loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Mafunzo, uhusiano bora huongeza ufanisi kazini

 NI ukweli usiopingika kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi hutumia muda mwingi wanapokuwa kazini kuliko wanaoutumia kuwa nyumbani na familia zao.

Kutokana na muda mwingi zaidi kwa siku hutumika ofisini na siyo nyumbani, mazingira ya kazi siku zote na mahali pote yanapaswa kuwa rafiki, ya kuvutia  na ya kuridhisha likiwamo suala la upatikanaji wa vitendea kazi na nyenzo nyingine muhimu zinazochochea utendaji kazi wa ufanisi.

Ni kwa msingi huo, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakary Kunenge alisema viongozi katika ofisi mbalimbali na kwa ngazi mbalimbali, wanapaswa kuwathamini wafanyakazi na wasaidizi wao ili kuwatia ari na moyo wa ufanisi hali inayoongeza tija.

Kunenge alikuwa akizindua Baraza la Wafanyakazi la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) jijini Dar es Salaam aliposhauri wafanyakazi wote kuthaminiwa na kusaidiwa kwa usawa yaani, wanaoonekana kufanya vizuri, na hata wenye upungufu ili nao wawe bora.

Hata hivyo, akasema wasiotaka kubadilika kiutendaji na hata kimaadili, wawajibishwe kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Kimsingi katika mazingira yote ya kazi ama ziwe za ofisini, au nje ya ofisi, uhusiano bora unaozingatia haki na wajibu wa mwajiri, mwajiriwa na hata viongozi waliopo huongeza tija kwa kuwa huchochea moyo wa wafanyakazi wote kujitolea, kujituma, kujifikirisha zaidi na kila mmoja kutamani kufanya kazi kwa ufanisi zaidi bila manung’uniko.

Kitendo cha viongozi wa ngazi mbalimbali katika taasisi, shirika au kampuni yoyote kuwa na mifumo mizuri inayoweka milango wazi kwa watumishi kuwasilisha changamoto zao kwa mujibu wa taratibu, husaidia kuwabaini na kuwapa msaada kadiri ya mahitaji na taratibu zilizopo.

Hii ni kwa kuwa siyo siri kwamba, inawezekana mfanyakazi anayeonekana kuwa na upungufu, ni bora zaidi kiutendaji kuliko anavyoonekana hasa anapothamaniwa na kutambua kuwa anathaminiwa.

Ifahamike wazi kuwa, mfanyakazi wa ngazi yoyote anaweza kuwa na changamoto zikiwamo za kifamilia ama za kikazi zinazohitaji msaada, ushauri au kutiwa moyo hasa na viongozi wake wa karibu kwani ndio wanaomjua na kufanya naye kazi kwa karibu.

Haya yote, yatakaa sawa kama taasisi husika pia itakuwa na mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi yakiwamo ya kisaikolojia.

Ndiyo maana ninasema, wafanyakazi wanapothaminiwa na kutambuliwa kazi zao, ama kupewa marupurupu mbalimbali hata kama maslahi yao ni ndogo, huongeza  ari ya kufanya kazi na kuongeza ufanisi.

Ifahamike kuwa, migogoro kazini inapoondolewa ama wafanyakazi wanaposikilizwa na kushirikishwa mambo mbalimbali kuhusu utendaji wao, huongeza uzalishaji kwa kuwa hujiona ni sehemu ya kampuni ama taasisi husika.

Uhusiano mzuri unapojengwa ofisini, hupunguza majungu na migogoro na kuchochea amani zaidi na nidhamu hali inayofanya wafanyakazi kuhudumia wateja wao kwa moyo.

Ikumbukwe kuwa, nidhamu ya kazi baina ya viongozi na wafanyakazi ni msingi mkubwa wa mafanikio kazini.

Ndiyo maana ninasema, popote pale, kila mmoja awe sehemu ya ofisi yeke na ili kuchochea ufanisi, mafunzo kazini yakiwa ya saikilojia na uhusiano huongeza ufanisi kazini.

 

 

WIKI iliyopita kulifanyika maadhimisho ya siku ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi