loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Tanzania mpya inakuja, sote tushiriki kujenga uchumi

HOTUBA ya Rais John Magufuli imeelezewa kuwa ni ya kipekee, iliyotoa taswira nzima ya maendeleo ya Watanzania kwa kugusa kila eneo na Wananchi wa kila kada.

Gazeti hili, lilizungumza na makundi mbalimbali ya Watanzania wakiwemo wasomi, viongozi wa dini, wafanyabiashara, wajasiriamali, wanasiasa na  wananchi wa kawaida, ambao wanaamini kuwa inatekelezeka kwa vitendo kwa namna ambavyo rais amejipambanua tangu awali katika kipindi cha kwanza kwamba akiahidi anatenda.

Mchungaji wa Taasisi ya Sauti ya Uhuru Shangwe Habari njema, iliyopo Kigamboni Dar es Salaam, Mchungaji Manfred Kashasha alisema hotuba hiyo ni ya kimapinduzi inapindua fikra kwa watanzania kuwa na mitazamo mipya ya kujitambua.

“Hotuba inazaa kizazi kipya kinachojitambua inaamsha namna ya kujitambua. Tunakuwa na uwezo wa kuamua mambo yetu. Inatusaidia kutambulika na ulimwengu na kuheshimika kama taifa. Magharibi walidhani hatuwezi kufanya vitu bila misaada. Ni mapinduzi ili dunia ijue kuwa Tanzania ndiyo kichwa cha Afrika,” alisema.

Alisema kupitia hotuba hiyo, sasa hatutapiga hodi kuomba msaada bali rasilimali zetu ndizo zitakazotumika. “Maeneo nina hakika yataleta mapinduzi ni kama Tanzania ya viwanda kwa sababu tuna raslimali nyingi. Na pia litaleta ajira. Nina hakika litatekekelzwa kwa sababu rais anachosema anatekeleza. Akipata timu sahihi litatekelezwa.

Kama kiongozi wa dini alisema ana jukumu la kuhamaisha waumini namna ya kuwa raia wema, wawajibike na wawe mabilionea na kuongeza kuwa amani na utulivu ni mahitaji ya maendeleo ambayo viongozi wa dini wanatakiwa kufundisha, kuhamasisha kupitia makongamano na mikutano.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima kwa upande wake, alisema kwa ujumla hotuba ya Rais Magufuli  imetoa mwelekeo mzima wa maendeleo ya Watanzania hasa kwenye maeneo ya msingi ya miundombinu na uchumi.

“Ni wazi huduma za jamii zitakuwa na muendelezo wake wa kuboreshwa lakini kubwa zaidi ni namna alivyotoa kipaumbele katika kuitambua sekta binafsi. Hiki kilikuwa kilio cha Wananchi kwa muda mrefu lakini sasa Rais huyu ameanza kukifanyia kazi,” alisema Dk Kitima.

Hata hivyo, alieleza kuwa pamoja na hotuba hiyo iliyojaa maono mazuri hususani kwa sekta binafsi kuna haja ya wizara husika zitakateuliwa kuwajibika kwa vitendo na kuonesha hasa dhamira ya Rais ya kushirikiana na sekta binafsi.

Alisema Dk Magufuli anayo changamoto ya kuhakikisha wizara atakazoziteua zinatimiza dhamira na maono yake kwa vitendo na si kukaa ofisini na kutunga sera tu.

“Kwa Mfano jana (juzi) katika hotuba yake Rais alitaja mifuko mingi tu inayohusisha na uwezeshaji kwa wananchi si kwamba watu hawaijui ila mtu akienda kuomba mikopo anasumbuliwa sana hadi anaamua bora auze hata kitu chake afanye anachotaka. Hotuba hii nzuri iendane na utendaji mzuri wa watendaji,” alisisitiza.

Kupitia Ukurasa wake Twitter mbunge wa Tanga Mjini Ummy Mwalimu alisema hotuba ya Rais ni ya kihistoria.

“Hakika nchi yetu imepata kiongozi mwenye maono na dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo zaidi ya kiuchumi na kijamii ili kuwainua watanzania walio wengi,” aliandika kwenye ukurasa wake.

Naye, Mwenyekiti wa TCCIA Wilaya ya Kibiti/ Rufiji na mjumbe wa Baraza la Biashara la wilaya na mkoa na mjumbe wa halmashauri kuu ya TCCIA Mkoa wa Pwani Maxillian Masero alisema ameipokea kwa furaha hotuba hiyo kwa kuwa imegusa mambo mengi waliyochangia katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Na jambo kubwa ni kununuliwa ndege ya mizigo. Wiki mbili zilizopita nilikuwa Arusha na Moshi bidhaa zetu lazima zitoke Njombe ziende hadi Namanga kisha Nairobi ziwe processed kisha Mombasa na zinapewa origin ya Kenya…,”

“…Kwanza tunakosa mapato na bidhaa zetu zinaonekana ni za Kenya nao wanapata kodi na chukulia usumbufu tunaopata hadi kufika Nairobi lakini tungekuwa na ndege inakwenda moja kwa moja bidhaa hazichelewi…hii  

ni fursa kubwa sana si kwa serikali tu bali uchumi wa nchi,” alisisitiza.

Alisema katika hotuba hiyo, Dk Magufuli alikaribisha uwekezaji na kufungua milango ya sekta binafsi hivyo TCCIA kama wadau wanapaswa kuibeba tuwe bega kwa bega na kumuunga mkono rais.

Naye, Katibu wa Chama Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia (UWAWATA) Lucas Mlipu, alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwagusa waganga na wakunga wa tiba asili jambo linalozidi kuwapa moyo.

“Siku za nyuma waganga tulikuwa hatuonekani, tulikuwa tunapotezewa tu ilifikia mahala hata hatuwezi kwenda Kanisani kuabudu wala Misikitini wakati sisi ni sawa tu na watoa huduma wengine wa huduma za afya. Lakini tunamshukuru Rais pale aliposema tiba asilia zisidharauliwe,” alisema.

Alisema kutokana na uamuzi wa Dk Magufuli wa kuruhusu matibabu na maduka rasmi ya dawa za asili nchini, akiwa kama Katibu atahakikisha waganga wote nchini wanasajiliwa, dawa zao zinapimwa ili kuwa tayari kuwahudumia wananchi.

“Tunataka na sisi ifikie kipindi ndani ya miaka hii mitano kama waoa huduma wa tiba mbadala au asilia tunachangia kmapato ya nchi yetu,” alisema.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa mazingira Boneventura Mwalongo, alielezea hotuba hiyo kuwa imegusa eneo muhimu kwa watoa huduma ya tiba asili hasa suala la dawa kuendelezwa, kufunguliwa kwa vituo kwa maana ya maduka ambayo ni sehemu ya vituo.

Alisema kwa ujuma kuwa imegusa kila nyanja kwa mwananchi wa kawaida imemgusa kila mmoja, imegusa kilimo, afya, imegusa kila binadamu, miundombinu, biashara na usafirishaji, raslimali na mazao kitoka vijijini kwenda kwenye masoko. “Kwa kweli kila eneo limeguswa,”.

Naye, Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ernest Mulaya alimpongeza Rais Magufuli kwa hotuba nzuri iliyosheheni maono na mwelekeo wa taifa hususani kwenye eneo la gesi ya helium.

Mulaya ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Durham nchini Uingereza alisema kama mtaalamu wa jiolojia na jiosayansi ya gesi helium alifarijika baada ya Rais kuonyesha watanzania juu ya utajiri mkubwa wa gesi hiyo nchini unaokaribia kufikia futi za ujazo bilioni 138 kwa eneo la Rukwa tu.

Alisema kiasi hicho cha gesi ni kikubwa na endapo nchi itazalisha kiwango hicho maana yake ni kwamba Tanzania ina uwezo wa kumsambazia kila mtu duniani ambapo kuna jumla ya watu bilioni 7.8 kiasi cha mtungi wa futi za ujazo 18 zaidi ya lita 500.

"Habari njema ni kwamba gesi hii ya helium ni gesi ambayo kwanza baadhi ya matumizi yake hayana mbadala katika maisha na afya ya binadamu hasa hospitalini mbali na matumizi mengine kama vile anga, vifaa vya electroniki, maabara na nyinginezo.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Profesa Raphael Chigunda, alisema hotuba hiyo ya Rais ni ya kihisoria kwa kuwa imegusa mambo ya msingi yanayohitajika kusukuma nchi mbele.

Alisema pamoja na mambo mengine anampongeza Rais hasa kwa kutoa kipaumbele kwenye kilimo ambapo ameelezea namna serikali ilivyojipanga kukiboresha na kumaliza changamoto ikiwemo sekta ndogo ya mifugo ambayo alikiri kuwa pamoja na utajiri wa mifugo uliopo bado mchango wake katika pato la taifa ni mdogo.

“Sisi kama wadau wa mifugo tumepata faraja na matumaini kupitia hotuba hii. Matumaini yetu ni watendaji sasa kujipanga na kuhakikisha hakuna vikwazo katika sekta hiyo,” alisema.

Alisema pia Rais ameonesha kukerwa na vikwazo vilivyopo kwa wawekezaji na kuamua kuhamisia Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika ofisi yake huku akitaka mwekezaji kupewa kibali ndani ya siku 14. “Tunaomba hili pia liangaliwe kwa wawekezaji na wajasiriamali wadogo nao wapunguziwe vikwazo hasa kutoka mnyororo wa mamlaka za udhibiti,”

 

foto
Mwandishi: Na Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi