loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Msalala wapongezwa kutenga bajeti kukabili utapiamlo

HALMASHAURI  ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga  imepongezwa  kwa kutenga bajeti   ya mapato yao ya ndani ya kiasi cha  shilingi milioni 32 kwa ajili ya kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango kwa lengo la kuokoa vifo vya wajawazito na watoto.

Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya uzazi wa mpango imeongezeka kutoka Sh milioni 3.6 mwaka 2018/19 na kufikia milioni 4.9  katika bajeti ya  2019/20 na hatimaye kufikia Sh  milioni 32 kwa mwaka huu wa fedha 2021.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk Ntanwa Kilagwile alisema hayo wakati wa kikao cha kufungwa kwa mradi wa  Health System Advocacy  uliokuwa umefadhiliwa na shirika la Amref Health Afrika.

Dk Kilagwale alisema kuwa  pongezi hizo zimetoka shirika la Amref kwa jitihada zao za kuhamasisha  kutenga bajeti,  lakini walijitahidi kuongeza  kwa ajili ya kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango na kuweza kuokoa vifo vya wajawazito na watoto,  hilo nalo waliliona na kuamua kulifanyia kazi.

Mkurugenzi kutoka shirika la Amref, Florence Temu  alisema kuwa jamii bado haina uelewa kuhusiana na elimu juu ya uzazi wa mpango ndio maana wao walihamasisha halmashauri kuongeza bajeti na kutoa elimu ili kuweza kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Daktari  bingwa wa watoto,  Mwita  Ngutunyi  kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga alisema kuna makosa mengi yamefanywa katika kupangilia uzazi na kusababisha watoto waliozaliwa kwa kufuatana kupata tatizo la utapiamlo.

"Upo utapiamlo wa kadiri, kwa  mkoa huu  nimekutana na watoto ambao wameachishwa kunyonya maziwa ya mama chini ya mwaka mmoja kwa  sababu ya mama huyo kuwa mjamzito  hali ambayo imeathiri makuzi ya mtoto kwani maziwa ya mama yana virutubisho vyote akiendelea kumyonyesha hayana madhara yoyote," alisema Dk Ngutunyi.

Muuguzi kutoka  halmashauri ya  Msalala, Monica Giliya  alisema tatizo la kutofuata uzazi wa mpango limekuwa changamoto lakini elimu imeendelea kutolewa kwa kila mama anayehudhuria kliniki  na mafanikio yameanza kuonekana. 

Aidha  mkazi wa kijiji cha Segese halmashauri ya Msalala, Johari Shija  mwenye watoto wanane na Maria Onesmo mwenye watoto watano walisema kwa wakati tofauti kuwa wanaogopa kutumia uzazi wa mpango kwa madai kuwa utawazidishia magonjwa na kushindwa kufanya kazi.

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Kahama

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi