loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wingi wa CCM bungeni gumzo zito

MATOKEO ya uchaguzi ngazi ya ubunge yameibua mjadala juu ya suala zima la bunge kutawaliwa na chama kimoja huku baadhi ya watu wakilitabiria kufanya kazi kwa tija kuliko lilipokuwa na wabunge wengi wa upinzani. 

Watu wa kada tofauti waliozungumza na HbariLEO, wamesisitiza kwamba si sahihi kutafsiri hatua ya bunge hilo kuwa na wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba ni kufa kwa mfumo wa vyama vingi kwa kuwa hali hiyo imetokea kama matakwa ya wananchi kupitia sanduku la kura. 

Bunge la heshima

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili jana juu ya suala hilo, ni pamoja na Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa aliyesema anaona bunge litarudi kama enzi za chama kimoja lilipokuwa likijadili hoja kwa heshima na mashiko tofauti na lilipokuwa na wapinzani wengi. 

“Wakati ule ilikuwa rahisi kujadili hoja kwa utulivu na kuzipitisha tofauti na Bunge lililopita lililokuwa na viti vya upinzani zaidi ya 100, limejaa vurugu na hoja zisizo na tija, mara wamesusia bajeti kwa kweli ilikuwa ni vurugu na unaona kabisa lilikosa nidhamu,” alisema Msekwa. 

Akaongeza: “Hata wananchi walichoshwa na hayo mambo wakaamua kuwafundisha, wamewashikisha adabu.” 

Msekwa ambaye aliongoza chombo hicho kabla na baada ya nchi kuingia mfumo wa vyama vingi, alisema nchi haijakosa wawakilishi kwa sababu kila mbunge akichaguliwa anawakilisha wananchi wa jimbo lake. 

Alisema pia sheria zinapotungwa zinakwenda kusaidia kila Mtanzania hivyo haoni kama kupungua kwa viti vya upinzani kutaleta athari mbaya kwa bunge katika kufanya uamuzi na kusimamia serikali na badala yake bunge litakuwa na mijadala yenye afya.

Uwajibishaji serikali

Mwingine aliyezungumza na gazeti hili ni aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR Mageuzi, David Kafulila aliyesema upinzani ni dhana iliyojengea watu mtazamo kwamba ili bunge liwe shirikishi katika kuiwajibisha serikali kuhimiza ifanye maendeleo, ni lazima kuwe na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani jambo alilosema si sahihi. 

“Hii ni dhana tu, lakini mimi naamini hata wabunge wa CCM wanaweza kusimama kuiwajibisha serikali na kupinga hoja wanazoona hazina manufaa kwa wananchi kwa hiyo kuwa na idadi ndogo ya viti vya upinzani hakuwezi kuleta athari katika uwezo wa bunge kusimamia serikali.”

“Bunge litaendelea kubaki kuwa shirikishi kama ilivyokuwa awali na hii ni historia ambayo ipo muda mrefu,” alisema Kafulila.

Alisema kitu ambacho wananchi watakikosa katika bunge hilo ni malumbano ya kisiasa ambayo sehemu yake kubwa, hayakuwa na tija. 

Aliyekuwa mbunge katika Bunge la 11 ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini aliyesema, Bunge litakuwa na tija zaidi kwa sababu hoja nyingi zitaamuliwa kwa mantiki na si kwa ushabiki wa pande mbili kati ya upinzani na chama tawala. 

Mbunge huyo ambaye ameshinda kwenye uchaguzi huu, alisisitiza kwamba mfumo wa vyama vingi haujafa na kwamba matokeo hayo iwe changamoto kwa vyama vya upinzani kujitazama na kuona wanaposhindwa ili wajirekebishe na kukubalika kwa wananchi.

“Itakuwa mijadala yenye afya tofauti na ubishi na kupinga kila jambo. Baraza la Wawakilishi (Zanzibar) walikuwa asilimia 100 ya wawakilishi wote wakiwa wa CCM na lilikwenda vizuri. Watanzania wasikate tamaa wala wasidanganywe,” alisema. 

Aliendelea kusema: “Waligeuza bunge kama gulio… Huwezi ukawa unapinga maendeleo yote; lazima wabadilishe mwelekeo na kufanya tathimini ya upungufu wao. Uchaguzi huu uwe funzo kwao, wabadilishe mfumo wao.” 

Fursa ya kuamua

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Joseph Lugendo alisema ushindi huo wa CCM katika nafasi nyingi za viti vya ubunge utawezesha kufanya maendeleo kwa haraka endapo watataka kupitisha jambo lolote watakalotaka bila kuwa na upinzani mkubwa.

Hata hivyo alisema, chama hicho kitatakiwa kuhakikisha hawashindwi katika mambo kiliyowaahidi wananchi vinginevyo, kitabebeshwa mzigo kwa kila udhaifu utakaojitokeza kutokana na uamuzi wake bungeni. 

“Huu ni mzigo mzito CCM wamejitwika, wakishindwa kutekeleza waliyoyaahidi hawatakuwa na mtu wa kumrushia lawama … yatawarudia,” alisema. 

Ni mapema kutabiri

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Lousile, amesema ni mapema kutabiri na kulielezea bunge lijalo litakuwa na ubora gani kutokana na wingi wa wabunge kutoka CCM. 

Lousile alisema bunge lijalo litakuwa la kijani kwani hadi sasa wabunge walioshinda wametoka CCM, lakini ni mapema kutabiri litakavyokuwa hadi litakapozinduliwa na watakapoanza kufanya kazi zao kama wabunge.

“Bunge lijalo limekuwa kijani tupu, wabunge wengi wametoka CCM… hatuwezi sasa kutabiri litakuwaje ni mapema, lakini likizinduliwa ndio tunaweza kupima uwezo wao ukoje,” alisema.

Alisema zamani lilikuwapo bunge la chama kimoja, lakini ndani waliibuka wapinzani wakitoa na kuibua hoja, mijadala na kukosoa ndani ya bunge, hivyo Watanzania wasubiri kuona bunge lijalo kwani inawezekana likawa na mvuto wa aina yake.

Kulingana na matokeo ya ubunge yaliyotangazwa ambayo ni zaidi ya robo tatu ya majimbo yote hadi tunakwenda mitamboni, CCM kilikuwa kinaongoza kwa wingi wa majimbo huku upinzani ukipata viti viwili. 

Bunge la 11

Kwa mujibu wa Kitabu cha Kumbukumbu za Wabunge, Bunge la 11, Toleo la Tatu-Februari 2019, idadi ya wabunge waliokuwapo ilikuwa 392 ambao kati yao, wabunge wa majimbo walikuwa 263. 

Idadi ya wabunge wa majimbo wa CCM ilikuwa 206, CUF 29, Chadema 26, ACT wazalendo mmoja, NCCR Mageuzi mmoja. 

Idadi ya wabunge wa viti maalumu ilikuwa 113 huku wabunge wa viti maalumu wa CCM walikuwa 66, Chadema 37, CUF 10. 

Wabunge wa kuteuliwa na rais walikuwa 10. Idadi ya wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi walikuwa watano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Kitabu hicho kinaonesha mgawanyo wa wabunge kichama ulikuwa CCM 287, Chadema 63, CUF 39, ACT Wazalendo mbunge mmoja, NCCR Mageuzi mmoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Akizungumzia sura ya Bunge lijalo, Msomi na Mwanadiplomasia ya Uchumi, Dk Watengere Kitojo alisema bunge linaweza kupoa kwani kwa matokeo yaliyotangazwa hadi sasa zaidi ya majimbo 220 kati ya 264 ya ubunge wamechukuliwa na wabunge wa CCM huku wa upinzani wakiambulia mawili.

“Kwa sisi ambao hatuegemei chama na tunaopenda kukosolewa, tungetamani wabunge wa upinzani wengi wangekuwepo ili tusikie hoja za pande zote jinsi wanavyokosoana ili kujenga, sasa kwa sura hii bunge linaweza kupoa, ingawa pia wanaweza kuibuka wabunge wapinzani ndani ya chama tawala na kubeba nafasi ya wale wa upinzani,”alisema Dk Kitojo.

Alisema hayo yote yametokana na vyama vya upinzani kushindwa kupanga karata zao mapema, lakini pia sera na hoja zao kuwa dhaifu ukilinganisha na hoja za CCM ambazo zimeonekana kutekelezeka zaidi na kutatua kero ya Watanzania.

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola na Angela Semaya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi