loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

‘Mafuriko’CCM yawaacha hoi wapinzani

MATOKEO ya Uchaguzi Mkuu kwa ngazi ya ubunge na udiwani yaliyoanza kutangazwa juzi usiku baada ya kumalizika kwa upigaji kura na yanayoendelea kutangazwa kote nchini, yameipa ushindi wa mafuriko wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuwaacha wapinzani wakiwa hoi.

 

Katika Bunge la 11, CCM ilikuwa na viti vya ubunge 186 kati ya viti 264 wakati vyama vya upinzani vyote kwa ujumla vilikuwa na viti 115, kati yake Chadema 70 na Chama cha Wananchi (CUF) 45.

 

Jumla ya viti vya bungeni vinavyotokana na majimbo ni 264, Viti Maalumu 113, wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi watano, Mwanasheria Mkuu na viti 10 vya Rais na jumla ni wabunge 393.

 

Lakini matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, yanaonesha kuna dalili za wapinzani kushindwa kufikia hata robo ya viti vyao hivyo kutokana na jinsi wagombea wa CCM walivyong’ara.

 

Wachambuzi wa masuala ya siasa walitabiri anguko na ushindi mkubwa kwa wagombea wa CCM kutokana na Serikali ya Rais John Magufuli kutekeleza kwa mafanikio makubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020, kiasi baadhi ya wapinzani waliokuwa madarakani, waliachia nafasi zao na kujiunga na CCM hata kabla ya kumaliza miaka mitano.

 

Katika uchaguzi huo, majina ya vigogo wakiwamo mawaziri na naibu mawaziri, wateule wa Rais katika nafasi za ubunge na nafasi mbali mbali za utendaji waliokuwa wakigombea, wengi wameshinda kwa kishindo.

 

Hadi jana jioni takribani majimbo 15 yaliyokuwa yakishikiliwa na upinzani, sasa yamechukuliwa na CCM. Hali hiyo inaashiria kuwa sasa chama hicho tawala kitakuwa na viti vingi bungeni kuliko ilivyopata mwaka 2015.

 

Oddo Ummy azoa 94%

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangazwa kupata ushindi wa asilimia 94 katika Jimbo la Tanga Mjini baada ya kupata kura 114,445 dhidi ya mpinzani wake, mbunge aliyemaliza muda wake, Mussa Mbarouk wa CUF aliyepata kura 7,497 sawa na asilimia sita.

 

Jimbo la Handeni Mjini mkoani Tanga, Reuben Kwagilwa (CCM) ameibuka mshindi kwa kupata kura 15,241, akifuatiwa na Sonia Magogo wa CUF aliyepata kura 6,713. Sonia alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

 

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Lushoto alimtangaza Shaaban Shekilindi wa CCM kuwa mshindi kwa kura 20,799 dhidi ya Gelmano Mbelwa wa Chadema kura 4,086 huku Ismail Mshangama akipata kura 3,246.

 

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Korogwe Mji alimtangaza Dk Alfred Kimei wa CCM kuwa mshindi akipata kura 16,969 dhidi ya Winjones Clarence wa Chadema kura 2,116 huku Amina Magogo wa CUF akipata kura 1,497.

 

Rashid Shangazi wa CCM alitangazwa mshindi Jimbo la Mlalo kwa kura 46,632 dhidi ya wapinzani wake Amir Mohamed wa Chadema kura 2,803 na mgombea wa ACT Wazalendo, Laurent Mkai kura 1,671.

 

Tulia, Msambatavangu  

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliibuka na ushindi wa kura 75,225 katika Jimbo la Mbeya Mjini dhidi ya mpinzani wake Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliyepoteza jimbo hilo aliloingoza kwa miaka 10 baada ya kupata kura 37,591.

 

Mwanamama mwingine, Jesca Msambatavangu amemaliza utawala wa miaka 10 wa Peter Msigwa katika Jimbo la Iringa Mjini, baada ya kutangazwa mshindi kwa kura 36,034 dhidi ya kura 19,331. Msambatavangu amewahi kuwa Mweyekiti wa CCM wa mkoa huo.

 

Mawaziri washinda

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano (Mazingira), Mussa Sima alishinda Jimbo la Singida Mjini kwa kupata kura 23,220 wakati Rehema Mkoha aliyegombea kwa tiketi ya Chadema amepata kura 15,467.

 

Jimbo la Iramba Magharibi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba alishinda kwa kura 38,675 dhidi ya Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa (Chadema) mwenye kura 6,520; kwa mujibu wa msimamizi, Lino Mwageni.

 

Katika Jimbo la Ilala, msimamizi Jumanne Shauri alimtangaza Waziri wa Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu kuwa mshindi kwa kura 26,499 sawa na asilimia 74.07 akifuafiwa na Juma Isaak wa Chadema kura 6,534 asilimia 18.26 na Mwinshehe Mwinzangu maarufu Kingwendu wa CUF kura 466. Zungu amewashinda wagombea 13.

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde ameshinda Dodoma Mjini kwa kupata kura 86,565 (86.44%) na kumbwaga Aisha Madoga wa Chadema kura 13,586 (13.56%).

 

Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile ametetea kiti chake cha ubunge kwa kupata ushindi wa kura 34,540 dhidi ya mpinzani wake, Mageleli Simon (Chadema) aliyepata kura 11,306 akifuatiwa na Mwanaisha Mndeme (ACT-Wazalendo) aliyepata kura 1,952.

 

Singida Kaskazini mshindi ni Ramadan Ighondo (CCM) kura 43,847 wakati aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo na waziri kwa miaka mingi kabla ya kuhamia Chadema, Lazaro Nyalandu aliambulia kura 15,555.

 

Manyoni Mashariki Dk Pius Chaya (CCM) ameshinda kwa kura 36,284 dhidi ya Aisha Luja (Chadema) kura 4,773 wakati Manyoni Magharibi mshindi ni Yahya Massare (CCM) kura 16,961 dhidi ya Jumanne Sunta (Chadema) kura 7,529.

 

 

Ng’enda ang’ara Kigoma

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) amepoteza jimbo hilo baada ya kuangushwa na Kirumbe Ng’enda (CCM) aliyepata kura 27,638, Zitto kura 20,600 na Francis Mangu (Chadema) aliyepata kura 1,227.

 

Jimbo la Muhambwe, CCM imeshinda kupitia Atashasta Nditiye aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano aliyepata kura 29,837 dhidi ya Felix Mkosamali (Chadema) aliyepata kura 15,249.

 

Jimbo la Buhigwe, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango (CCM) alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 43,481 dhidi ya Lukulazo Pastory wa Chadema kura 13,775 na Ibrahim Sendwe (ACT Wazalendo) kura 13,007.

 

Jumanne Kishimba ameibuka na ushindi katika Jimbo la Kahama Mji mkoani Shinyanga kwa kupata kura 35,709 akifuatiwa na Joachim Assecheka Mwati (Chadema) aliyepata kura 10,740 na Swalehe Mapande (ACT Wazalendo) amepata kura 1,094.

 

Aeshi Hilaly ametetea kiti chake katika Jimbo la Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa baada ya kushinda kwa kura 36,807 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Shadrack Malila aliyepata kura 17,829.

 

Kwa upande wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mkoa wa Ruvuma, Hassan Kungu (CCM) ameibuka mshindi kwa kupata kura 30,056 baada ya kumbwaga mpinzani wake, Ado Shaibu (ACT Wazalendo) aliyepata kura 18,300.

 

Jimbo la Longido, Dk Steven Kiruswa ametetea kiti chake kwa kura 61,885 akimbwaga Pauline Laizer wa Chadema aliyepata kura 1,037 akifuatiwa na Feruz Juma (NRA) aliyepata kura 21.

 

Fred Lowassa aliyewania Jimbo la Monduli kwa tiketi ya CCM ameshinda kwa kura 72,502 sawa na asilimia 93 dhidi ya Cesilia Ndosi wa Chadema kwa kura 4,637 asilimia 5.96.

 

Tarimo aibeba Moshi Mjini

Katika Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo wa CCM amepata kura 31,169 na kumshinda Raymond Mboya wa Chadema aliyepata kura 22,555. Kwa miaka 25 jimbo hilo limekuwa chini ya uongozi wa upinzani hasa Chadema.

 

Katika Jimbo la Rombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara mbalimbali, Profesa Adolf Mkenda ameshinda kwa kura 48,122 na kumshinda Patrick Asenga wa Chadema aliyepata kura 9,519, huku Dk Godwin Mollel akitetea kiti chake Jimbo la Siha kwa kura 22,176, na kumshinda Elvis Mosi wa Chadema aliyepata kura 8,614.

 

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi ametangazwa mshindi Jimbo la Shinyanga Mjini kwa kupata kura 31,831 asilimia 63 akimshinda aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba (Chadema) aliyepata kura 16,608.

 

Katika Jimbo la Mbarali, Francis Mtega (CCM) amepata ushindi wa kura 55,737 akifuatiwa na Liberatus Mwang’ombe (Chadema) 28,104 na Juma Hanji wa ACT Wazalendo aliyepata kura 1,256.

 

Mtwara Mjini, Hasan Seleman (CCM) alipata kura 22,411, akifuatiwa na Abdallah Nachuma (CUF) aliyepata kura 13,586 na Hassani Abdallah (ACT - Wazalendo) aliyepata kura 1,113.

 

Bahi, Kondoa

Katika Jimbo la Bahi Mkoa wa Dodoma, Msimamizi wa uchaguzi, Dk Fatma Mganga alimtangaza Kenneth Nolo (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 40,629 akifuatiwa na mgombea wa CUF, Geodfrey Pamwe  kura 2,254.

 

Jimbo la Kondoa Mjini, Ally Makoa (CCM) ameshinda kwa kura 15,220 huku mpinzani wake Salehe Kizota wa Chadema akipata kura 1,862. Kondoa Mjini lilikuwa linashikiliwa na Edwin Sanda aliyeshindwa kura za maoni

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama Mji mkoani Shinyanga, Anderson Msumba alimtangaza Jumanne Kishimba (CCM) kuwa mshindi wa ubunge baada ya kupata kura 35,709 akifuatiwa na Joachim Mwati (Chadema) aliyepata kura 10,740 na Swalehe Mapande (ACT-Wazalendo) alipata kura 1,094.

 

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbinga Mjini, Grace Quintine alimtangaza Menas Mbunda (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 26,698 dhidi ya mgombea wa Chadema, Ephraim Millinga aliyeambulia kura 5243.

 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amechaguliwa tena kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela na kuwabwaga wagombea wengine sita waliokuwa wanawania kiti hicho cha ubunge.

 

Akitangaza rasmi matokeo hayo jana, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilemela, John Wanga alisema Dk Angeline alipata kura 147,724 na kumshinda Greyson Waryoba wa Chadema aliyepata kura 24,022.

 

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Magu, Lutengano George alimtangaza Boniventura Kiswaga (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 139,975 sawa na asilimia 85.92, wapinzani wake wa Sospeter Lushanga-ACT-Wazalendo- wakipata 2,953 sawa na asilimia 1.87 na Reginald Kwizera wa Chadema kura 14,475 asilimia 4.19.

 

Bukoba Mjini yarejea

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Bukoba Mjini amemtangaza Stephen Byabato (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 29,883 dhidi ya Chifu Karumuna (Chadema) aliyepata kura 16,673.

 

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Magharibi, Saad Mtambule alimtangaza mshindi Noah Mollel (CCM) kura 72,160 akifuatiwa na John Kivuyo ACT Wazalendo aliyepata kura 2,492 na Gibson Blasus (Chadema) kura 22,743.

 

Jimbo la Arumeru Mashariki, Msimamizi wa Uchaguzi Emmanuel Mkongo alimtangaza Dk John Pallangyo (CCM) kuwa alipata kura 84,858 dhidi ya Rebeca Mngodo (Chadema) aliyepata kura 14,688.

 

Jimbo la Kasulu Vijijini, Vuma Augustino (CCM) ameshinda kwa kupata kura 37,795 sawa na asilimia 54 akifuatiwa na Simon Ruseba (Chadema) 20,904 asilimia 30 na Kazara Kinyoma (ACT-Wazalendo) kura 975 asilimia 14.

 

Tabora yote CCM

Mkoani Tabora, CCM imezoa majimbo yote; Jimbo la Nzega Mjini, Husein Bashe amepata kura 16,082 akifuatiwa na Andrew Atonga wa Chadema kura 2,663, Antony Sambali ACT Wazalendo kura 166 na Masudi Salum CUF kura 102

 

Jimbo la Nzega Vijijini, mgombea wake, Dk Hamis Kigwangalla alipita bila kupingwa, lakini Jimbo la Bukene, Selemani Zedi ameshinda.

 

Jimbo la Sikonge, mshindi aliyetangazwa ni Joseph Kakunda wakati Jimbo la Igalula ametangazwa Protes Venant kuwa mbunge mpya, huku Tabora Kaskazini, Amasi Maige ametetea kiti chake.

 

Wakati Ulyankulu mgombea Rehema Magila alipita bila kupingwa, CCM imeshinda pia Urambo kupitia kwa Margaret Sitta, Kaliua mshindi ni Alois Kwezi, Seif Gulamali ametetea kiti Manonga, wakati Emmanuel Mwakasaka ameshinda tena Tabora Mjini na kuweka rekodi ya kutetea kiti hicho kwa mara ya pili. George Ngasa ameshinda Igunga.

 

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Mikumi na Kilosa, Asajile Mwambambale alitangaza James Londo (CCM) kuwa mshindi katika Jimbo la Mikumi kwa kupata kura 31,411 sawa na asilimia 62.7 dhidi ya Joseph Haule wa Chadema aliyepata kura 17,375 asilimia 34.7 .

 

Mgombea wa Ubunge Jimbo la Ulanga, Salim Hasham (CCM) ameibuka mshindi baada kupata kura 32,613 sawa na asilimia 75, mgombea wa Chadema, Simba Imani kura 9,393 sawa na asilimia 21.61, mgombea wa CUF, Batuli Mtenga kura 459 sawa na asilimia 1.06, na wa NCCR Mageuzi, Tumbo Kichamo kura 147 sawa na asilimia 0.34.

 

Katika Jimbo la Arusha Mjini kama ilivyokuwa kwa Jimbo la Kawe, matokeo yake yalikuwa yakisubiri kwa hamu, lakini hadi tunakwenda mitamboni yalikuwa hayatangazwa ingawa kulikuwa na dalili kuwa miaka 10 bungeni ya Gobless Lema na Halima Mdee imefika mwisho, ushindi ukielekea kwa Mrisho Gambo na Askofu Josephat Gwajima.

 

Katika kituo cha kujumuisha matokeo cha Jimbo la Arusha Mjini, ilipofika saa 12 jioni jana wanaCCM walikuwa wakiiimba ‘tunamtaka mbunge wetu.”

 

Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo ameshinda kwa kura 79,950, akifuatiwa na Abbas Mayala wa Chadema kura 11,285, Precedius Luhabuza wa ACT Wazalendo kura 637 na Felician Lutandala wa CUF kura 317.

 

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko (Dar), Halima Mlacha (Dar), Anastazia Anyimike (Dodoma), Veronica Mheta (Arusha), Amina Omari (Tanga), Nashon Kennedy (Mwanza),  Nakajumo James (Moshi), John Mhala (Longido), John Nditi (Moro), Frank Leonard (Iringa), Abby Nkungu (Singida), Fadhil Abdalla (Kigoma), Diana Deus (Bukoba), Lucas Raphael (Tabora), Kareny Masasy (Shinyanga), Peti Siyame (Rukwa) na Muhidin Amri (Songea).

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi