loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Anguko la upinzani ni matokeo ya ukosefu wa hoja

OKTOBA 28, mwaka huu, Watanzania 15,091,950 walipiga kura kuwachagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitano.

Kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi huo uliovishirikisha vyama vya siasa 19, kati ya hivyo vyama 15 vilisimamisha wagombea kwa ngazi ya urais, wabunge na madiwani, ambako Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitoa takwimu zinazoonesha jumla ya wapigakura waliojiandikisha kwenye daftari la wapigakura walikuwa 29,754,699.

Idadi hiyo ni kubwa lakini cha kushangaza ni mwamko mdogo uliojitokeza wa wapigakura ambao karibu nusu ya wapiga kura hawakupiga licha ya kujiandikisha.

Hiyo imetokana na sababu mbalimbali zilizotajwa na baadhi ya wasomi na wananchi wa kawaida kuwa ilichangiwa na vyama vya upinzani kutoa matishio ya amani wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi.

Baadhi ya vitisho hivyo vilisababisha wapigakura wengi kuogopa kwenda vituoni kwa hofu ya kuzuka kwa vurugu ilhali ukweli ni kwamba uchaguzi ulienda kwa amani na utulivu mkubwa.

Matokeo yalionesha kuwa vyama vya upinzani na wagombea wake katika nafasi mbalimbali kuanzia udiwani hadi urais, vilipoteza nafasi nyingi huku Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiibuka mshindi kwa kujizolea madiwani, wabunge 256 kati ya wabunge 264 wa majimbo.

Vyama vya upinzani kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiambulia mbunge mmoja, Chama cha Wananchi (CUF) kimepata wabunge watatu, Chama cha ACT-Wazalendo kimepata wabunge wanne.

Wakizungumzia anguko hilo la upinzani, watoa maoni wamesema limechangiwa na vyama husika vya siasa kukosa hoja zenye mashiko za kuwashawishi Watanzania kuwachagua.

Pia imebainika kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilitimiza kiu ya wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inaonekana kwa macho hivyo kuwashawishi wananchi kutochagua vyama vingine ambavyo hata hivyo wanasema havikuwa na hoja nzito zenye ushawishi.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti baada ya NEC kutangaza matokeo ya uchaguzi huo yaliyowaangusha wagombea wengi wa vyama vya upinzani hata wale wakongwe, Msomi na mwanadiplomasia, Dk Watengere Kitojo anasema matokeo yametawaliwa na uhalisia wa vitu vinavyoonekana kufanywa na serikali na sio ahadi hewa.

Dk Kitojo aliyesema si mwanachama wa chama chochote, bali msomi na mwanadiplomasia ya uchumi na anachokiona kwenye matokeo hayo ni kwamba Watanzania wameamua kutokana na yale waliyoyaona yanatekelezwa huku kero zao zikitatuliwa.

Anasema kiu ya Watanzania wengi imekatwa, lakini pia vyama vya upinzani vingi havikuwa na hoja kwani hoja zilizokuwepo awali zimefanyiwa kazi na Serikali ya Awamu ya Tano na sasa utekelezaji wake unaonekana kwa macho.

“Wapinzani hawakuja na hoja za kushawishi  Watanzania kuwachagua bali zaidi walinadi hoja ya kudai maendeleo ya watu na si ya vitu wakati ukweli ni kwamba maendeleo ya watu lazima yaanze na maandalizi ya vitu,” anasema.

Katika hilo, Dk Kitojo anawashauri wapinzani kuwa mfumo wao wa hoja unapaswa kutengenezwa upya na kuja na sera zenye mashiko zitakazoshawishi Watanzania kuwapigia kura.

“Upinzani hawakujipanga, mfumo wao wa hoja ulikuwa dhaifu sana, nilitegemea haya matokeo tangu mwanzo, walishindwa kuchanga karata zao vizuri za kupata mgombea anayekubalika kwa Watanzania, wakafikiri watapewa madaraka kwa kuonewa huruma, walikosa sera na mgombea makini,” anasema Dk Kitojo.

Akizungumzia masuala ya diplomasia ya uchumi juu ya mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu, Dk Kitojo anasema:

“Katika Diplomasia ya Uchumi, Lissu ni adui namba moja wa nchi, walikosea kumpa nafasi ya kugombea urais kwa sababu alizunguka mataifa ya nje kuichafua nchi yake, hiyo haikubaliki kidiplomasia kabisa. Hata kama nyumbani kwako ni kubaya huwezi zunguka nje kuisema na kuipaka matope nyumba yako, halafu unarudi unaomba upewe ridhaa ya kuiongoza, haikubaliki.”

Wakati Dk Kitojo akisema hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Lousile anapigilia msumari hoja hiyo kwa kusema wapinzani wanatakiwa kujipanga na kuweka mikakati ya ushindi kama chama kwa ajili ya uchaguzi ujao na kuhakikisha wanarekebisha kasoro au dosari zao.

“Umefika wakati wa wapinzani kutengeneza mikakati mapema kama chama, badala ya mgombea mmoja mmoja. Wengi wao walikuwa wakipambania kila mtu binafsi kushinda kwenye jimbo lake lakini hawakujenga msingi wa kwenda kimkakati kama chama kuhakikisha ushindi,” anasema Dk Lousile.

 Anaongeza, “CCM imekuwa na utaratibu wa kujipanga kuanzia ngazi ya chama hadi kwa wagombea wake na kubebana kuhakikisha ushindi badala ya kwenda mmoja mmoja.”

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini anasema kitendo cha wapinzani kupinga miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kasi kwa miaka mitano ya Rais John Magufuli ni sababu kubwa ya wananchi kuwanyima kura.

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, Maggid Mjengwa anasema dhana ya kupinga maendeleo ya vitu kuwa sababu ya maendeleo ya watu ndio hasa kilichosababisha wapinzani kukosa majimbo mengi.

Mhadhiri na Mchambuzi wa Masuala ya Diplomasia wa Chuo cha Diplomasia Tanzania (CFR), Israel Sosthenes anasema wapinzani walikuwa na ushawishi wa aina yake kwenye vyombo vya uamuzi mfano Bunge, na hata baraza la madiwani na kwamba kuanguka kwao kunatokana na hoja zao wenyewe.

Sosthenes anasema kwa anguko hilo, ndani ya wabunge na wadiwani wa chama tawala wataibuka wenye mtazamo tofauti wa kuibua hoja kama zilizokuwa zikiibuliwa na hao wa upinzani na hivyo kwa wale wanaodhani Bunge halitakuwa kali, mawazo yao si sahihi.

“Unajua ndani ya chama kuna wanaoibuka na kuwa wapinzani kwa wengine, sasa katika Bunge lijalo, hasa baada ya upinzani kuanguka wataibuka wabunge watakaoonekana machachari na kuziba ile nafasi ya hao wapinzani tena mpambano unaweza kuwa mkali kuliko isivyotarajiwa,” anasema Sosthenes.

Ismail Ramadhani ni mfanyabiashara mkazi wa Dar es Salaam anasema anguko la vyama vya upinzani lilitegemewa kutokea mapema kutokana na wao kuanza kususa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana, ambao baadhi ya vyama hivyo viliwataka wagombea wao kujitoa katika uchaguzi huo ilhali walikuwa wanakubalika.

“Kwenye ule uchaguzi wa viongozi wa mitaa, viongozi wa vyama vya upinzani walipowalazimisha wagombea wao kujitoa ilhali walikuwa wanakubalika ndio mgogoro ukaanza, cha kushangaza viongozi hao wakagombea kwenye Uchaguzi Mkuu nafasi mbalimbali, hapo ndipo wananchi wakakosa imani na wengi wakawanyima kura,” anasema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, matokeo yake yamempa ushindi mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli huku pia chama hicho kikipata madiwani wengi na wabunge 256 wa majimbo kati ya majimbo 264 na kushuhudia wabunge wengi wa upinzani wakiwamo waliokuwa madarakani kwa miaka 10 wakipoteza majimbo yao.

 

WIKI iliyopita kulifanyika maadhimisho ya siku ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

1 Comments

  • avatar
    Mitana kadorho
    05/11/2020

    Wapinzani wajilaumu wenyewe, hakuna mtu anapinga maendeleo ya rais Magufuli. Watanzania ndugu zangu, mimi siko mtanzania, lakini Magufuli ameacha niipende Tanzania kuliko taifa langu. Mimi kwa upande Wangu, ni Magufuli njoo alipashwa kulalamika kuhusu kura zake, maana nina uhakika alipashwa kushinda na 98 %.Bila haya wapinzani wenu wanajigamba eti walionewa. Nani mtu mwenye akili timamu angechagua Lissu asiye na adabu kwa rais wake na taifa lake? Ilitakiwa akamatwe, afungwe jela kwa kukisaliti taifa la Tanzania

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi