hali ya utulivu ambayo inachangia na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.
 
"Zoezi la kupiga kura liko vizuri halina matatio yoyote nimeshapiga kura na sasa narudi nyumbani sijaona hali ya sintofahamu, hali ya usalama ni kubwa na amani pia imetawala," amesema huku akitoa wito kwa akina mama na vijana majumbani kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
 
Akizungumzia zoezi la upigaji kura Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mtwara Mjini Kanali Emmanuel Mwaigobeko alisema vituo vyote vya kupigia kura vilifunguliwa kuanzia sa moja na wananchi kuanza kujitokeza kupiga kura na kwamba hakuna tatizo lolote ambalo limetokea.
foto
Mwandishi: ANNE ROBI Mtwara

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi