loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Wasomi, wanasiasa waeleza kilichoponza upinzani

ANGUKO la upinzani katika matokeo ya uchaguzi mkuu yanayoendelea kutangazwa nchini limetajwa kuwa limechangiwa na na vyama husika vya siasa kukosa hoja zenye mashiko za kuwashawishi Watanzania wawachague. 

Aidha, kitendo cha serikali kutimiza kiu ya wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ni jambo lingine lililofanya wananchi kutochagua vyama vya upinzani. 

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti baada ya matokeo ya udiwani na majimbo takribani 220 ya ubunge kutangazwa kati ya majimbo 264, watu wa kada tofauti wamesema matokeo yamedhihirisha kuridhishwa na utelelezwaji wa mambo mbalimbali yaliyoahidiwa. 

Msomi na Mwanadiplomasia, Dk Watengere Kitojo alisema matokeo yametawaliwa na hali halisi ya vitu vinavyoonekana kufanywa na serikali na siyo ahadi hewa.

“Mimi siyo mwanachama wa chama chochote, ni mwana diplomasia na uchumi ninachokiona katika matokeo haya Watanzania uamuzi wa yale waliyotaka, wameona kero zao zimetatuliwa, kiu yao imetimizwa na serikali ya awamu ya tano, upinzani kwa kweli walikosa hoja kwa maana hoja zote zilikuwa zimeshasemwa au kutimizwa kwa kiasi na serikali,” alisema Dk Kitojo.

Alisema wapinzani hawakuja na hoja za kushawishi  Watanzania kuwachagua bali zaidi walinadi hoja ya kudai maendeleo ya watu na siyo ya vitu wakati ukweli ni kwamba maendeleo ya watu lazima yaanze na maandalizi ya vitu.

Dk Kitojo alisema mfumo wa hoja za wapinzani katika kampeni za uchaguzi huu hazikuwa nzito wala hawakuwa na sera zenye mashiko kushawishi Watanzania kuwapigia kura na kusema mfumo wao wa kutengeneza hoja ulikuwa dhaifu.

“Upinzani hawakujipanga, mfumo wao wa hoja ulikuwa dhaifu sana, hata mwelekeo ya matokeo ya urais unaona walishindwa kuchanga karata zao vizuri za kupata mgombea anayekubalika kwa Watanzania, wakafikiri watapewa madaraka kwa kuonewa huruma, walikosa sera na mgombea makini,’’ alisema Dk Kitojo.

Akizungumzia masuala ya diplomasia ya uchumi juu ya mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, Dk Kitojo alisema:

“Katika Diplomasia ya Uchumi, Lissu ni adui namba moja wa nchi, walikosea kumpa nafasi ya kugombea urais kwa sababu alizunguka mataifa ya nje kuichafua nchi yake, hiyo haikubaliki kidiplomasia kabisa. Hata kama nyumbani kwako ni kubaya huwezi zunguka nje kuisema na kuipaka matope nyumba yako, halafu unarudi unaomba upewe ridhaa ya kuiongoza, haikubaliki,’’alisema. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Lousile alisema wapinzani wanatakiwa kujipanga na kuweka mikakati ya ushindi kama chama kwa ajili ya uchaguzi ujao na kuhakikisha wanarekebisha kasoro au dosari zao.

“Umefika wakati wa wapinzani kutengeneza mikakati mapema kama chama, badala ya mgombea mmoja mmoja. Wengi wao walikuwa wakipambania kila mtu binafsi kushinda kwenye jimbo lake lakini hawakujenga msingi wa kwenda kimkakati kama chama kuhakikisha ushindi,” alisema. 

Aliendelea: “Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekuwa na utaratibu wa kujipanga kuanzia ngazi ya chama hadi kwa wagombea wake na kubebana kuhakikisha ushindi badala ya kwenda mmoja mmoja.”

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, alisema hatua yao ya kupinga miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kasi kwa miaka mitano ya Rais John Magufuli ni sababu kubwa.

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Maggid Mjengwa pia alisema dhana ya kupinga maendeleo ya vitu kuwa sababu ya maendeleo ya watu ndio hasa kilichosababisha wapinzani kukosa majimbo mengi.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, wabunge wengi wa upinzanii wakiwemo waliokuwa madarakani kwa miaka 10 wameanguka katika majimbo yao huku wabunge wa CCM wakiibuka washindi. Hadi jana mchana, kati ya majimbo 220 yaliyotangazwa, upinzani umepata majimbo mawili. 

Rais wa Tanzania Dk John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi