loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wadau waombwa kupunguza bei vyakula vya mifugo

KATIBU  Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo), Profesa  Elisante ole Gabriel, amewataka  wenye viwanda vya uzalishaji  vyakula vya mifugo kutoa unafuu kwa watumiaji wa bidhaa zao.

Alisema  bila kuathiri gharama za uendeshaji wenye viwanda hivyo wana wajibu wa kuwawezesha wafugaji kutumia  kwa wingi vyakula  bora kwa mifugo yao.

Profesa Ole Gabriel alisema hayo hivi karibuni  mjini Morogoro  wakati akifunga mafunzo kwa wakaguzi wa chakula cha mifugo kutoka  kanda ya mashariki inayoshirikisha  mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Pwani na Dodoma.

Katibu mkuu huyo, alisema gharama za vyakula vya mifugo ipo juu hasa vyakula vya kuku, hivyo  ni vyema, Idara ya uendelezaji wa malisho na vyakula vya mifugo kufanya tathmini ya hali halisi ya utengenezaji wa vyakula vya mifugo.

"Nashauri wazalishaji wa vyakula vya mifugo wakae meza moja na walaji ili kuangalia mnyororo wa gharama zao na kuleta unafuu kwa walaji," alisema Profesa  Ole Gabriel.

 

Hata hivyo, alizitaka taasisi  na viwanda  vyote vinavyozalisha chakula cha mifugo hapa nchini kufanya utafiti wa kina wa malighafi zinazotumika kwenye kuchakata chakula  hivyo ili kuona kuwa zinakidhi vigezo vya kutumika kwa  chakula cha mifugo.

Naye  Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Malisho na Vyakula vya Mifugo, Dk Asimwe Rwiguza, alisema tabia ya kutumia  nafaka ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu kutengeneza lishe ya mifugo ikome kwani bidhaa hizo zinapoliwa na wanyama zinaleta madhara pia kwa binadamu. 

Dk  Rwiguza, alisema kuwa wanyama wanapokula vyakula hivyo vyenye kiwango kikubwa cha sumukuvu  inaingia kwenye mazao yatokanayo na mifugo kama maziwa na nyama  na baadaye maziwa nayo yanatumika  na binadamu kwa kunywa  na ulaji wa  nyama.

Pamoja na kutoa rai kwa wafugaji, Dk  Rwiguza pia aliwataka  wakaguzi wa chakula cha mifugo waliopata mafunzo hayo kwenda kutoa elimu kwa wafugaji namna bora ya kufuga kwa kuzingatia ufugaji wa kisasa.

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi