loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Shivyawata waomba mifuko 100 ya saruji

SHIRIKISHO la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) Kibaha Mjini Mkoa wa Pwani, limeomba wadau wa maendeleo kuwasaidia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza mradi wao wa ufyatuaji wa matofali.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Katibu wa Shivyawata, Happiness Matagi alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake.

Matagi alisema kuwa mradi huo uliyumba kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

“Mradi unashindwa kwenda vizuri kutokana na mota wanayoitumia njia moja inayotumika kufyatulia tofali huwa inaungua ambapo inatakiwa ni ya njia tatu ambayo ndiyo itakuwa na uwezo," alisema Matagi.

Alisema kuwa mota hiyo imekuwa ikiungua mara kwa mara na kusababisha gharama kuwa kubwa na gharama nyingine zinatokana na matumizi ya maji.

“Tunaomba watu mbalimbali watusaidie mifuko 100 ya saruji, mchanga lori 20 na ujenzi wa kisima cha maji ili kupunguza gharama za maji kwani bili inayokuja ni kubwa sana,” alisema Matagi.

Alisema kuwa ili kuboresha mradi huo, pia wanahitaji mashine ya kuchanganyia mchanga badala ya mashine wanayoitumia ya kuchanganya na mikono.

“Mradi ulianza mwishoni mwa mwaka jana na tayari walishafyatua matofali 4,000 na sasa zimebaki tofali 700 na fedha za kuanzishia mradi huo walipata mkopo wa shilingi milioni 10 kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha,” alisema Matagi.

Aliongeza kuwa wanachama wa Shivyawata kupitia vikundi wana miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya ushonaji, maduka ya simu, utengenezaji wa simu, ushonaji nguo, ushonaji viatu, bustani, ushonaji wa mazulia, ufugaji wa kuku na uuzaji wa mbuzi ambapo vikundi 25 vimepokea mikopo kutoka halmashauri.

Matagi aliongeza kuwa endapo watapatiwa vitu hivyo, watakuwa na uwezo wa kuendesha mradi na kituo chao ambacho walikabidhiwa na halmashauri.

foto
Mwandishi: John Gagarini, Kibaha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi