loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wabunge wateule waahidi makubwa

BAADHI ya wabunge wateule wameeleza siri ya ushindi wao na kuahidi kutekeleza mambo mbalimbali kuwaletea wananchi maendeleo. 

Mbunge mteule wa Jimbo la Muheza, Hamisi Mwinjuma maarufu kama Mwana FA baada ya kutangazwa aliwashukuru wananchi wa Muheza kwa kumpa ushindi na kusema kuwa wamemkopesha kura na kwamba  atawalipa maendeleo.

Mbunge mteule wa Tunduru, Daimu Mpakate alisema ushindi alioupata haukuwa rahisi kutokana na mgombea wa chama cha ACT Wazalendo, Abdala Mtutura kuwa na uzoefu katika siasa kwani alishawahi kuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano.

Mpakate aliwaahidi wananchi na wapiga kura wa jimbo hilo kuwa, katika kipindi cha miaka mitano atahakikisha wanasimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana na wananchi.

Alisema moja kati ya changamoto kubwa katika jimbo hilo ni miundombinu mibovu ya barabara, kwa hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) changamoto hiyo itakwisha. Aliwataka wapiga kura kuwa na imani naye.

Kutoka Kishapu, mkoani Shinyanga mbunge mteule wa jimbo hilo Boniface Butondo alisema kuwa  atahakikisha yale yote  aliyoahidi  kwa wananchi anayasimamia   na kutekeleza  ikiwamo upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo hayana pamoja na  usimamizi kwa wachimbaji wadogo wa almasi.

Kwa upande wake, mbunge mteule wa jimbo la Solwa, Ahmed Salum  baada ya kutangazwa alisema kuwa anashukuru  kupata nafasi hiyo  huku akiainisha vipaumbele vyake  ni  kuhakikisha anafikisha maji, umeme na afya katika maeneo ya vijiji.

Mbunge mteule wa jimbo la Mbarali, Francis Mtega alisema ushindi wa kishindo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo ni matokeo ya wananchi kuielewa vizuri Ilani ya chama hicho sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika miaka mitano iliyopita chini ya Rais John Magufuli.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi, Mtega alisema wananchi walisoma ilani ya CCM na kuielewa na kwa kuwa imeeleza mambo mengi yanayogusa maendeleo yao.

Alisema zawadi pekee anayotakiwa kuwapa watu wa jimbo hilo ni kuwatumikia kwa uadilifu mkubwa na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alitaja mambo atakayoanza nayo mara baada ya kuapishwa kuwa ni pamoja na kutafuta suluhisho la migogoro ya ardhi ambayo ndiyo changamoto kubwa wilayani hapa sambamba na migogoro ya wakulima na wafugaji.

 “Ni kweli Mbarali ina changamoto nyingi sana..kuna migogoro mingi ya ardhi, migogoro baina ya wakulima na wafugaji ni mingi na hata wakati wa kampeni zangu nilikuwa nikisisitiza sana amani umoja, utulivu,mshikamano ili sisi sote tuishi kwa undugu kwa sababu wote tunategemeana,” alisema.

Mtega aliwaomba pia wana Mbarali wakiwamo waliokuwa wagombea wenzake kupitia vyama vingine kushirikiana kwa pamoja wakitambua kuwa wagombea walikuwa wengi lakini nafasi ilikuwa ya mtu mmoja hivyo ni wakati wa kushirikishana mawazo kwakuwa lengo ni kuwaletea maendeleo wananchi.

Kutoka Mwanza, mshindi wa kiti cha ubunge katika jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM),Dk Angelina Mabula aliwashukuru wakazi wa jimbo la Ilemela kwa kumchagua tena aweze kuwaongoza kwa miaka mitano mingine.

Akizungumza katika ofisi za CCM, kata ya Kirumba, Dk Mabula alishukuru kwa kupata ushindi wa asilimia 84.

Wakati huo huo,  kutoka mkoani Arusha, mbunge mteule wa Jimbo la Longido, Dk Steven Kiruswa, alisema hatawaangusha wananchi kutokana na  imani waliyoionyesha wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi